Na isri Mohamed, JamhuriMedia, Manyara
MTOTO wa miaka nane, mwanafunzi wa darasa la pili wa shule ya msingi Maisaka mjini Babati mkoani Manyara, amekutwa amejinyonga kwa kutumia mkanda juu ya mti wa mstafeli uliopo nje ya nyumba yao.
Taarifa za awali zinadai kwamba chanzo cha mtoto huyo kujinyonga ni migogoro ya wazazi wake ya mara kwa mara ambapo mara ya mwisho mama aliamua kuondoka nyumbani na kuwaacha na baba yao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mruki, Abdillah Rajab, amesema tukio hilo limetokea Machi 16, 2024 majira ya saa 7, mchana, ambapo pia amethibitisha wazazi wa marehemu kuwa na tabia ya kugombana mara kwa mara mbele ya watoto sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mwenyekiti amesema mara ya mwisho kugombana, baba mzazi wa marehemu anayefahamika kwa jina la Adam Abdallah alimpokonya mkewe ufunguo wa nyumba mbele ya watoto wao.
Kwa upande wake Baba wa marehemu amekiri kuwepo kwa ugomvi wa mara kwa mara kati yake na mkewe ambao watoto wamekuwa wakiushuhudia lakini hakutarajia kama ungeweza kuleta athari kubwa kiasi hiko.
Mwili wa mtoto huyo umechukuliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.