Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Njombe
JESHI la Polisi mkoani Njombe limewaomba viongozi wa makanisa na misikiti kutoa mafunzo mema ya dini kwa watoto ili kupunguza matukio ya vijana ama watoto kujichukulia sheria mkononi kwa kujiua.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani Njombe,Kamanda wa Polisi Hamis Issah amesema kuwa wamesikitishwa na tukio la mtoto (jina linahifadhiwa) wilayani Makete ambaye ameamua kujiua baada ya wazazi wake kumuonya baada ya kuwaacha punda na kwenda kula mazao ya shamba la watu.
“Huyu mtoto baaada ya kufokewa na wazazi wake kuhusiana na kumwacha punda ambaye alikwenda kula mazao katika shamba la watu baada ya yeye (marehemu) kwenda kucheza na wenzake,” amesema.
Kamanda wa Polisi Issah amesema Mtoto huyo aliacha punda aliokuwa nao machungani na kwenda kucheza na Watoto wenzake hali iliyomfanya baba yake kumuonya baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwenye shamba.
Amesema kuwa baada ya kupokea malalamiko hayo alimfokea mtoto wake kwa kumtaka achunge punda kwa umakini lakini mtoto huyo aliamua kuchukua maamuzi magumu akatafuta sumu akanywa na kufariki.
Hata hivyo Kamanda Issah ametoa wito kwa wazazi na walezi kutafuta njia sahihi ya kuzungumza na watoto huku pia akiomba viongozi wa dini kutokana makanisa mbalimbali pamoja na misikiti kuendelea kutoa mafunzo mema ya dini kwa watoto ili wawe na imani na kuacha kuchukua maamuzi magumu kama hayo.