Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ujio wa msimu wa sita wa Tamasha la michezo la Ladies First umetambulishwa jana jijini Dar es Salaam.

Tamasha la Ladies First ni tukio la kimichezo lilioanzishwa kwa lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake katika michezo.

Tamasha hilo liliasisiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 ikiwa ni sehemu ya maono ya mwanariadha mkongwe Juma Ikangaa ambaye alikusudia kutilia mkazo ushiriki wa wanawake katika michezo.

Akizungumza jana katika mkutano na wanahabari, Mtendaji mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha amesema kuwa kwa msimu wa mwaka wataendesha tamasha hilo kwa kuzingatia umri kwa washiriki ambapo wamelenga kugusa vijana wadogo ili kuibua vipaji vya wale ambao bado ni wadogo.

“Pamoja na kwamba kila mwaka tunafanya mashindano haya kwa mwaka huu tumelenga kuwanoa vijana na kuibua vipaji ambapo tumeona wengi wanaotoka kwenye mashindano wanaenda mbali zaidi.

Kwa mwaka huu tumeweka ukomo katika swala la umri na hivyo tutakuwa na wanawake vijana ambao wako chini ya miaka ishirini, tunataka kuibua vipaji zaidi kwasababu miaka mingi tumekuwa tukitoa uhuru wa kila mtu kuja lakini kwa mwaka huu tumeona tulenge pia kuibua vipaji vya wale ambao bado ni wadogo.”

Aidha kwa upande mwingine pia mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Kitaifa la Japani (JICA) ambao pia wameshiriki kuandaa tamasha hilo kwa mwaka huu, Bwana Ara Hitoshi nae ameongeza kuwa tamasha hilo limekuwa jukwaa muhimu la kutoa fursa kwa wanawake na wasichana na kuchochea usawa wa kujinsia katika michezo huku kukishuhudiwa mafanikio muhimu yaliyofikiwa na wanawake katika michezo.

“Kwa miaka kadhaa Ladies First limekuwa jukwaa muhimu kutoa fursa kwa wanawake na wasichana na kuchochea usawa wa kujinsia katika michezo. Kila toleo la tukio limechangia kupunguza pengo la uwakilishi wa wanawake katika michezo, hasa nafasi ya uongozi na mashindano ya riadha ambapo tumeshuhudia mafanikio muhimu. Mfano mmoja wa kuvutia ni wanariadha wa kitanzania kufanikiwa kwenye mashindano ya kimataifa. Wanariadha kama Magdalena Shauri na Jackline Sakilu waliowahi kushiriki katika mashindano ya awali ya Ladies First walishiriki katika Olimpiki za Paris mwaka 2024.”

Aidha pia mwanariadha mkongwe wa kimataifa wa kitanzania Juma Ikangaa amewaasa watoto wa kike kuitumia vizuri fursa ya tamasha la hilo kwani limekuja kuwakwamua vijana hao kuelekea katika dunia ya fursa kwa wasichana huku akisisitiza michezo ni ajira isiyopimika.

Ufunguzi rasmi wa tamasha hilo la Ladies first utafanyika jumamosi hii ya Novemba 23 katika uwanja wa Benjamin mkapa shughuli itakayoongozwa na Waziri wa Utamaduni, sanaa na michezo, Dkt: Damas Ndumbaro.