Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abbubakar Zubery amehimiza wananchi wajiepushe na uzushi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Amewataka kutumia hekima na busara wanapopokea taarifa yoyote ili kuepuka kupotosha jamii.
Mufti alisema hayo wakati akipokea futari iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa wanawake wa Jumuiya ya Wanawake wa Bakwata Taifa (JUWAKITA).
“Hizi zama tulizo nazo kuelekea uchaguzi mkuu, fitna nyingi, unafiki mwingi, maneno mengi, kujipendekeza kwingi kuzua zua mambo kwingi, watu kutokumuogopa Mungu,” alisema.
Aliongeza: “Anaweza kusimama mtu akazungumza maneno yenye busara mazuri na yenye muongozo mzuri lakini kutokuwa makini kumsikiliza ukamtafsiri vingine, tutumie hekima zaidi na busara zaidi katika maisha ili tuweze kufanikiwa.”
“Tulicho nacho sasa hivi ni kuhakikisha tunajiandikisha ili kujiweka tayari, wakati unapofika tuweze kuingia katika kazi ya kumchagua tunayemtaka katika ngazi ya diwani, mbunge na rais,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alihimiza wanawake wajiepushe na fitna, uzushi hasa katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
“Tunapokuwa pamoja kwenye sadaka hizi, tunataka akimamama washiriki katika maombi, dua na katika kuhakikisha taifa linakuwa na amani na hasa nyakati hizi tunapoelekea kwenye uchaguzi, mivurugano ni mingii sana na uongo ni mwingi sana,” alisema Chalamila.
Wakati huo huo, alihimiza wanawake wasimame imara na wajitambue katika malezi ya watoto ili kupunguza watoto wa mitaani.
Chalamila alisema ili kuwa na kizazi chenye maadili baadaye, ni muhimu wazazi kusimamia malezi ya watoto
Zaidi ya watu 600 kutoka kata 102 za wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam wamepokea sadaka ya bidhaa za chakula kutoka kwa Chalamila ikijumuisha sukari, mchele, mafuta na tende.
