Mazingira yanajumuisha, kwa mujibu wa Uislamu, vyote vinavyomzunguka mwanadamu, akiwa ni msimamizi. Ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayostahili kuenziwa na kutunzwa ikiwa ni sehemu ya kuonyesha shukrani zetu kwa Mwenyezi Mungu kwa neema hizi zisizo na mfano.
Kama anuani ya makala hii inavyojieleza, tunalenga kuangazia mafunzo ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) juu ya mazingira na utunzaji wake, tukizingatia ukweli usio na shaka kuwa mazingira ni miongoni mwa neema alizotuneemesha nazo Mola wetu Mlezi tunazopaswa kushukuru, kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 36 (Surat Yaa-Siin) Aya ya 33 hadi ya 35 kuwa:
“Na ishara hiyo kwao – ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila! Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukachimbua chemchem ndani yake, ili wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?”
Mwenyezi Mungu Mtukufu Ameiumba Ardhi na mazingira yote, kwa ujumla wake, kwa hali nzuri, bora na kwa kiwango kinachotosheleza mahitaji ya wanadamu na viumbe wengine na kwamba upungufu wowote unaotokea au uharibifu, basi chanzo chake ni shughuli za uharibifu na ufisadi zinazofanywa na wanadamu wenyewe kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 30 (Surat Ar-Ruum) Aya ya 41 kuwa: “ Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu.”
Mtume Muhammad ametoa mafundisho muhimu juu ya mazingira na umuhimu wa kuyatunza, akigusia vipengele mbalimbali vya mazingira vikiwemo; maji na hewa, upandaji wa miti, utunzaji wa njia (barabara) na kadhalika.
Kuhusu maji na hewa, sote tunafahamu thamani na umuhimu wa neema hizi mbili kwetu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatubainishia hayo katika Qur’aan Tukufu Sura ya 16 (Surat An-Nahl) Aya ya 10 na 11 kuwa: “Yeye ndiye anayekuteremshieni maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia. Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni na mitende, na mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu wanaofikiri.”
Kwa kuzingatia umuhimu na thamani ya maji na hewa, Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amekataza kujisaidia katika maji yaliyotuama; amekataza kutumia hovyo maji (Israfu) hata wakati wa kuchukua udhu au kukoga kwa lengo la kufanya ibada; amekataza pia kufanya dhara lolote kwake mtu binafsi au kwa viumbe na mazingira ikiwemo uchafuzi wa hewa.
Ieleweke kuwa jambo lolote linalofanywa na wanadamu na linaharibu mazingira iwe ni uchafuzi wa maji au hewa, basi jambo hilo linakwenda kinyume cha mafundisho ya Mtume Muhammad.
Tunasoma katika Hadiith (jambo lolote linalohusishwa na Mtume Muhammad iwe kauli yake, kitendo chake au kukubali kwake jambo lililofanywa) ya Mtume Muhammad kuwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Ziogopeni laana mbili.” Wakauliza: “Ni zipi laana mbili Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: “Kwenda haja mtu katika njia wanayopita watu au kivuli chao (wanapopumzika).
Katika Hadiith nyingine zimetajwa sehemu tatu nazo ni; sehemu ambayo ni rasilimali, njia wanayopita watu na kivuli ambacho watu hupumzika.
Tunaona hapa Mtume Muhammad akitukataza kuchafua mazingira katika sehemu hizi tatu muhimu kwa mahitaji ya wanadamu.
Kuhusu upandaji wa miti, Mtume Muhammad amesisitiza kupanda miti ikiwemo mitende ili kupata faida ya uzuri wa mazingira, matunda na vivuli, na kwamba mtu anapopanda mti kisha wakala matunda ya mti huo wanadamu, ndege na wanyama bila ya idhini yake, basi huhesabiwa ni sadaka na Mwenyezi Mungu humlipa malipo makubwa.
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesisitiza upandaji wa miti kwa kiwango cha kumtaka mtu ambaye atakuwa katika wakati mgumu katika siku ya tukio la mwisho wa dunia (Qiyama) kwamba wakati huo pamoja na uzito wa siku hiyo akiwa na mche wa mti katika mkono wake basi na aupande.
Ni dhahiri hakuna namna bora ya kupima umuhimu aliouelezea Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) juu ya kusisitiza upandaji miti kuliko mfano huu.
Mtume ametushajiisha kupanda miti kwa msisitizo wa kupata ujira (thawabu) endelevu kwa muda wote ambao mti ule utakuwepo hata kama mpandaji atakuwa amekufa na kwamba ataendelea kulipwa ujira wa kupanda mti huo hadi Siku ya Qiyama.
