Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye Wande Shija, mkazi wa Mtaa wa Mbagala B Kitongoji cha Magharibi kwa tuhuma za kumnywesha sumu mtoto mchanga wa siku moja wa jirani yake.
Akizungumza kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi, mama wa mtoto huyo aitwaye Kashinje Julias , mkazi wa mtaa wa Mbagala B, amesema kuwa tukio hilo limetokea Machi 19, 2024, majira ya saa 9, mchana alipokwenda bafuni kuogeshwa na dada yake aliyemtaja kwa jina la Flora Elias mara baada ya kutoka hospitalini.
Amesema kuwa baada ya kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Igunga, aliongozana kwenda nyumbani kwake akiwa na dada yake.
“Tulipofika nyumbani dada Frola alichemsha maji ya moto ya kuoga na yalipokuwa tayari alikwenda kuniogesha bafuni na kumwacha mtoto chumbani akiwa amelala.
” Wakati tukiendelea kuoga ghafla tulisikia kilio kikali cha mtoto na kuamua kuvaa nguo kwa haraka.
“Tulipofika chumbani mtoto aliendelea kulia kwa mfululizo na dada alipombeba alisikia harufu kali bila kujua ni nini na inatoka wapi.
“Mimi na dada tulianza kumnusa mtoto mwilini na ndipo tulipobaini kuwa mdomoni kuna harufu kali ambayo hatukuweza kufahamu kwa haraka ni nini.
“Kutokana na kitendo hicho tulishikwa na bumbuazi kwani hatukujua ni kitu gani kimetokea na kwa nini mtoto alikuwa akilia sana tena sana binafsi nilishikwa na uchungu kana kwamba ni mjamzito tena” amesema kwa uchungu.
Amesema kuwa wakati tukio linatokea kulikuwa na watu wanne ambao ni dada Flora, mdogo wake aitwaye Maria Daniel na jirani yao aliyefahamika kwa jina la Wande Shija,.
“Dada alimbeba mtoto na kutuamuru kwa sauti ya ukali wote kwenda hospitalini kisha Polisi ambako tuliamini kuwa tunaweza kufahamu kilichomsibu mtoto na nani aliyempa kitu mdomoni.
“Baada ya kufika hospitali haraka tulipewa huduma ya kwanza ambapo madaktari walifanya jitihada mbalimbali za kuokoa maisha ya mwananhu.
” Wakati juhudi hizo zikiendelea manesi watatu walitukalisha chini na kuanza kutuhoji kwa pamoja na kisha mmoja mmoja ambapo masaa mawili yalikuwa ni mahojiano tu.
“Kutokana na mahojiano hayo ndipo jirani yetu Wande alikiri kumnywesha sumu mtoto wangu, sikuamini baada ya manesi kusema kifupi niliumwa ghafla na sikujua huyo jirani yetu nimfanye nini wakati huo, mimi walinishika na nililia sana sikujua kosa langu nini kwake.
Mganga Mfawizi Hospitali ya Wilaya ya Igunga Melchades Magongo amesema kuwa walimpokea mtoto huyo Machi 19, 2024 akiwa anatapika na kushindwa kupumua vizuri na mdomoni akiwa ananukia harufu idhaniwayo kuwa ni sumu.
“Ni kweli tumempokea mtoto huyo mchanga akiwa katika hali mbaya huku akitapika na kushindwa kupumua na mdomoni akiwa na harufu kali ya sumu.
“Tulimuanzishia matibabu ya kurudisha kupumua vizuri na kuzuia kutapika na kurudisha hali ya mwili kuwa na nguvu, ilifikia hutua mtoto akapata degedege na joto kupanda hivyo tuliendelea na juhudi za kuokoa maisha yake na tukachukua vipimo kwa ajili ya uchunguzi zaidi” amesema.
Ameongeza kuwa pamoja na jitihada kubwa zilizofanyika lakini Machi 29, saa 8 mchana alifariki dunia na Machi 30, 2024 sampuli zilichukuliwa sampuli katika baadhi ya viungo vyake na kupelekwa kwa mkemia mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao amekiri kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo na atafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa upelelezi ikiwa ni pamoja na kutoa majibu ya sampuli zilizopelekwa mkemia mkuu.