Mwanafalsafa William Arthur Ward anasema, “Shukrani inaweza kubadili siku za kawaida kuwa siku za shukrani, kubadili kazi za kila siku kuwa furaha, na kubadili fursa za kawaida kuwa baraka”.
Kwa msingi huo, nawashukuru wasomaji wangu wote wa makala ya wiki iliyopita iliyokuwa ikisema ‘Kuporomoka kwa maadili nani alaumiwe?’
Leo ninaomba nizungumzie makuzi na malezi bora kwa watoto. Katika dunia ya leo na ijayo, malezi na makuzi bora kwa mtoto ni wajibu na hitaji la msingi. Mtoto ni malezi, uliandaliwa vyema na wazazi/walezi wako nawe pia huna budi kumwandaa vyema mtoto wako.
Malezi bora ni kutengeneza kesho njema ya mtoto. Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia. Maisha ya mtoto wako na msingi uliompa leo ndiyo utakaowezesha maisha bora ya mama na baba bora wa baadaye.
Baba mwema na mama mwema wanaandaliwa leo. Kama tunataka kujenga Taifa imara lenye weledi na umahiri na uwezo wa kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa sasa, basi ni lazima tuwekeze kwa watoto. Dunia ya kesho inatudai. Haitudai pesa, haitudai barabara, haitudai bandari, inatudai mbegu ya maadili bora. Malezi yana nguvu ya kuibomoa jamii au kuijenga. Ni lazima sisi kama wazazi na walezi tuwe tayari muda wote kutoa malezi yanayoiunganisha jamii badala ya kuibomoa. Tuko kwenye karne ambayo watoto wengi wanapata malezi ya wazazi pekee.
Wanakosa malezi shirikishi ya jamii inayowazunguka. Hili ni somo, ni lazima tuanze kutoa malezi shirikishi. Tutoe malezi yanayolenga kujenga jamii inayosikilizana. Malezi ni shule ambayo tunaweza kuitumia kupandikiza roho ya upendo kati ya mtu na mtu, kati ya familia na familia, kati ya taifa na taifa, na kati ya bara moja na bara jingine.
Tuzibe ufa kabla ya kujenga ukuta. Kila mzazi na mlezi, na mwanajamii awe tayari kuwa daraja la mawasiliano ya kutoa habari njema kwa jamii. Dunia inalilia amani. Hakuna jamii inayoweza kuwa rafiki wa dunia yenye amani kama haitoi malezi bora kwa watoto wao.
Tunaishi katika ulimwengu ambao kwa nyakati fulani hauna huruma kabisa. Dunia ya leo inatamani kuishi bila Mungu. Imefika mahali mwanadamu anafikiri kwamba, kuna mambo mengine ambayo Mwenyezi Mungu aliyapanga kimakosa au aliyaweka kwa kusahau. Inatia huruma. Ninaweza kuandika kufuru nyingi za mwanadamu juu ya Muumba wake, lakini kalamu yangu inanielekeza kuandika; malezi bora ni chanzo cha habari njema katika uso wa dunia ya leo na ijayo. Wazazi, walezi na wanajamii wote tujitahidi kuwa waenezaji wa sera ya malezi bora katika jamii na Taifa letu.
Katika dunia ya leo iliyojaa kila aina ya sauti na purukushani za kila namna, sisi kama wazazi na walezi tunahitajika kujitambua kwamba tunao wajibu wa kuondoa njaa na kuleta shibe. Kuondoa umaskini na kuleta utajiri. Kuondoa maradhi na kuleta afya njema. Kuondoa ujinga na kuleta uelevu. Kuondoa mashindano na kuleta ushirikiano. Kuondoa utengano na kuleta umoja. Kuondoa uchonganishi na kuleta upatanisho. Kuondoa unyonyaji na kuleta ukarimu. Kuondoa ukandamizaji na kuleta usawa. Kuondoa upweke na kuleta faraja. Kuondoa wivu na kuleta kutakiana mema. Kuondoa hasira na kuleta huruma. Kuondoa dhuluma na kuleta haki. Kuondoa ubwanyenye na kuleta unyenyekevu. Kuondoa uhasama na kuleta uelewano. Kuondoa uadui na kuleta urafiki. Kuondoa vita na kuleta amani. Kuondoa kukata tamaa na kuleta matumaini. Kuondoa kifo na kuleta umilele. Huo ni wajibu wetu.
Jamii yetu ya Kiafrika imeusaliti utamaduni wake. Afrika ni yetu. Wa kuiua ni sisi na wa kuijenga ni sisi. Taifa ambalo limetupilia mbali mafunzo ya utamaduni wake ni kama taifa ambalo limetupilia mbali moyo wake. Tujiulize!
Lugha za kikwetu zimekwenda wapi? Viko wapi vitabu vilivyoandikwa kwa lugha za kikwetu? Taaluma za mababu zetu ziko wapi sasa? Nani hivi leo anayeweza kutuimbia nyimbo za ngoma za kikwetu na kutueleza mafundisho yaliyomo? Nani hivi leo anaweza kutupigia muziki kwa vyombo vile vya zamani vitoe sauti kama ya kijana akimposa mchumba wake anapotoka kuteka maji mtoni? Nani hivi leo anayeweza kupiga mbiu ikatoa sauti ya kumtoa nyoka pangoni? Desturi zetu, mila zetu, ujamaa wetu, vyote tumeviangamiza kwa visingizio vya ukisasa.
Hakuna njia ya kujifundishia historia pasipo kufahamu shina la historia yenyewe. Jamii yoyote ile ni lazima itembee katika ukweli, haki, maadili, mwanga na elimu. Hakuna jamii inayoweza kuendelea pasipo watu wake kuwa wakweli na wenye maadili na akili tafakari na akili bainifu.