Hili la kupata thawabu endelevu hadi siku ya Qiayama linawahusu pia wale wanaohuisha mapori yaliyokufa ili miti yake iendelee kumea na kusaidia kupatikana kwa hewa safi, mvua za kutosha na mazingira mazuri ya kufurahisha.
Ikumbukwe kuwa miongoni mwa mambo yanayomletea mtu thawabu ni kuyaweka mazingira katika hali ya usafi kama vile kuondoa chochote chenye kuleta maudhi au madhara kwa wanadamu barabara.
Mtume Muhammad alimuelezea mtu mmoja aliyebahatika kuzawadiwa kuingia peponi kwa sababu ya kuukata mti uliokuwa unawaletea adha wapita njia.
Linalozungumzwa ni kuondoa njiani chochote ambacho kuwepo kwake kunaleta maudhi au madhara kwa binadamu na viumbe wengine, ikiwemo uchafu katika mazingira yetu, iwe barabarani, katika mitaro na mito na kadhalika ambavyo tumeshuhudia mara kadhaa vikisababisha mafuriko na majanga mengine ikiwemo maradhi ya mlipuko.
Ieleweke kuwa unapochunguza maisha ya Mtume Muhammad utabaini falsafa yake ya kumfundisha mwanadamu kuishi maisha rafiki na mazingira yake na vinavyokusanywa na mazingira hayo kwa imani kuwa mwanadamu na mazingira yanayomzunguka ni viumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba kila kilichoumbwa kuna hekima na kusudi la kuumbwa kwake ambalo halina budi kutimizwa.
Qur’aan Tukufu inatuwekea wazi hili tunaposoma Sura ya 46 (Surat Al-Ahqaaf) Aya ya 3 kuwa: “Hatukuziumba Mbingu na Ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na waliokufuru wanayapuuza yale wanayoonywa.”
Falsafa hii inaelekeza umuhimu wa kuyatendea wema mazingira na kwamba ingawa mwanadamu amepewa usimamizi lakini yeye si mmiliki wa dunia na vilivyomo, yeye si mmiliki wa mazingira mwenye kuamua kipi kiwepo na kipi kisiwepo. Mmiliki pekee ni Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba tukifuata muongozo wake tutafaulu kuepuka majanga ya kimazingira na kinyume chake tutaonja madhara.
Nihitimishe makala hii kwa kuweka wazi mtazamo wa Mtume Muhammad juu ya utunzaji wa mazingira ambao ni misingi mitatu:
Msingi wa kwanza ni sehemu ya faida. Uislamu unawahimiza watu kutumia na kuhifadhi mazingira ili faida itokanayo na utunzaji wa mazingira iendelee kupatikana. Mtume ametutahadharisha hata kuua ndege kimchezo bila ya haja ya kumla kwa kusema: “Mtu yeyote anayeua ndege bure, (ndege huyo) atapiga kelele Siku ya Qiyama akisema: Ewe Mola, hakika fulani ameniua bure, wala hakuniua kwa ajili ya kufaidika.”
Msingi wa pili ni sehemu ya uzuri. Mazingira yakitunzwa ni sehemu ya uzuri wa mandhari ya dunia hii na kuna Aya kadhaa za Qur’aan Tukufu zinazoelezea uzuri wa mimea, bustani na kadhalika. Mtume Muhammad ametufundisha kuwa: “Mwenyezi Mungu ni Mzuri na Anapenda vizuri.” Hivyo tuna wajibu wa kutunza mazingira ili kulinda uzuri wake tutakaoufurahia na kukumbuka neema za Mungu Mwenyezi.
Msingi wa tatu ni mazingira safi ya kimaumbile. Mtume Muhammad kwamba viumbe walio katika mazingira ni umma unaomtukuza Mwenyezi Mungu kama tulivyo sisi wanadamu, na kwamba wana haki ya kupata hifadhi na si kuangamizwa au kuuawa isipokuwa kwa masilahi maalumu yaliyofikiriwa. Mtume Muhammad alipata kueleza kisa cha mtume mmoja aliyeng’atwa na sisimizi akisema: “Mtume mmoja miongoni mwa mitume aling’atwa na sisimizi mmoja, naye akaamrisha kuuawa sisimizi wote waliokuwepo katika kijiji alichokuwa anaishi. Mwenyezi Mungu akamuuliza: “Kung’atwa kwako na sisimizi mmoja, umeangamiza umma wa sisimizi unaomtukuza Mwenyezi Mungu?” Kuthibitisha hilo tunasoma katika Qur’an Tukufu Sura ya 6 (Surat Al-An-aam) Aya ya 38 kuwa: “Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi (tunadhibiti kila wafanyalo). Hatukupuuza Kitabuni (mwetu) kitu chochote. Kisha watakusanywa kwa Mola wao Mlezi.”
Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Simu: 0713603050/0754603050