Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songwe
Mahakama ya Wilaya ya Momba Imemhukumu Bw Esau Andrew Hinjo aliyekuwa Askari wa SUMA JKT-Tunduma adhabu ya kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh. 500,000 kwa kosa la kuomba na kupokea hongo kinyume na Kifungu cha 15(1) (a) na 2 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2022.
Hukumu dhidi ya Esau Andrew Hinjo imetolewa katika Kesi ya Rushwa Na.23763/2024 Agosti 21, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Claud Msenjelwa wa Mahakama ya Wilaya ya Momba.
Kesi hiyo imeendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Lilian Matara.
Ilielezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa shtaka la kupokea hongo kiasi cha sh.120,000/- toka kwa Joseph Itera Chunche kama kishawishi cha yeye kutokamata nyavu haramu za kuvulia Samaki.
Mshtakiwa alikiri makosa yake na kulipa faini ya sh.500,000.