Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameunda timu maalumu kuchunguza tukio la mlipuko wa lori la mafuta ulioua watu 71  na majeruhi 59 kwa mujibu wa takwimu za hadi Jumapili alasiri.

Timu hiyo inatarajiwa kukamilisha kazi zake Ijumaa wiki hii na kwa mujibu wa maelezo ya waziri mkuu, ibainishe yeyote ambaye amezembea katika kutimiza wajibu wake kwa wakati kuhusu ajali hiyo ya aina yake.

“Hii tume inaanza kazi leo (Agosti 11, 2019) hadi Ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii si mara ya kwanza, ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi Watanzania pale gari linapoanguka tusitumie kama fursa, twende tukaokoe binadamu waliopo pale,” amesema waziri mkuu alipozungumza na waombolezaji waliofika katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao.

“Tuungane na waliofikwa na tatizo, tuwatie moyo, tuwape pole. Na waliopo hospitalini waendelee vizuri na matibabu. Rais amehuzunika sana. Ana ugeni mkubwa wa marais 16, ametuleta sisi wasaidizi wake. Makamu wa rais amenipigia simu kunipa salamu zake za pole. Jambo hili si dogo. Lazima tujiridhishe. Ajali imetokea katikati ya manispaa, saa mbili. Ajali ilipotokea kila mmoja na majukumu yake aliwajibika? Kuna trafiki, polisi. Gari lilipoanguka tu, nani alijitokeza kwanza? Waliokwenda na madumu walipata taarifa za awali kwamba litaanguka? Muda wa kukutana wote hao (wananchi) nani aliwajibika kuwazuia?

“Ninachojua, trafiki huwahi ajali hata kwa kukodi gari. Je, walifanya hivyo? Fire (Zimamoto) ilikuja kwa muda gani? Lazima tujiridhishe. Nitaunda tume ya wataalamu wanipe majibu ya maswali haya. Itafanya kazi kuanzia leo (Jumapili – Agosti 11, 2019) hadi Ijumaa, hata kama nimehusika wanitaje,” amesema waziri mkuu.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu amesema Rais Magufuli tayari amekwisha kutoa kibali cha kutolewa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa zinazohitajika.

Katika hatua nyingine, taarifa zinabainisha kuwa Rais Magufuli aliwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo waliofikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi. Inaelezwa kuwa kuna majeruhi takriban 43 Muhimbili, wengi wakidaiwa kuungua mwili kwa zaidi ya asilimia 80.

Taarifa zaidi hadi Jumapili jioni zilibainisha kuwa katika Hospitali ya Mkoa ya Morogoro imebaki na majerahi 15 wa ajali hiyo ya moto. Akizungumza kutokea Muhimbili Jumapili jioni, Rais Magufuli amewataka Watanzania kutowahukumu waathirika wa mkasa huo wa moto.

“Naona watu wanasema kwamba hawa wote walikwenda kuiba, tusiwe majaji, wengine walikwenda kusaidia huku wengine wakiwa wapita njia. Mwingine alikuwa safarini kuelekea Mtwara, akazuiliwa na moto ulipolipuka ukamkuta,” amesema na kuongeza kuwa serikali yake itagharimia matibabu kwa waliojeruhiwa, huku akitoa Sh 500,000 kwa kila majeruhi.

Matukio ya aina hii yamewahi kutokea katika nchi mbalimbali Afrika. Julai 2, 2010 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilishuhudia watu 292 wakiteketea kwa moto baada ya lori la mafuta kuanguka Kijiji cha Sange, watu hao waliokufa walikuwa katika harakati za kufyonza mafuta kutoka katika lori hilo, lakini DRC tena, Oktoba 6, 2018 ilishuhudia watu 53 wakifa kwa ajali ya aina hiyo, eneo la Kinshasa, huku Kenya Januari 31, 2009 ikishuhudia ajali ya namna hiyo iliyoua watu 122 eneo la Molo, kaskazini mwa Nairobi.

Septemba 16, 2015 Sudan Kusini vilevile ilishuhudia watu 203 wakifa kwa ajali ya namna hiyo huku wengine 150 wakijeruhiwa wakati wakijaribu kuiba mafuta. Novemba 17, 2016 huko Msumbiji takwimu za vyombo mbalimbali vya kimataifa mitandaoni zinaeleza kuwa watu 93 waliuawa kwa ajali ya aina hiyo kama ilivyokuwa Julai 12, 2012 huko Nigeria ambako watu 104 waliuawa kwa ajali ya aina hiyo katika Jimbo la River State.