DAR ES SALAAM
Na Regina Goyayi
Msanii wa filamu nchini, Stanley Msungu, amewatoa hofu mashabiki wake akisema kinachoonekana jukwaani si maisha yake halisi.
Akizungumza na JAMHURI jijini hapa, Msungu anasema kumekuwa na shaka miongoni mwa mashabiki wa filamu wakihisi kwamba anachokiigiza ni uhalisia wa maisha yake.
“Hapana. Kinachoonekana ni maigizo, wala si tabia yangu. Watu wasinihisi vibaya,” anasema msanii huyo aliyeshiriki katika tamthiliya kadhaa zikiwamo mbili za kuvutia; ‘Jua Kali’ na ‘Tunu’.
Uigizaji wake katika filamu hizo umeendana, akionyesha tabia inayodhaniwa kuwa ni mbaya ya kupenda sana mapenzi (wanawake), hivyo kuzusha hisia kwamba hivyo ndivyo alivyo hata katika maisha halisi.
“Inapaswa kufahamika kwamba katika michezo ya kuigiza, si muigizaji anayejipangia ‘character’ (nafasi au eneo la kuigiza). Mimi mwenyewe sipendi lakini nilijikuta nimepewa nafasi hiyo.
“Wala si kwamba ninaiweza sana! Imetokea tu katika ‘story’ hizi mbili nikapangiwa kuigiza namna ile. Nafasi zinafanana. Kwa kuwa watunzi wanahitaji mtu katika nafasi hiyo, ikanibidi kutekeleza majukumu hayo. Ujue hii ni kazi yangu, si kwamba ni tabia yangu,” anasema.
Msungu anasema kwa kuwa anaelewa anachokifanya, haoni kama kuna changamoto zozote za kumkwaza awapo kazini, labda kama kuna wanaochukia au kumchukia binafsi kutokana na nafasi anazopewa kuigiza.
“Msanii kama kioo cha jamii, kazi yetu ni kufikisha ujumbe mahususi kwa jamii inayolengwa na ukiona mtu amekasirika, basi ufahamu kwamba kwa asilimia kubwa ujue ujumbe umemgusa.
“Kwa hiyo hayo ni mafanikio na furaha kwa muigizaji. Kwamba kazi imefanyika sawasawa na ujumbe uliotakiwa kufika umewagusa na kuwafikia walengwa. Wamekipata kilichokusudiwa. Naomba nisichukuliwe au kudhaniwa kuwa ndivyo nilivyo,” anasema.
Pamoja na hali hiyo, Msungu anasema anamshukuru Mungu kwa kuwa kwa upande wa familia yake, ndugu na jamaa zake wa karibu wamekuwa wakimtia moyo katika kazi yake.
“Hata watoto wangu wanatazama kazi zangu na ninapokosea hunikosoa wakihoji; hapo kwa nini hukufanya hivi, ila imefanya vile?
“Ni jambo jema sana hili. Pia wanaelewa kuwa hiyo ni moja ya kazi zangu ambazo zinanipatia riziki na wao wapate mahitaji yao,” anasema.
Kwa upande wa uigizaji, Msungu anasema anajiamini, na kwamba nafasi yoyote atakayopewa anaimudu, hasa kama atapangwa na mtu anayeelewa nini cha kufanya.
“Kazi hugeuka kuwa ngumu kidogo iwapo ukipangwa na mtu ambaye haimudu nafasi aliyopewa. Hapo hata wewe mwenyewe kiwango chako kitaonekana kushuka. Lakini mkikutana wote mnajitambua! Huwa safi sana,” anasema.
Anamtaja Godliva kama mmoja wa wasanii wa kike ambao wakipangwa naye kufanya kazi hufarijika na kufurahi. “Mashabiki watarajie kazi nzuri zaidi zinafuata,” anasema.