Katika Rufaa ya Jinai Namba 273 ya 2017, kati ya GODFREY GABINUS @ NDIMBA na YUSTO ELIAS NGEMA •••..•.•.•••••.••••.•••.••••.•••• APPELLANTS
Na EXAVERY ANTHONY @ MGAMBO dhidi ya JAMHURI (haijaripotiwa), hukumu ya Februari 13, mwaka huu (2019) majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wanaeleza kanuni tano ili ushahidi wa kumtambua mtu umtie mtuhumiwa hatiani.
Lakini kabla ya hayo, ushahidi wa utambuzi ni nini? Ushahidi wa utambuzi ni ushahidi ambao mtuhumiwa aliweza kutambuliwa wakati akitenda kosa. Mathalani mtu anaiba au anaua na katika kitendo hicho akashuhudiwa na mtu fulani. Inawezekana kuwa alitambuliwa na mtendewa wa tukio (victim) ama mtu mwingine yeyote.
Aidha, kumtambua mtu akitenda kosa ni wakati wowote inaweza kuwa mchana, jioni ama usiku, na anaweza kutambuliwa mtu husika akiwa peke yake wakati wa kutenda kosa au wakiwa wengi, hasa katika makosa ambayo hutendwa na watu wengi.
Zifuatazo ni kanuni tano za mahakama ili mtuhumiwa apatikane na hatia au aachiwe huru kwa ushahidi wa utambuzi:-
Kwanza, muda ambao shahidi aliweza kumtambua mtuhumiwa akitenda kosa. Kama ilikuwa usiku na hakuna mwanga basi ushahidi huu hupungua uzito, na kama ilikuwa mchana, ushahidi huu huongezeka uzito. Kwa maana kuwa ikiwa usiku na hakuna mwanga uwezekano wa kumtambua mtu kwa makosa ni mkubwa zaidi, hivyo kuleta shaka katika utambuzi. Wakati ikiwa mchana uwezekano wa kumtambua mtuhumiwa bila kukosea ni mkubwa zaidi.
Pili, umbali kati ya shahidi na mtuhumiwa aliyetambuliwa, kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alikuwa umbali gani kutoka alipokuwa shahidi. Umbali ukiwa mkubwa maana yake utambuzi unakuwa hafifu, hivyo kuleta shaka katika uwezekano wa kumtambua mtu kwa usahihi. Wakati umbali ukiwa mdogo au karibu, maana yake uwezekano wa utambuzi kuwa madhubuti ni mkubwa, hivyo kuondoa shaka.
Tatu, jem kulikuwa na mwanga? Iwe ilikuwa usiku au mchana suala la kama kulikuwa na mwanga linazingatiwa. Hata mchana wakati mwingine tukio linaweza kutokea sehemu pasipo na mwanga, mfano chumbani kama milango na madirisha vimefungwa, ama pengine ambapo hakukuwa na mwanga.
Kama kulikuwa na mwanga wa kutosha maana yake utambuzi ni rahisi, hivyo kuepuka uwezekano wa shaka katika utambuzi, na kama hakukuwa na mwanga wa kutosha ni kinyume chake.
Nne, aina ya mwanga. Mwanga wa umeme wa taa ya kawaida na mwanga wa kibatari ni tofauti. Kadhalika mwanga wa mwezi na mwanga wa jua la mchana ni tofauti. Lakini pia hata huo mwanga wa umeme nao hutofautiana. Mwanga wa umeme wa taa hafifu kama zile zitumikazo kwenye kumbi za starehe ni tofauti na mwanga wa taa za kawaida za majumbani. Hivyo itakapothibitika kuwa hakukuwa na mwanga au mwanga uliomtambua mtuhumiwa ulikuwa hafifu usiotoa nafasi ya kuona vizuri, tafsiri yake uwezekano wa kutambua kimakosa ni mkubwa, wakati ikithibitika kulikuwa na mwanga wa kutosha usio hafifu, basi uwezekano wa kutambua ni mkubwa na pengine usio na shaka.
Tano, je, shahidi alimfahamu mtuhumiwa kabla ya tukio? Maana yake kuachana na siku hiyo alipomuona mtuhumiwa akitenda kosa, je, kabla ya hapo alikuwa akimfahamu? Kama alikuwa akimfahamu, maana yake utambuzi wake ni wa kuaminika, kwa kuwa mtu unayemfahamu kabla ni rahisi sana kumtambua hata akiwa mbali, kwa sababu ni mtu ambaye ni hadhiri kwako (familiar).
Wakati, kama ulikuwa humjui kabla ya tukio, kwa maana kuwa siku unamuona akitenda tukio ndiyo ilikuwa siku ya kwanza, basi tafsiri yake uwezekano wa kukosea katika kumtambua unaweza kuwa mkubwa.
Kwa hiyo kila kimoja katika hivi kitapimwa na kuangaliwa kwa uzito wake ambapo kimojawapo kikionekana kutoridhisha maana ushahidi wa utambuzi umekosa nguvu na mtuhumiwa anaweza kuachiwa huru.