Wiki iliyopita makala hii iliishia pale ambapo Gurumo alipofika katika bendi hiyo akawa kiongozi wa bendi sambamba na kuasisi mtindo wa ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’. Mtindo huo ni wa asili ya ngoma za Kizaramo.
Muda mfupi, Hassan Bichuka, naye aliondoka katika bendi ya Juwata kwenda kuungana na Gurumo katika bendi ya Mlimani Park Orchestra.
Baada ya Bichuka kuondoka, uongozi ukamchukua mwimbaji aliyekuwa akishabihiana naye kwa sauti, Shaaban ‘Kamchape’, akitokea katika bendi ya Dodoma International ya mjini Dodoma.
Gurumo alirejea tena katika bendi yake ya Juwata mwaka 1991, akapewa wadhifa wa kuwa kiongozi wa bendi hiyo, baada ya kupiga muziki katika bendi ya Mlimani Park Orchestra pamoja na Orchestra Safari Sound (OSS) kwa nyakati tofauti.
Nyimbo walizotoka nazo zilikuwa ‘Nidhamu ya Kazi’, ‘Ete’, ‘Queen Kasse’, ‘Mariamu Ninakujibu’, ‘Usia wa Baba’, ‘Msafiri Kafiri’, ‘Tupa Tupa’, ‘Ndugu Kassim’ na nyingine lukuki.
Baadaye bendi hiyo ilibadilishwa jina na kuwa OTTU Jazz kufuatia kubadilika kwa jina la Chama cha Wafanyakazi kuwa OTTU. Hakuna ubishi kwamba bendi ya OTTU Jazz au kwa jina jingine wakajiita ‘Baba ya Muziki’, ilitikisa Jiji la Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla wakipiga kwa mtindo wa ‘Msondo Ngoma’, ‘Magoma Kitakita’ au ‘Mambo Hadharani’.
Wakati huo ilikuwa katikati ya wimbo wapenzi na mashabiki wa Msondo walikuwa wakiimbishwa kibwagizo cha “Msondo Yee, Msondo Waa…” Wapenzi walikuwa wakiitikia: “Afyaaaa.”
Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake katika Ukumbi wa Amana uliopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki kama vile Joseph Lusungu, Mnenge Ramadhani, Muhiddin Maalim, Hassan Rehani Bitchuka, Saidi Mabera na TX Moshi William, Nicko Zengekala, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, Mustapha John Ngosha, Suleiman Mwanyiro ‘Computer’, Tino Maselenge (Masinge) ‘Arawa’, Abdull Ridhiwan Pangamawe, Roman Mng’ande ‘Romario’ na Athumani Momba.
Wengine ni Salehe Bangwe ‘Mwana Kigoma’, na bila kuwasahau Huruka Uvuruge na Said Mabera mpiga solo mahiri ambaye tangu ajiunge katika bendi hiyo hajathubutu kuondoka.
Baada ya Hospitali ya Amana kupanuka, OTTU Jazz walitakiwa kuondoka kwa kile kilichodaiwa ni kuwabughudhi wagonjwa kwa makelele ya vyombo vya muziki wao. Hivyo walilazimika kuhamia katika Ukumbi wa AfriCenter, uliopo Barabara ya Kigogo.
Baadhi ya nyimbo ‘zilizogongwa’ na OTTU Jazz zilikuwa ‘Kicheko’, ‘Mawifi Mnanionea’, ‘Ndoa Ndoana’, ‘Nimezama katika Dimbwi,’ ‘Mti Mkavu’, ‘Wabakaji’, ‘Tabu’, ‘Pricila’, ‘Penzi la Mlemavu’, ‘Piga Ua Talaka Utatoa’, ‘Tuma’, ‘Wapambe’, ‘Asha Mwana Sefu’, ‘Ajali’, ‘Mtanikumbuka’, ‘Barua ya Kusikitisha’, ‘Mwana Mkiwa’, ‘Kalunde’, ‘Kaza Moyo’, ‘Jesca’, ‘Kwenye Penzi’, ‘Binti Maringo’, ‘Dalili’ na nyingine nyingi.