Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera
Hali ya taharuki imezuka katika kijiji cha Bukabuye, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kufuatia mti uliong’oka kwa upepo mkali ndani ya miaka mwili iliyopita na matawi yake kutumika kama kuni, kukutwa umejisimika tena kwenye shimo lake kama vile haukuwahi kungo’lewa.
Wakazi wa eneo hilo wamejikuta wakipata hofu mpaka kushindwa kuwatuma watoto wao dukani, huku wakihusisha mti huo na masuala ya kishirikina.
“Kila mtu alikuwa anasema la kwake kuhusu huo mti, maana mti hauwezi kuwa umeshalala chini halafu ukasimama tena ghafla, mtu asubuhi ameingia pale amekata mti, mara umesimama, ikawa imetupa taharuki kila mmoja anaogopa mpaka kuwatuma watoto tumeshindwa.
“Kuna miujiza, uchawi, mambo mengi yamesemeka hivyo ila kusema ukweli mambo ya uchawi ndio yamesemwa zaidi” amesema.
Kufuatia taharuki hiyo imewalazimu wataalam wa masuala ya jiolojia kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam kufika eneo la tukio ili kubaini ukweli, ambapo pia wamefanya mkutano wa hadhara na wanakijiji.
“Mti huu uliota katika mwamba, hivyo mizizi yake haikuweza kwenda chini zaidi na watu walipoanza kuukata uzito wa juu ukapungua na kubaki uzito wa chini ambao ndiyo uliouwezesha mti huo kurudi tena katika shimo lake ambalo bado lilikuwa wazi” amesema Profesa Nelson Boniphace.