Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea
Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma Jacklin Ngonyani Msongozi amewataka wanawake mkoani humo kujitokeza kugombea nafasi za mwenyekiti wa Serikali za Mitaa ili kukuza usawa wa kijinsia na kuimarisha demokrasia ndani ya nchi.
Msongozi ameyasema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na wanawake wengi kwenye nafasi za maamuzi ili walete mabadiliko chanya katika jamii.
Amesema kuwa uwepo wa wanawake katika uongozi unaleta mtazamo mpya na unasaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na jamii nzima kwa ujumla na kufanikisha malengo ya maendeleo na kwamba uongozi wa pamoja ni muhimu katika kujenga jamii imara na si vinginevyo.
“Ndugu zangu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji, vitongoji niwaombe sana wanawake wenzangu mjitokeze kwa wingi Kuwania nafasi hizo kwa sababu wanawake tunaweza, wala msiogope lolote kwenye kugombea tuseme tunaweza na chenji inabaki wapo wanawake wengine wanauwezo lakini hawatambui kama wanauwezo ni jukumu letu sisi ambao tunaona anaweza twende tukamshauri ili aweze kugombea na wewe ambaye unaona unaweza kugombea jitokeze “amesema Mbunge Msongozi.
Hata hivyo amewaasa wananchi kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani kumekuwepo na wimbi kubwa sana ambalo linahusiana na maswala ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii inayotuzunguka jambo ambalo halikubaliki na sio mila zetu na desturi yetu watanzania.
Amesema kuwa ukatili wa kijinsia unajumuisha vitendo kama vile unyanyasaji wa kimwili ,kingono na kisaikolojia dhidi ya watu wa jinsia fulani na kwamba sababu za ukatili wa kijinsia zipo nyingi ikiwemo ukosefu wa Elimu,unyanyasaji wa kutumia nguvu, mitazamo potofu kuhusu jinsia na mambo menginw mengi hivyo ni jukumu la kila Mmoja wetu kukemea vitendo hivyo.