NA BASHIR YAKUB
Watoto ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 nao hushitakiwa mahakamani. Wanaweza kushitakiwa kwa jinai au madai. Isipokuwa tofauti na wakubwa ni kuwa hawa wanazo Mahakama zao.
Sheria Namba 21 ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 97(1) kinaanzisha Mahakama za Watoto. Makosa ya ukorofi, kukosa usikivu, matunzo, usalama wa mtoto, wizi, kubaka, matusi, kujeruhi, mauaji, kuharibu mali na mengine ya jinai mnayoyajua hushughulikiwa hapa kwa mujibu wa kifungu cha 98b (1) cha sheria hiyo.
Tutaona hapa chini utaratibu tangu mtoto kufikishwa mahakamani hadi kuhukumiwa. Marejeo yote katika makala ni kutoka Sheria Namba 21, Sheria ya Mtoto ya 2009.
-
Mtoto anavyofikishwa mahakamani
Mtoto anaweza kufikishwa mahakamani na polisi, mzazi, mlezi au yule mtu aliyemkosea/mtendewa. Na ikiwa Mahakama itatumia wito (summons) ya kumtaka kufika mahakamani basi mtoto au mzazi, mlezi ndiye atasaini wito huo na kumfikisha mtoto mahakamani katika tarehe iliyopangwa.
-
Mtoto kusomewa shitaka
Baada ya mtoto kufika mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 03(1) atasomewa shitaka na msoma shitaka au hakimu atafafanua shitaka hilo ili mtoto aelewe vizuri.
-
Dhamana ya mtoto
Inaweza kuwa ya polisi kwa mujibu wa kifungu cha 101 au ya mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 104. Ikiwa mtoto ametenda kosa la kudhaminika basi atapata dhamana na ikiwa kosa lake si la kudhaminika au mazingira hayaruhusu kudhaminika, mtoto hatapewa dhamana. Kumbe tunaona kuwa suala la dhamana linawuhusu hata watoto.
-
Mtoto kupelekwa mahabusu baada ya kukosa dhamana
Ikiwa mtoto atanyimwa dhamana, basi kwa mujibu wa kifungu cha 104(1) cha sheria hiyo basi atapelekwa mahabusu. Mahabusu hapa ni taasisi maalumu kwa ajili ya watoto au kuwekwa chini ya uangalizi wa kamishna wa ustawi wa jamii. Siyo Segerea, Butimba au Ukonga.
5.Kukubali na kukana shitaka
Kwa mujibu wa vifungu vya 107 na 108(1) mtoto akikubali shitaka na Mahakama ikaridhika, atatiwa hatiani na upande mwingine akikana basi kesi itaendelea kwa upande wa mashtaka kusikilizwa. Kwa hiyo, hapa tunaona kuwa mtoto naye huulizwa kukiri ama kukataa kosa.
6.Kusikilizwa kesi ya mtoto
Upande wa mashtaka utawasilisha kesi yao ya kumshitaki mtoto na kutaka aadhibiwe. Wataleta mashahidi na ushahidi wao kuthibitisha kosa alilotenda mtoto na wakimaliza kesi yao itafungwa.
Kadhalika, upande wa mtoto utakuja na utetezi wao na kutaka mtoto aachiwe huru. Utaleta mashahidi na ushahidi kuonesha kwamba mtoto hakutenda kosa. Upande wa mtoto unaruhusiwa kuwakilishwa na mzazi, mlezi, afisa ustawi wa jamii. Haya ni kwa mujibu wa vifungu vya 108,109 na 110.
-
Mtoto kupatikana na hatia au kutopatikana na hatia
Kwa mujibu wa kifungu cha 111(1) ikiwa kesi dhidi ya mtoto itathibitika, basi mtoto atatiwa hatiani na ikiwa haitathibitika ataachiwa huru.
-
Adhabu baada ya hatia
Vifungu vya 118(1) na 119(2) vinatoa adhabu ya faini, fidia, gharama na kifungo kwa mtoto. Mara nyingi malipo ya adhabu hizi hulipwa na mzazi, mlezi, au ndugu. Kuhusu kifungo mtoto haendi jela kama mtu mzima.
Itatolewa amri ya kuondolewa katika mkoa au wilaya alikokuwa anaishi na akaishi kwingine (repatriation), atapelekwa shule za mafunzo maalumu za watoto watukutu, atawekwa chini ya uangalizi wa afisa ustawi wa jamii au chini ya taasisi nyingine nk. Atapewa adhabu moja kati ya hizi.
Yote kwa yote wazazi wasijisahu katika malezi na mienendo ya watoto kwani inaruhusiwa mtoto kupelekwa polisi, mahakamani na kuhukumiwa. Hatua hizi kwa mtoto wako si nzuri. Zitakupotezea muda na gharama kubwa.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.