Kumbuka, tunazungumzia malezi na makuzi bora kwa mtoto. Hatuwezi. Na tena hatuwezi kuwa Taifa lenye nidhamu bora katika utawala, siasa, uchumi pasipo maadili bora. Jamii isiyojali mustakbali wake ni jamii kipofu, ni jamii inayoelekea kufutika katika uso wa dunia.
Dunia yetu itageuka kuwa paradiso ya duniani kama wazazi na walezi watatoa malezi na makuzi bora kwa watoto wao na jamii inayowazunguka. Malezi bora yanajenga jamii salama yenye watu salama. Malezi bora yanajenga taifa salama lenye watu salama. Malezi bora yanajenga dunia salama yenye watu salama.
Uhodari wa kuishi si uhodari wa kuishi miaka mingi, la hasha! Ni uhodari wa kuwa msaada katika jamii inayokuzunguka na ulimwengu kwa ujumla wake. Tutafanikiwa kiroho, kimaadili, kisiasa, kijamii na kiuchumi endapo kila mtu atawajibika kufanya kazi kwa maadili mema na kwa nafasi yake aliyopo. Mama awajibike katika kutoa malezi bora ya kifamilia.
Baba awajibike katika kutoa malezi bora katika familia. Ni ukweli usiohitaji hoja kwamba maisha ya kimaadili ya kibinadamu na uwezo wake wa kupenda, yanaamshwa kwanza na upendo wa wazazi. Mchungaji A.W. Tower alipata Kunena haya, “Malezi bora kwa mtoto ni lulu kwa ulimwengu.”
Kesho bora ya mtoto inajengwa na leo bora ya mzazi bora. Methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya, “Samaki mkunje angali mbichi.” Itakuwa ni biashara isiyolipa kumkunja samaki akiwa mkavu. Atavunjika, na utapata hasara ambayo pengine hukutegemea kuipata.
Nakubaliana na Frederick Douglass kusema, “Ni rahisi sana kujenga watoto imara kuliko kukarabati watu wazima waliovunjika.” Mzazi au mlezi unatakiwa uwe mlezi saa ishirini na nne. Unatakiwa uwe mlezi siku saba za wiki. Unatakiwa uwe mlezi siku 30 za mwezi. Unatakiwa uwe mlezi siku 365 za mwaka. Malezi hayana likizo. Malezi ni utumishi. Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia. Tafakari kesho ya mtoto wako umeiandaaje. Jielewe kwamba wewe ni mzazi na mlezi. Chukua nafasi yako kama mzazi.
Mtoto anapozaliwa ni kama malaika. Hana kosa anapokuwa amezaliwa. Anakuwa mgeni aliyeleta habari njema kwenye familia. Wazazi, ndugu na jamaa hufurahi kumpokea mtoto aliyezaliwa.
Tunapokuwa tunazungumzia maadili ya ulimwengu wa sasa kwamba yameyumba lazima kwanza tutupie jicho letu kwenye familia zetu. Tunatoa malezi ya aina gani kwenye familia zetu? Ya kujenga au kubomoa? Jibu tunalo sisi wenyewe walezi na wazazi. Tuelewe kwamba jukumu la kujenga Taifa letu ama kulibomoa tunalo sisi wazazi, walezi na wanajamii.
Ustawi wa Taifa unaanzia nyumbani. Kinyume chake ni kweli. Kuporomoka kwa Taifa kunaanzia nyumbani. Ni methali ya Kiafrika. Uhai wa taifa unategemea uhai wa familia. Tunapaswa kutambua kuwa mafanikio ni tunda la bidii. Methali ya Kichina inasema hivi, “Ukinieleza nitasahau, ukinionesha nitasahau, bali tukishirikiana nitaweza.”
Ni hakika wazazi na walezi wana ulazima wa kushirikiana katika malezi na makuzi ya watoto. Papa Yohana Paul wa II alipata kuandika hivi, “Namna familia inavyoenda, ndivyo taifa linavyoenda na ndivyo dunia yote inavyoenda.”  Kinachomtofautisha mzazi bora na bora mzazi ni malezi anayotoa katika familia yake.
Tusizae kwa sababu tunaweza kuzaa. Tuzae kwa sababu Mwenyezi Mungu ametupatia nguvu ya kimaadili ya kuwalea watoto wetu. Tusikubali kuwa wazazi wa kuzaa na kuwatelekeza watoto wetu. Tukubali kuwa wazazi na walezi bora kwa sababu Mwenyezi Mungu ametuamini sana na ametupatia mamlaka ya kuwa wazazi na walezi bora. 
Ukosefu wa malezi na makuzi bora kwa motto, kunamfanya asiwe na uwezo wa kujitambua yeye ni nani kati ya walimwengu, hali hiyo inamfanya asiwe na uhimili wa kiakili na wa kiutashi wa kutafakari na kusimamia malengo aliyonuia kuyatekeleza katika maisha yake.
Tunaweza kuwa na watoto wengi katika Taifa letu lakini wakawa ni watoto ambao ni walemavu wa kifikra, kimaadili na kizalendo. Hatuhitaji kuwa na watoto wengi wenye ulemavu wa kifikra na kimaadili. Tunahitaja kuwa na watoto wengi katika Taifa letu wenye ukomavu wa kimaadili, wenye hofu ya Mwenyezi Mungu na walio na uwezo wa kuibadilisha dunia kutoka kwenye sura ya vita kwenda kwenye sura ya amani.

0789 090828 au 0719 700446