Na Isri Mohamed
Mwanafunzi Joel Malick, wa kidato Cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara iliyopo mkoani Manyara aliyepotea katika mlima wa Kwaraa walipokwenda kufanya utalii wa ndani pamoja na masomo kwa vitendo, amepatikana akiwa amedhoofika huku mwili ukiwa na majeraha.
Joel ambaye alipotea kwa siku 26 na kutafutwa bila mafanikio huku wazazi wake wakiwa wameshakata tamaa, amepatikana Oktoba 9, 2024, upande wa pili wa mlima uliopo msituni hapo akiwa dhoofu huku akiomba msaada, ambapo mtu mmoja alimuona na kumsaidia kumfikisha hospitali na kisha kusambaza taarifa ambazo ziliwafikia Jeshi la Polisi na wazazi wake.
Akizungumza baada ya kumuona mtoto huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Manyara akipatiwa matibabu, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendinga amesema hali ya mtoto huyo si mbaya sana kwa sababu anaweza kuongea, ila ana majeraha mengi na mikwaruzo mwilini.
“Vipimo vya awali ambavyo vimeshafanywa mpaka sasa hivi havioneshi kwamba ana tatizo kubwa zaidi ya mwili kudhoofika ambayo inawezekana ni kwa sababu ya kukosa chakula na kukaa sehemu ambayo haikuwa sahihi kwa muda mrefu.
“Madaktari wanaendelea na tiba kwanza ya mwili wake kwa ajili ya kupata afya, lakini pia madaktari wa tiba ya afya ya akili nao wameanza kufanya kazi kuhakikisha kwamba tunamuweka mtoto katika hali iliyokuwa sawasawa, ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa madaktari mpaka afya yake itakapokuwa salama” amesema RC Sendiga.
Nae Baba mzazi wa mtoto huyo, Johanes Malick, ameelezea furaha yao kama familia ya kumpata Joel akiwa mzima kwani walikuwa wameshakata tamaa.
“Tulipambana sana, tangu tukio lilipotokea hatujawahi kutoka Babati, tuliamua kupigana mpaka tumpate mtoto wetu na Mungu amesaidia, tunawashukuru wote waliotupigania kwa sala na maombi”