Dk. Frannie LeautierMchumi kutoka Tanzania, Dk. Frannie Leautier ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais Mwandamizi katika kundi la Benki ya Mendeleo ya Afrika (AfDB). Benki hiyo ilimtangaza rasmi mwezi Mei, mwaka huu.

Dk. Frannie alikuwa  Mwenyekiti na mwanzilishi mwenza wa Mkopa Private Equity Fund, taasisi ambayo ilikuwa imejikita katika masuala ya mitaji kwa kampuni ndogo na za kati zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mwanamama huyo anaheshimika duniani kote kama mtaalam wa masuala ya maendeleo kwa zaidi ya miaka 25 ya ujuzi wake wa kitaaluma. Anategemewa kuleta chachu mpya katika benki hiyo ya maendeleo ya Afrika kwa kuleta uzoefu katika masuala ya kifedha kutoka kwenye taasisi binafsi na za umma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoko katika mtandao wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, dada huyo anafahamika zaidi kwa kuwa mtu wa kupenda kuona matokeo mazuri na amekuwa akihubiri ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

 Dk. Frannie ni msomi wa shahada ya uzamivu, katika shahada yake hiyo aliyoipata miaka 26 iliyopita, alijikita katika mifumo ya miundombinu kutoka katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Massachusetts, nchini Marekani. Katika shahada yake ya uzamili aliyoipata mwaka 1986, alijifunza masuala ya usafirishaji.

Mwaka 1992-1994 alijiunga na Benki ya Dunia kama mchumi wa masuala ya usafirishaji, katika idara ya miundombinu, akishughulikia ukanda wa Amerika ya Kusini, ambapo katika utumishi wake alipata tuzo ya umahiri katika kuandaa miradi ya miundombinu nchini Peru.

Kati ya mwaka 1994-995 alipanda na kuwa Mchumi wa Benki ya Dunia katika masuala ya utafiti. Baadaye alipandishwa na kuwa Mchumi Mwandamizi katika Idara ya Miundombinu, akishughulikia Asia Kusini. Baadaye 1995-1997 aliongezea wigo na kufanya kazi katika nchi nyingine sita kutoka katika Bara la Asia.

Amekuwa Mkurugenzi Mkuu, akisimamia miundombinu barani Asia chini ya kitengo cha Benki ya Dunia kuanzia mwaka 1997 hadi 1999. 

Pia amewahi kusimamia miradi ya sekta za nishati na maji ambayo imefadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Dunia hususani sekta ya uchukuzi. Ametunukiwa tuzo ya utendaji mahili.

Dk. Leautier aliteuliwa kuwa Mkuu wa Utumishi na Mkurugenzi katika Ofisi ya Rais wa Benki ya Dunia kuanzia mwaka 2000 hadi 2001. Baadae aliteliwa kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia akiwa kiongozi katika taasisi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2007.

Kutokana na mchango wake mkubwa katika taasisi hiyo kubwa ya fedha akifanya kazi kwa umakini, kujiamini na uaminifu alitunukiwa tena tuzo ya utumishi bora mwaka 2003 katika Benki hiyo. Pia alitunukiwa tuzo ya Mahili ya Rais aliyotunukiwa mwaka 2002 kutokana na mchango wake wa utumishi huko Barani Amerika Kusini.

Kuanzia mwaka 2007 hadi 2013 aliteuliwa kuwa Profesa akifundisha uongozi katika Dunia ya Utandawazi na Sayansi huko Paris alipokuwa akichukua kozi ya juu katika masuala ya kimataifa na uongozi.

Dk. Leautier amekuwa na uzoefu mkubwa katika sekta za umma pia amewahi kuwa kiongozi mshiriki wa Fezembat kuanzia 2007 hadi 2009, kampuni inayojihusisha masuala ya uongozi na huduma za ushauri kwa viongozi waandamizi wa kampuni zinazowekeza katika madini, miundombinu na nishati na utafutaliji wa masoko.

Mwaka 2009 hadi 2013 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (ACBF). Hapo alifanikiwa kufufua na kukuza sifa katika utawala, uwajibikaji na ubora kwa taasisi.

Hayo ni matokeo ya jitihada zake na mchango wake kwa Serikali za Afrika uliozifanya zipate maendeleo ambayo ni mara tano zaidi katika kipindi cha utendaji wake na pia kuongeza mapato yake kutoka kwa wahisani wa nje. Ameonyesha uzoefu, ushupavu na mvuto katika mabadiliko.

Dk. Laeutier ni mpenda maendeleo. Amesaidia wajumbe wa bodi za mashirika mbalimbali hususani wanawake katika Benki ya Dunia, Taasisi ya Mafunzo ya Ulinzi, Uwekezaji na Utafiti wa Uchumi Barani Afrika, Taasisi ya Kimataifa ya Viazi, Chuo Cha Sayansi na Teknolojia Cha Nelson Mandela na mpango wa Uchumi wa Dunia akiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika mwaka 2013 hadi 2014 na taasisi ya Kujenga Uwezo Barani Afrika.

Dk. Leautier amekuwa na mtazamo na uzoefu wa kipekee kwa maendeleo ya sekta za umma na binafsi kutokana na rekodi zake katika uendeshaji wa mashirika ulioleta mafanikio. Katika jarida la The New African ameorodheshwa kati ya watu 100 wenye mafanikio kuanzia mwaka 2011 hadi 2013. Anaelewa kwa ufasaha lugha za Kiingereza na Kifaransa, pia anaweza kuzungumza Kispaniola na Kiarabu.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk. Akinwumi Adesina akizungumzia uteuzi wake anasema, “Nimefurahishwa na Dk. Frannie Leautier kujiunga na Benki akiwa na nafasi ya juu ya Makamu wa Rais. Amekuwa na mtazamo mkubwa wa maendeleo na anaufahamu mkubwa kuhusu Afrika.

“Atatoa mchango mkubwa katika utendaji na kuzijengea uwezo sekta binafsi. Ni mmoja wa wadau wakubwa wa maendeleo ya Afrika, atasaidia katika jitihada za kuipeleka Benki katika maendeleo makubwa zaidi.”

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Aziz Mlima anasema, mwanamama huyo ni Mtanzania mwenyeji wa Lushoto, aliyesomea Jangwani Sekondari, na baadaye akasoma uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Dk. Mlima anasema, anao uzoefu wa kutosha na ni msomi aliyebobea na pia aliwahi kufanya kazi katika taasisi ya Africa Capacity Building Foundation yenye makao yake makuu jijini Harare, Zimbabwe.

“Kwa nafasi yake mpya ndani ya AfDB ni nafasi ya juu ya utendaji ndani ya Benki hiyo… Jukumu lake kubwa ni kwa Afrika nzima. Lakini pia kama sehemu ya juu ya Uongozi wa AfDB anaweza kisaidia kuwa kichochea cha mikopo na miradi mikubwa na yenye tija kwa maslahi ya Tanzania, EAC na SADC kama sehemu muhimu ya kiungo kwa kanda zote hizo,” anasema Dk. Mlima.

Anasema kanda hizo alizozitaja zitaweza kufanikiwa, lakini yote yanategemea mazingira ya ndani ya kifedha ya AfDB na ufutiliaji kutoka “kwetu wenyewe”.

“AfDB imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa fedha katika ujenzi wa miundombinu kama barabara na pia wanaweza kutumika katika ujenzi wa madaraja na flyovers kama walivyofanya Addis Ababa na Tunisia,” anasema Dk. Mlima.

Hapa nchini AfDB wametoa fedha za ujenzi wa barabara ya Dodoma-Singida, Arusha-Namanga na nyingine kadhaa.