Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Zanzibar
MTOTO wa gwiji wa muziki wa Afrika, Hayati Oliver Mutukudzi, Selmor Mutukudzi amekonga nyoyo za mashabiki mbalimbali waliofurika viunga vya Ngome Kongwe ndani ya Mambo Club Unguja, Zanzibar, katika usiku wa tamasha la 21, lililoanza leo Februari 9-11, 2024.
Selmor Mutukudzi ambaye alipanda jukwaani na bendi yake, aliweza kuanza na vionjo vya nyimbo maarufu za Baba yake ikiwemo‘Neria’ na Todii’ ambavyo viliamasha hisia za mashabiki wengi waliolipuka kwa shangwe na kuimba nae pamoja.
Kando ya jukwaa hilo, awali, Selmor Mutukudzi amesema kuwa, ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kushiriki tamasha la Sauti za Busara ambapo amekuwa akituma maombi ya kushiriki ila akikosa nafasi.
‘’Nimekuwa, nikiomba kushiriki Sauti za Busara, muda mrefu ila nikikosa nafasi. Nashukuru kwa mwaka huu kwani imenipa hali kubwa ya kuonesha owezo wangu.
Selmor Mutukudzi kipaji chake kilioneka tokea akiwa na miaka 10, baada ya baba yake kumuingiza kwenye muziki na kuonesha nyota yake ambapo akaweza kuwa na nyimbo mbalimbali ikiwemo Albamu aliyoipa jina la ‘Shungu’ aliyoitoa mwaka 2008 huku ikiwa na nyimbo kama Chiro,Iwewe, Neni, Shungu na kibao cha Handiende.
Hadi sasa ameweza kufikisha Albamu Sita ambazo zikiwa na nyimbo mbalimbali, aidha mbali ya muziki pia ni mwanaharakati wa utetezi wa mabinti wa kike na hata kuungana kuimba wimbo wa ‘’Strong Girls’’ ikiwa ni harakati za kutetea mabinti hao Afrika .