Na Mwandishi Wetu JAMHURI MEDIA, Dar es Salaam.
Wizara ya Afya imepokea msaada wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya dola za Kimarekani 488,000 ili kusaidia upimaji wa vimelea vya Malaria na magonjwa mengine kwa ufanisi zaidi ikiwa ni mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na ugonjwa huo (PMI).
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) kimekabidhiwa sehemu ya msaada huo kwa Niaba ya vyuo vilivyopo chini ya Wizara ya Afya vinavyotoa mafunzo ya kozi ya maabara vilivyopo katika Mikoa sita vitakavyofaidika na msaada huo.
Akizungumza katika hafla hiyo Bi. Anne Murphy, Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya kutoka USAID Tanzania, amesema kuwa Hadubini 133 na vitendanishi vingine vya maabara vilivyotolewa vitawezesha Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kuimarisha uwezo wa kimaabara katika uchunguzi na kusaidia utoaji matibabu ipasavyo hivyo, kusaidia kuokoa maisha ya watu na kuzuia madhara ya malaria.
Serikali ya Marekani imeipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya kutokana na juhudi zake zilizosaidia kushuka kiwango cha ugonjwa huo nchini kutoka 14% mwaka 2015 mpaka 8% mwaka 2022.
Awali akitoa salamu za ufunguzi, Mkurugenzi Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi ameshukuru kwa msaada huo uliolenga kusaidia kuendelea kupambana na kuutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.
Ameongeza kuwa msaada huo umekuja wakati muafaka kipindi ambacho Serikali kupitia Wizara ya Afya imewekeza fedha nyingi ili kuboresha huduma za afya nchini kwa kununua Dawa na vifaa tiba.