Na Alex Kazenga, JamhuriMedia, Katavi
Utalii wa kuvua samaki (spot fishing) katika mto Ndido wenye maji yanayoonyesha hadi samaki, mawe na wadudu walioko ndani ya maji katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni kivutio kizuri kwa watalii, achilia mbali utalii wa kutazama wanyama wakiwa kwenye makundi makubwa ndani ya hifadhi hiyo.
Mto Ndido unasifa ya kutiririsha maji safi yanayopita juu ya mawe kiasi cha kumuwezesha mtalii anayefanya utalii wa kuvua samaki kumuona samaki anavyonasa kwenye chambo pamoja na mawe ya kuvutia yenye maumbo mduara mithili ya golori ndani ya maji.
Utalii wa aina hiyo umebainishwa Februari 28, 2024 na Afisa Uhifadhi wa hifadhi ya Katavi, Beatrice Msuya alipozungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo kujionea na kutangaza vivutio vya hifadhi hiyo.
“Hiifadhi yetu ya Taifa Katavi ina vivutio vingi vya utalii, kipo kivutio kikubwa cha ziwa Katavi ambalo limebarikiwa kwa kuwa na viboko wengi kuliko hifadhi zote zilizopo nchini,” amesema Beatrice.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi inapatikana mkoani Katavi ikiwa ndani ya wilaya tatu za mkoa huo; wilaya ya Mlele, katika Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya yaTanganyika na Wlaya ya Mpanda katika Halmashauri ya Nsimbo.
Beatrice akielezea kivutio cha ziwa Katavi kilichopo ndani ya hifadhi hiyo amesema mbali na idadi kubwa ya viboko pia ina samaki aina ya kambale na kamongo wanaozaliana kwa wingi.
Maji ya ziwa Katavi yakiwa mengi anasema baadhi ya samaki husafiri na kwenda kwenye mito mingine iliyopo nje ya hifadhi ambao wanaweza kuvuliwa na wananchi wa maeneo hayo kwa vibali maalum vya Serikali.
“Hapa tunao simba wanaotembea kwa makundi, twiga, swala ,tembo, chui, pundamilia, lakini pia tuna aina mbalimbali za ndege,” amesema na kuongeza kuwa ndani ya hifadhi hiyo wanalo zao la utalii wa Utamaduni.
Utalii wa Utamaduni ndani ya hifadhi anaeleza kuyahusisha makabila mawili; Wabende na Wapimbwe ambao wana tamaduni za kuabudu mizimu ambao ndio asili ya jina la mkoa wa Katavi.
“Mkoa wa Katavi umetokana na mwindaji aliyeitwa Katabi , huyu alikuwa kiongozi wa kimila aliyeshughulikia masala ya matambiko ya wapimbwe na Wabende. Kabala ya kuwa hifadhi wawindaji waliamini Kabla ya kwenda kuwinda lazima wapite kwenye mti WA mkwaju uliotumiwa na Katavi kama eneo la matambiko,” amesema.
Ingawa masuala ya kutambikia mizimu yanaonekana kuwa ya zamani Beatrice anasema makabila hayo mawili bado yanafanya matambiko ndani ya hifadhi hasa uliopo mti huo wa mkwaju.
Kwa mujibu wa Beatrice, Wapimbwe na Wabende yanafanya matambiko chini ya mkwaju wakiomba mizimu wa Katabi na mke wake wawape baraka na kuwaondolea mabalaa.
“Sehemu hii ya matambiko ni kivutio, makabila yanayozunguka hifadhi hii na mkoa wa Katavi pamoja na Watanzania kwa ujumla ambao bado wanafanya ibada za asili wanaweza kuja kuona namna asili inavyoenziwa na kutunzwa.,” amesema.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ilianzishwa mwaka 1974, kati ya hifadhi 21 zilizopo nchini yenye inashika nafasi ya tano kwa ukubwa, ambapo ina jimla ya kilometa za mraba 4471.
“Niwaombe Watanzania nyakati za likizo na mapumziko waje kwenye Hifadhi yetu waone wanyama kwa ukaribu pamoja na uoto wa asili wenye miti inayofunika ardhi ya hifadhi na kuifanya kuwa na uoto wa aina yake,” amesema .