Nilidhani nimeandika kiasi cha kutosha katika mada hii, lakini kutokana na msukumo wa wasomaji wa safu hii, na watazamaji wa kipindi cha ‘Jicho la Habari’ kupitia Star TV, nilichoshiriki Jumamosi iliyopita, nimelazimika kuandika tena juu ya mada hii.
Naamini wengi tunafahamu kinachoendelea Mtwara. Kwamba Wizara ya Nishati na Madini ilipotangaza kupitia kwa Waziri wake Profesa Sospeter Muhongo, kuwa bomba la gesi litajengwa, waliingia barabarani, wakachoma nyumba kadhaa na kuharibu miundombinu likiwamo daraja la Mikindani.
Sitanii, wamechoma hadi gari la wagonjwa. Nyumba za Serikali na waandishi wa habari ndizo zikawa asusa yao. Wakailazimisha Tanzania kwa mara nyingine kutumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kudhibiti vurugu. Vijana kwa wazee wamejiandaa kupinga ujenzi wa bomba la gesi.
Ukiwa Mtwara swali unaloulizwa ni inatoka au haitoki? Ukisema inatoka, unapotezwa. Ukisema haitoki, unanunuliwa pombe. Mwanzo sentensi ilikuwa ni kwamba gesi ikienda Dar es Salaam Mtwara wanaachwaje? Jibu alilitoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa wanajengewa viwanda 57. Tayari ujenzi wa kiwanda cha saruji umeanza.
Mtwara imetengewa megawati 400 za umeme na wanaunganishiwa kwa bei ya punguzo. Vijiji vyote vya Mtwara na Lindi linakopitia bomba, wanaunganishiwa umeme. Hata hivyo, ikumbukwe gesi inayosafirishwa kwa bomba ni asilimia 16 tu ya gesi yote iliyogunduliwa. Sisikii wakizungumzia asilimia 84 iliyosalia.
Rais Jakaya Kikwete amelisemea vizuri hili. Amesema haijapata kutokea sehemu yoyote duniani, wenyeji wa eneo moja inakopatikana rasilimali wakasema ni yao na isitolewe. Ametumia lugha nzuri tu, kwamba kuifanya gesi hiyo iwe na manufaa ni lazima ifikishwe sokoni.
Sitanii, hapo ndipo nadhani kiwango cha uelewa kinapungua au kuna makundi ya watu wanaopotosha kwa makusudi wakilenga nchi yetu iingie vitani. Nchi nyingi duniani zilizogundua rasilimali kama gesi, mafuta, urani, wamepata matatizo sawa na yanayotukumba.
Wala sitahoji kama Mtwara wanakumbuka iwapo kabla ya gesi kugunduliwa, nao walikuwa wanatumia rasilimali zinazotoka mikoa mingine kwa ajili ya shule, hospitali na miundombinu mingine.
Uholanzi walipogundua mafuta, Wadachi walidhani matatizo yao yamekwisha. Wakaacha kufanya kazi. Wakawa wanashinda kwenye maandamano kuishinikiza serikali yao iwagawie fedha. Baadaye Serikali ikawadhibiti, ikatunga sheria kuwa hakuna mtu anayestahili malipo bila kufanya kazi. Mgogoro ukaisha.
Sina hata chembe ya shaka kuwa Mtwara wamepotoshwa. Wamejazwa matumaini hewa. Wanadhani gesi iliyogundulika ndiyo mwarobaini wa matatizo yao. Hawaoni tena faida ya kulima hata korosho. Wanadhani litafunguliwa dirisha wananchi wagawiwe fedha. Hii haitakaa itokee.
Sitanii, ukiliangalia kwa kina suala hili, utabaini kuwa tatizo si kwa wananchi wa Mtwara, bali tatizo ni makundi ya kimaslahi. Namaanisha nini? Makundi ya kimaslahi kwa msingi kwamba yapo makundi mengi yenye kuona bomba la gesi linaua biashara zao.
Nchi za Magharibi zinaona Tanzania inaelekea kujikoboa katika lindi la umasikini kutokana na matumizi ya gesi yaliyoinua mataifa mengi yaliyoendelea. Hili haliwafurahishi. Wanafahamu miaka 15 ijayo, Tanzania itakuwa na uchumi mkubwa kuliko nchi zote za Afrika.
Wanatutengenezea migogoro tugombane kama walivyofanya Sudan, Nigeria, Congo, Angola na kwingine. Tukigombana wanaingia hapa kwetu kwa mwavuli wa kutusuluhisha, wanachukua kila kitu.
Inawezekana baadhi ya watu hatufikiri sawasawa. Ni lazima kujiuliza Tanzania ina umaarufu upi hadi Rais Xi Jinping atembelee kwetu, siku chache baadaye Rais Barrack Obama naye aje kufuata nyayo? Mwenye macho haambiwi tazama. Rais mstaafu George Bush na mkewe nao watakuja tena nchini mwaka huu. Jiulize kuna nini?
Makundi mengine yanayochochea hizi vurugu ni wauza mafuta. Gesi ikifika hapa nchini kwao biashara ya mafuta viwandani, mitambo ya kufua umeme Tanesco na pengine kwenye magari binafsi itapungua kwa kiasi kikubwa. Hili ni tishio kwao.
Nchi nyingi zilizoendelea zinatumia ama treni za umeme au treni zinazojiendesha kwa gesi. Ukitumia gesi gharama unayotumia kwenye gari au treni kwa siku inashuka kwa asilimia 70. Imetokea hivyo kwa Kiwanda cha Saruji cha Twiga Cement na viwanda vingine vingi hapa nchini.
Sitanii, la mwisho Tanzania sasa itakuwa ni nchi ya pili duniani kwa kuzalisha urani (uranium). Nchi ya kwanza ni Kazakhstan wanazalisha wastani wa tani 19,000 kwa mwaka, ikifuatiwa na Canada inayozalisha wastani wa tani 9,500 kwa mwaka.
Pale Nantumbo, Tanzania itazalisha tani 14,000 kwa mwaka. Bado hujataja Bahi, kule Dodoma na maeneo ya Singida. Je, kwa ufupi unadhani rasilimali kiasi hiki haziwatoi udenda waroho? Nasema jibu unalo.
Nahitimisha kwa kuwapongeza wahariri wote Tanzania kwa kuamua kukataa kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi katika suala hili la Mtwara kwa maslahi ya Taifa. Nasema tukatae vurugu kwa gharama yoyote, na Serikali inao wajibu wa kulinda maisha ya wananchi.