Mshambuliaji wa Difaa El Jadida ya Morocco, Simon Msuva, ametajwa katika orodha ya mastaa kutoka Afrika Mashariki ambao wanaweza kumfuata Mbwana Samatta katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Samatta aliweka historia mwanzoni mwa mwaka huu kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza EPL alipojiunga na Aston Villa akitokea Genk ya Ubelgiji kwa ada ya paundi milioni 10.

Uhamisho huo uliifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu ya Afrika Mashariki kutoa mchezaji wa EPL, ikiungana na Kenya na Burundi.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na Goal Africa umebaini kuwa nchi za Afrka Mashariki zina vipaji vingi na upo uwezekano wa wachezaji kadhaa kutoka eneo hilo kujiunga na EPL.

Msuva, ambaye ni winga wa zamani wa Yanga ya Dar es Salaam, ambaye hivi sasa anakipiga katika timu ya Difaa El Jadida ya Morocco, anatajwa katika orodha ya nyota hao.

Msuva ni mmoja wa washambuliaji wanaocheza pamoja na Samatta katika timu ya taifa – Taifa Stars. Mapema mwaka huu naye alitajwa kuwa yumo mbioni kujiunga na moja ya klabu kubwa Ulaya lakini mipango ikaharibika.

Benfica na Leganes zilitajwa kama timu ambazo zilikuwa zinahitaji huduma ya winga huyo mwenye kasi awapo uwanjani. Hata hivyo, wakati mipango yake ya uhamisho ikiendelea, mabosi wake wa sasa walimshauri aendelee kubakia Morocco.

Kutokana na utulivu alionao winga huyo mwenye miaka 26 hivi sasa, anaonekana hawezi kulazimishwa kuhama ingawa ili ajiunge na EPL anapaswa kwanza kupitia katika nchi nyingine ambako ataonyesha makali yake.

Mchezaji mwingine anayetajwa ni Michael Olunga, ambaye hivi sasa anahesabika kama mchezaji wa pili kwa thamani kutoka Afrika Mashariki nyuma ya Samatta.

Olunga ni mchezaji mwenye nguvu na akili na anatajwa kuwa na uwezo wa kucheza EPL au katika ligi nyingine barani Ulaya, jambo ambalo tayari amekwisha kulifanya.

Itakumbukwa kuwa Olunga tayari amekwisha kufunga ‘hat trick’ katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu nchini Hispania – La liga – dhidi ya Las Palmas Januari 2018.

Hata hivyo, maendeleo yake yamekuwa mabaya katika miaka miwili iliyopita na akalazimika kukimbilia Japan kwenye Ligi Daraja la Pili. Ingawa ligi hiyo ina fedha sana, lakini haijamsaidia Olunga kuinua kipaji chake.

Alifunga magoli mawili wakati timu yake ya Kashiwa Reysol ikiichakaza Kyoto Sanga kwa 13-1 Novemba mwaka jana, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 anahitaji kucheza timu kubwa zaidi ili kujenga jina.

Eric Ouma naye anatajwa kama nyota anayeweza kujiunga na Samatta kuichezea EPL. Ni mlinzi wa pembeni wa Kenya, ambaye amepewa jina la utani ‘Marcelo’, akifananishwa na beki kisiki wa Real Madrid ya Hispania.

Januari Ouma alijiunga na AIK ya Sweden na iwapo ataonyesha makali katika ligi hiyo haitashangaza iwapo timu za Uingereza zitamhitaji.

Nyota wa Uganda mwenye umri wa miaka 19, Allan Okello, naye anatajwa kama mmoja wa nyota ambao wanaweza kucheza EPL, wakifuata nyayo za Samatta.

Kijana huyo alihamia Paradou SC ya Algeria mwezi Januari akitokea KCCA ya Uganda, akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.

Timu hiyo ina academy inayoheshimika kwa kuwapika vijana ambao baadaye wanaibuka kuwa moto wa kuotea mbali.

Okello ni mchezaji bora wa Uganda mwaka uliopita, na aliifungia KCCA magoli 39 katika mechi 112 alizoichezea.

Akiwa na umri wa miaka 22, Farouk Miya, amekwisha kuiongoza Uganda katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2017 nchini Msri na tayari ameshaanza kutikisa katika ligi ndogo ndogo barani Ulaya.

Agosti alihama kutoka HNK Gorica ya Croatia na kukimbilia Konyaspor ya Uturuki ambako tayari ameshaanza kuonyesha makali yake kwa kufunga magoli matano katika mechi 19 za ligi alizocheza msimu huu na kuongoza orodha ya wafungaji katika klabu yake.

Inaaminika kuwa uzoefu anaoupata katika Super Lig utamwezesha Miya kuwa mmoja wa nyota maarufu kwenye EPL pale atakapoamua kujiunga nayo.