Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Mbunge wa Geita, Joseph Musukuma amesimama bungeni leo asubuhi akiomba mwongozo wa Spika kuhusu mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo mkoani Dar es Salaam ulioanza leo, akisema kuwa watoka maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya kupata bidhaa lakini maduka yamefungwa.

Hata hivyo, Naibu Spika, Mussa Zungu amemjibu kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na viongozi wa wafanyabiashara na kwamba taarifa rasmi ya Serikali kuhusu mgomo huo itatolewa baada ya vikao hivyo.

“Naomba nianze kutumia mwongozo kwa kutumia lugha ya Dar es Salaam, wanasema kuwa kazini kwako kuna kazi na kwamba kumekuwa na kipeperushi ambacho kinatokea mitandaoni kuwa kuanzia Jumamosi kuhusiana na wafanyabiashara wa Kariakoo na sehemu nyingine nchini kufunga maduka Jumatatu ambayo ni leo.

“Tunapozungumza sasa hivi, Kariakoo imefungwa hakufanyiki biashara na sisi wabunge kuna mambo ambayo tuliya-‘rise’(tuliyaibua) katika michango yetu. Tunatambua kuwa kamati ya wafanyabiashara ipo hapa kufanya mazungumzo na Serikali kutatuliwa matatizo yao.” amesema.

Ameomba mwongozo kuhusu kauli ya Serikali kuhusiana kugoma kwa wafanyabiashara wa Kariakoo na kwamba watu wao kutoka vijijini wamekwenda Kariakoo kufuata mahitaji wamekuta Kariakoo maduka yafungwa.

“Wengine hawana nauli wanaanza tena kuomba tena kwetu wabunge, nilikuwa naomba mwongozo wako ni nini kauli yako kuhusiana na wafanyabiashara kufunga maduka,” amesema.

Akijibu mwongozo huo, Zungu amesema anafahamu juzi Musukuma alizungumzia suala hilo na kwamba Serikali na wafanyabiashara wanakutana na kwamba taarifa kamili wataipata baada ya kikao hicho kumalizika.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, wanalamikia kuchoshwa na vitendo wanavyofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mwisho