Mabeberu hawawezi kuhujumu na kudhulumu utu na uchumi wa Mtanzania bila kibali cha Watanzania. Kibali hiki hutolewa na Watanzania wachache vibaraka wenye uroho na tamaa ya ukubwa na utajiri wa haraka haraka.

Mimi na wewe, Mtanzania mwenzangu wa karne hii, tunasakamwa na unyonge wa moyo na unyonge wa umaskini. Tumeona, tumezaliwa, tumekulia katika ari ambayo mataifa yote yanajiona yana ubora kuliko sisi. Binadamu wa dunia nzima wanatucheka.

Mabeberu wa dunia nzima wanatudharau, wanatukebehi, wanatukejeli ili wapate kututumia kama vihongwe wa kuwazalishia mali. Kwao wao sisi ni limbukeni tunaoweza kudanganywa kwa hali na mali mpaka kufikia kiwango duni cha kuusaliti utu wetu wenyewe.

Mtanzania mwenzangu tunapokuwa wavivu na wazembe kiasi cha kuzorotesha mipango yetu ya maendeleo, tunaukaribisha umaskini na kuzidisha unyonge wetu ili mabeberu watutafune na kuudhulumu utu na uchumi wetu daima dumu. Kwani wajinga ndio waliwao.

Wewe na mimi hatuwezi tukalima, tukavuna. Tukala, tukashiba. Tukalala, tutaamka. Tukalia, tukacheka sawa na binadamu wengine, kama hatutachukua hatua thabiti za kuuandama unyonge wetu na kuupiga pigo la kifo cha fofofo. Unyonge wetu lazima uuawe.

Mavuno na shibe, cheko na furaha, kulala na kuamka salama lazima kutokane na uchumi tunao utengeneza. Hatuwezi kuwa na uchumi huo iwapo hatutaweka pamoja mkazo katika maarifa yetu, nguvu zetu na usalama wa mapato na matumizi yetu kihalali na kinaga ubaga.

Uchumi wa nchi au watu ni lazima ulindwe, udhibitiwe na utumike katika utaratibu mzuri na uliokubaliwa na watu au nchi yenyewe. Hii ina maana masuala ya ulinzi na usalama yanakuwako muda wote kunyima mwanya msemo usemao, ‘mvunja nchi ni mwananchi.’ Hadhari Iwekwe.

Hapa nchini iko hali ya Watanzania wenzetu ya kutojitambua katika masuala ya kujikomboa kiuchumi na kijamii, hata kufikia kuuza utu wao na mali zao kwa mabeberu. Katika hali hii hatuwezi tukaua unyonge wetu na ulimbukeni wetu iwapo hatutakubali kujitambua, kubadilika na kuacha mazoea.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli, inatuzindua na inatukumbusha tuukatae na tuuondoe unyonge wetu na ulimbukeni wetu na tuanze kwenda pamoja katika kujikomboa kiuchumi. Wakati wa kufanya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ni sasa. Twende.

Kujitambua, kubadilika na kuacha mazoea kuna hitaji matendo na kauli ya ukweli, si maneno. Tukumbuke msemo wetu wa Kiswahili: “Maneno mengi ni ukongo.” Kuongea sana ni sawa na uendawazimu. Tunahitaji matendo tupate kula uhondo. Wewe Mtanzania mwenzangu acha mazoea, jitambue.

Tukijitambua kifikra na kimawazo ndiyo kujikomboa. Tukibadilika kimatendo na kimsimamo ndiyo kujiamini na tukiacha mazoea na desturi ndiyo kujikosoa katika maeneo yetu huko viwandani, mashambani, maofisini na sokoni. Na tuwe macho muda wote katika usalama wa uchumi wetu.

Mtanzania mwenzangu wa karne hii tushiriki kikamilifu katika kuweka utu wetu na kutunza uchumi wetu. Mambo haya si hiari, si hisani wala si saidia kwa nchi yetu. Ni haki na wajibu kwa kila Mtanzania. Unapofuata utaratibu huu ndiyo unatekeleza demokrasia ya kweli.

Uchumi tunaoujenga hapa nchini hauhitaji kejeli na maandamano wala ujuzi wa nahau kupinga hiki na kutega hiki, kwa visingizio vya haki za binadamu. Haki isiyo na wajibu si haki, ni dhuluma, ni usaliti. Dhuluma na usaliti huo ndiyo uliotufikisha hapa. Sasa tuachane nao, si mtaji, si mpango murua.

Namalizia na kutoa ushauri kwako kwamba zingatia na tafakari methali mbili zifuatazo. “Mvunja kwao hakui ila kuwa kama seserumbe” na “Mvunja nchi ni mwananchi.” Acha mazoea haya.