Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tunduru

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro amesema,ni muhimu suala la upandaji miti katika wilaya hiyo liwe endelevu na jambo la mara kwa mara ili kusaidia uhifadhi wa mazingira.

Mtatiro amesema hayo,baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti lililofanyika katika eneo la Kanisa la Upendo la Kristo Masihi (KIUMA) kata ya Matemanga wilayani humo.

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta kulia,akimsaidia mwakilishi wa Shirika la Word& la Nchini Ujerumani Deed Susanna Diechmanna kupanda mti wa kumbukumbu  wakati wa zoezi la upandaji miti katika viwanja vya kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Kiuma

Mtatiro,amewakumbusha viongozi wa ngazi za vijiji,kata na Halmashauri kuendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti katika maeneo yao na kushauri aina ya miti inayofaa ambayo haina athari kimazingira hasa kwenye vyanzo vya maji.

Amesema,uharibifu wa mazingira unaongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na shughuli za kibinadanu ikiwamo kilimo na ufugaji holela, huku waharibifu hao wakishindwa kupanda miti mipya katika maeneo hayo,jambo linalo weza kuhatarisha maisha ya binadamu na viumbe hai wengine.

Amesema,suala la upandaji miti ni muhimu katika jamii yetu kwani itasaidia sana kukabiliana na changamoto ya hewa ukaa inayoweza kuhatarisha maisha ya Binadamu,hivyo wananchi wana wajibu wa kuzuia hatari hiyo.

Aidha,amelipongeza kanisa hilo kwa kuandaa zoezi la upandaji miti na kuzitaka taasisi nyingine za dini,serikali na binafsi kuiga mfano wa Kanisa la Upendo kutokana na harakati zake za kupanda miti mara kwa mara ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kushoto na Katibu Mkuu wa  Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta wakipanda mti wa kivuli katika viwanja vya Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Kiuma wilayani Tunduru.

Amesema,serikali imekuwa na mikakati mbalimbali katika kuhakikisha inatunza mazingira ambapo alitaja miongoni mwa mikakati hiyo ni kupanda miti kwa wingi katika taasisi,idara za serikali na taasisi binafsi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassan Kungu alisema,amewaomba wananchi wa jimbo hilo kuunga mkono jitihada za serikali za utunzaji mazingira kwa kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, akimwagilia maji mti alioupanda  wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti  lililofanywa na Taasisi ya Kiuma wilayani humo,kulia ni Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Daniel Malukuta.

Naye Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta alisema,kila mwaka taasisi hiyo imekuwa na utaratibu wa kuotesha miche na kupanda miti kuzunguka maeneo yake ili kutunza mazingira na kuhamasisha jamii na waumini wa kanisa la Upendo kuona suala la upandaji miti ni muhimu katika maisha yao.