Tajiri mkubwa barani Afrika Aliko Dangote amewashangaza watu wengi wa Nigeria baada ya kusema hana nyumba nje ya nchi hiyo.

Dangote alisema alikuwa na nyumba mbili – katika mji aliozaliwa wa Kano, na Lagos – na aliishi katika nyumba ya kukodi kila anapotembelea mji mkuu, Abuja.

Aliorodheshwa na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi nchini humo.

Utajiri wake ulipanda kwa $400m zaidi mwaka jana, na kumpa thamani ya jumla ya $13.9bn (£10.7bn), Forbes walisema wakati huo.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijitajirisha kwa saruji na sukari – na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha uchumi cha Nigeria, Lagos.

Mfanyabiashara huyo alibainisha hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote Jumapili.

Maoni yake yaliwashangaza wengi katika nchi ambayo watu matajiri wana sifa ya maisha ya kifahari.

Wanigeria wengi matajiri wanamiliki nyumba London, Dubai na Atlanta.

Matamshi yake yamezua hisia nyingi kwenye mitandao ya kijamii, huku wengine wakisema ni uamuzi wa busara wa kibiashara kwani ni nafuu kulipa kodi kuliko kununua nyumba.

Bw Dangote alisema sababu ya uamuzi wake ni kwamba anataka kuona Nigeria inakua.

“Sababu ya kutokuwa na nyumba London au Marekani ni kuwa nilitaka kuangazia ukuaji wa viwanda nchini Nigeria,” alisema.

“Nina shauku kubwa juu ya ndoto ya Nigeria na kando na nyumba yangu ya Lagos, nina nyumba nyingine katika jimbo langu la Kano, na nyingine ya kukodi huko Abuja.

“Ikiwa nitakuwa na nyumba kote Marekani na kwingineko, singeweza kutuliza akili na kufanya kitu kwa ajili ya watu wangu.”

Bw Dangote anajulikana kumiliki makazi ya kifahari katika Kisiwa cha Banana maarufu cha Lagos, ambako Wanigeria wengi wenye hadhi ya juu pia wana majumba ya kifahari.

Mchanganuzi wa masuala ya umma Sani Bala alisema Bw Dangote alikuwa akionyesha mfano mzuri sana.

“Wanaijeria wanahitaji kuelekezwa upya kuelewa kumiliki majumba kadhaa sio mafanikio wakati pesa zingehitajika mahali pengine.

“Dangote alisema aliuza nyumba yake huko London mnamo mwaka 1996 na nina uhakika pesa zilizopatikana kutokana na mauzo zilirejeshwa katika biashara yake – huo ndio mfano wa kuiga