Muasisi wa taifa la Zimbabwe, Robert Mugabe, alizikwa Jumapili iliyopita katika makaburi ya kitaifa mjini Harare.

Wafuasi wa Mugabe walipanga foleni kutoa heshima za mwisho siku ya Alhamisi katika Uwanja wa Rufaro mjini Harare. Mke wa Mugabe, Grace, pamoja na wanafamilia wengine waliongoza waombolezaji kuuaga mwili.

Tangu alipofariki dunia mwishoni mwa wiki jana, mvutano uliibuka kati ya familia na serikali kuhusu ni wapi ambapo angezikwa. Mwisho, serikali na familia walikubaliana azikwe katika makaburi ya mashujaa ‘Heroes Acre’ yaliyoko jijini Harare.

Ingawa Rais Emmerson Mnangagwa alimtaja hayati Mugabe kama baba wa taifa, huku baadhi ya wanafamilia wakihoji ni kwa nini serikali ilitaka azikwe kwenye eneo la kuwazika mashujaa wa kitaifa wakati ‘viongozi hao hao walimdharirisha kwa kumuondoa madarakani kwa kutumia jeshi.’

Familia ilikuwa ikishikilia kwamba ingependa azikwe kijijini kwake na wala si mjini Harare. Maelfu ya waombolezaji wakivalia fulana za ZANU – PF walikusanyika katika uwanja huo kutoa heshima zao katika sehemu ambapo Mugabe aliapa kwa mara ya kwanza alipochukua madaraka mwaka 1980.

Mugabe alisimamia uchumi wa taifa hilo lililogubikwa na mfumuko wa bei, madai ya rushwa na upinzani kutoka Chama kikubwa cha siasa cha MDC.

Licha ya hayo, Wazimbabwe wengi bado wanamkumbuka kiongozi huyo wa zamani kama mkombozi wao kutoka kwa utawala wa Wazungu wachache waliokuwa wameshikilia ardhi na uwezo wa kupata elimu.

Mahali alikozikwa Mugabe

Mazishi hayo yalifuatia mgogoro kati ya familia ya Mugabe na serikali kuhusu mahali ambapo   angezikwa.

Baadaye ilikubalika kwamba angezikwa katika makaburi ya mashujaa mjini Harare.

Awali mipango ya mazishi hayo kufanyika Jumapili iliyopita ilionekana kufutiliwa mbali. Mugabe alikuwa na umri wa miaka 95 alipofariki dunia wiki iliyopita alipokuwa akitibiwa nchini Singapore.

Mugabe ni nani?

Mwaka 1980, Mugabe alishinda uchaguzi na kuwa waziri mkuu.

Mwaka 1982 aliushutumu upinzani kwa kujaribu kupindua serikali. Maelfu ya watu waliuawa alipolituma jeshi lake lililopata mafunzo Korea Kaskizini kuwakandamiza maadui zake.

Mwaka 1987, alibadilisha katiba ili imruhusu kuwa rais na kuongeza mamlaka yake. Uchumi ulidorora baada ya mwaka 2000 kuwanyang’anya walowezi mashamba.

Wakati Mugabe aliagiza kunyakua mashamba yaliyomilikiwa na watu weupe yaliyokuwa kinara wa uchumi, mfumuko wa bei ulisababisha sarafu ya Zimbabwe kukosa thamani.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2008, Mugabe alilazimika kugawana madaraka na kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai.

Ndoa yake na Grace Mugabe, aliyemzidi kwa miaka 40, yaweza kuwa sababu iliyomponza kuondolewa madarakani. Wengi walikasirishwa na Grace kuandaliwa kuwa mrithi wake.

Robert Mugabe, Rais wa kwanza wa Zimbabwe anaacha nyuma haiba ya uongozi wake wa miaka 37 katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Kuna baadhi wanampongeza kwa kuwa shujaa wa ukombozi na wengine wakimshutumu kwa kuharibu uchumi wa taifa ambalo liliwahi  kujitosheleza kwa chakula katika Bara la Afrika.

Mwaka 2017, naibu wake wa muda mrefu, Emmerson Mnangagwa, alimlazimisha kujiuzulu na kuchukua wadhifa huo wa urais.

Mwaka 2018, kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miongo kadhaa, mamilioni ya Wazimbabwe walipiga kura zao katika uchaguzi ambao Mugabe hakuwemo kwenye karatasi ya kura.

Mugabe katika uchaguzi huo alikuwa miongoni mwa wapiga kura. Lakini itakumbukwa kuwa alikuwa kiongozi mwenye maneno makali na hakukubali kustaafu kimya kimya.

Alikuwa akitetea utendaji wake alipokuwa kiongozi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Marehemu Robert Mugabe, rais wa zamani wa Zimbabwe alieleza: “Enzi hizo nilikuwa muda wote nikipigania turejeshwe kwenye utaratibu wa kikatiba, kurejeshwa kwenye sheria, kurejeshwa kwenye uhuru kwa ajili ya watu wetu, kwenye mazingira ambayo watu wetu wanaweza kuwa huru.”

Wazimbabwe wengi ambao wamezaliwa baada ya uhuru wa taifa hilo mwaka 1980, wanasema kuna ukweli katika hayo maneno.

Alikuwa shujaa, mpiganaji ambaye alifanya kila awezalo kudai uhuru wa Zimbabwe kutoka kwa Waingereza mwaka 1979. Mwanzoni kabisa, aliwasihi Wazimbabwe kufikia maridhiano baada ya miaka 15 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo ilisababisha kupatikana kwa uhuru wa taifa hilo.

Pia awali alipanua mifumo ya elimu na afya na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa zile zinazopigiwa mfano barani Afrika.

Uchumi wa nchi ulianguka baada ya kupitishwa kwa programu mpya ya umiliki wa ardhi,  hivyo kusababisha kupanda kwa mfumuko wa bei na viwango vya juu mno vya ukosefu wa ajira.

Lakini hata wakati alipokuwa akipiga kura yake mwaka 2018, alifurahishwa sana na watu wake, ambao walimshangilia na kumuita kuwa ni mzee wa ukoo, yaani GUSHUNGO.

Mugabe amezikwa katika makaburi ya mashujaa mjini Harare. Atakumbukwa na Wazimbabwe na Waafrika kwingineko barani humo.