Na Isri Mohamed
Mtoto Malick Hashim (6) aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili tangu julai 15, baada ya kuchinjwa na kitu chenye ncha kali shingoni na anayedaiwa kuwa ni dada wa kazi, ameruhusiwa kutoka hospitalini hap oleo Agosti 07, baada ya jopo la madaktari waliokuwa wakimuhudumia kujiridhisha na hali yake.
Mtoto huyo ambaye alikuwa mahututi akishindwa kupumua wala kuongea kutokana na kitu hicho chenye ncha kali kutenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti, kwa sasa yupo salama na atarudi nyumbani ili kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida huku hospitali ikiahidi kufuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhavile amesema, watalaam wa hospitali wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata mtoto huyo tangu alipopokelewa Julai 15 mwaka huu.
Kwa upande wa Baba mzazi wa mtoto huyo, Hashim Kitumbi ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa kulipia gharama za matibabu za mtoto wake, madaktari wa hospitali ya Taifa Muhimbili waliokuwa wakimuhudumia mtoto katika kipindi chote alicholazwa pamoja na watanzania wote kwa ujumla walioguswa na tukio la mtoto wake.
Naye Daktari Bingwa wa Tiba na Magonjwa ya Dharura, Dkt. Juma Mfinanga amesema mara tu baada ya mtoto huyo kupokelewa akiwa na hali mbaya kutokana na majeraha aliyopata walihakikisha anapata huduma ya kwanza ya kurejesha hali ya upumuaji, kupata damu na badaye kuita timu husika ya wabobezi wa upasuaji wa shingo, pua, koo na masikio.