Maneno haya yaliandikwa Desemba, 2017 na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro ambaye wiki iliyopita ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM. Chini ya kichwa cha habari “Comrade Samson Mwigamba amenigutusha kitandani, Mtatiro alilaani uamuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba kujiunga CCM. Tunawaletea neno kwa neno kama alivyoandika Mtatiro mwenyewe. Endelea….
Ameongea mambo mengi sana lakini nataka kumjibu juu ya jambo moja, suala la vyama vya upinzani kubadilisha mkakati ili kupambana na CCM ya Magufuli.
Mwigamba anasema JPM ataupoteza upinzani na lazima ubadili mbinu, maneno hayo yanasemwa pia na watu wengi sana ambao wanajinasibisha na CCM, kiukweli yanasemwa hata na baadhi na wanachama waandamizi wa vyama vyetu.
Well and Good; kabla ya vyama hivi havijabadilisha mbinu lazima tujiulize, kwani huyo Magufuli anafanya kipi kikubwa hadi kuvipoteza vyama vya upinzani, maana tukikijua kitu hicho ndipo tutajua vyama vya upinzani vinahitaji dawa gani.
Kwa ujumla, JPM hawezi akavipoteza vyama vya upinzani kwa kujenga reli ya SGR, kununua ndege za Bombardier, kutumbua watendaji serikalini, kupambana na ufisadi kwa kuwakamata mafisadi waliosakwa muda mrefu kama SADIFA n.k.
Hayo yoote na mengine hayawezi kupunguza nguvu za upinzani na wala hayawagusi wananchi wa kawaida ambao wanahitaji pesa mifukoni, biashara zao zikue, mazao yao yauzwe, wajenge nyumba bora, wapate uhakika wa matibabu na wawe na huduma za uhakika za kijamii – mambo ambayo hadi sasa yako vilevile.
LAKINI mimi binafsi najua kuwa njia ya kuviua vyama vya upinzani ni moja tu, kuvizuia visifanye shughuli za kisiasa kama mikutano ya hadhara na maandamano, kuzuia visitangazwe na vyombo vya habari, kuvipora ushindi kwa nguvu kwenye chaguzi, kukamata na kufunga viongozi wake, kuwaaminisha wananchi kuwa vyama hivyo vinatetea umagharibi, usaliti na vitavunja amani na kwa hiyo kutumia vyombo vya dola kuwaumiza wafuasi na viongozi wa vyama hivyo ili wakate tamaa, kutaifisha mali zao na biashara na viongozi wao n.k.
Kwa ujumla JPM na serikali yake wanaweza kuviua vyama vya upinzani kwa njia za mabavu, uimla, udikteta na kutumia ukatili wa hali ya juu dhidi ya vyama hivyo.
JE YANAFANYIKA?
Ndiyo, yanafanyika, tena kwa kasi kubwa kweli kweli. Mwigamba na watu wenye akili kama zake wajue kuwa kuirudisha AIRTEL serikalini hakuwezi kuua upinzani hata kidogo.
Walioiuza AIRTEL kifisadi kimya kimya ndiyo hao hao wanairudisha serikalini kwa nguvu wakifanya hivyo mbele ya KAMERA ili tuwapigie makofi na kuwasujudu.
Wenye akili timamu hawawezi kuwapogia magoti kwa sababu wanafanya jukumu la kurekebisha makosa yao na kwa kweli walipaswa kupiga magoti na kutuomba radhi wakati “wanaiokota AIRTEL” kwa mara nyingine.
SABABU YA UPINZANI KUFA INAJULIKANA!
Ndiyo, ni mabavu, na kwa kweli nchi zote duniani zilizotumia mabavu na ukatili mkubwa dhidi ya vyama vya upinzani, vyama hivyo vilisambaratishwa, viongozi wake walikimbilia uhamishoni, waliuawa na ama walihamia jela.
Familia zao zilisakwa zikatwezwa na kuteswa. Nchi za Zimbabwe, Uganda, Rwanda, Burundi n.k. haya yanatokea, waziwazi. Tanzania nako yameshaanza kutokea.
VYAMA VYA UPINZANI VIFANYEJE?
Nakuuliza Mwigamba na wewe Mtanzania unayesema vyama vya upinzani vibadilishe mbinu.
Hebu niambieni, vyama vya upinzani vinapoandamwa na serikali ya chama dola, serikali ikadharau katiba na sheria za nchi, ikazuia vyama hivi visifanye kazi, ikavipiga vita kwenye MEDIA, ikapeleka viongozi wake jela…
Ikajaribu kuwatisha na kuwaua viongozi wa upinzani, ikawapora ushindi kwenye chaguzi kwa kutumia JANJAWEED, mitutu ya bunduki, DED’s na machineries zote za serikali…kwenye mazingira kama hayo, vyama hivyo vibadili mbinu na kufuata ipi?
Mbinu za kupambana kisiasa katika nchi zimeshatajwa katika katiba, sheria na kanuni mbalimbali. Ikiwa hizo kanuni na sheria na katiba havifuatwi, na sasa siasa zinaendeshwa kimabavu, vyama vya upinzani vibadili mbinu na kuanza kufanya nini?
Nakuomba Mwigamba na wenzako wenye mawazo kama haya mtuletee majibu ya kina. Mbinu za kupambana na serikali ili viongozi wa upinzani wasiendelee kusukumizwa jela ni zipi?
Mbinu za kuhakikisha vyama vya upinzani vinawaondoa polisi na majeshi kwenye chaguzi zetu ni zipi?
Mbinu za vyama vya upinzani kuzuia mawakala wake wasitolewe kwenye vituo vya kupigia kura chini ya mtutu wa bunduki ni zipi?
Mbinu za viongozi wa upinzani kuzuia RC’s, DC’s n.k. wasiwe mawakala wa NEC na watoa maamuzi juu ya nani ashinde na nani ashindwe ni zipi?
Mbinu za viongozi wa upinzani kuzuia wagombea wake wasiswekwe ndani na kupigiwa kura wakiwa lupango, bila sababu, ni zipi?
Mbinu za kuzuia viongozi wa upinzani na wafuasi wao wasitishiwe maisha na kuuawa ni zipi?
Mbinu za vyama vya upinzani kuzuia wafuasi wao kupigwa na kukatwa mapanga kwenye vituo vya uchaguzi ni zipi?
Mbinu za upinzani kuzuia ma-DED wasiwatangaze wagombea wa CCM walioshindwa ni zipi?
Mbinu za upinzani za kuzuia NEC isiongozwe na makada wa CCM na maafisa waandamizi wa “KITENGO” ni zipi?
Hebu tuelezeni, upinzani ubadilishe mbinu ili u-deal na JPM, ufanyeje? Hili swali si kwa Samson Mwigamba tu, ni kwa kila Mtanzania. Nawaomba mlihamishie mpaka kwenye GROUPS zenu za whatsup na mtueleze.
Ukishindwa kuchangia hapa unaweza kunitumia maoni, whatsup +255787536759 au [email protected]
Mtatiro J,
22 Disemba 2017