Na Lookman Miraji

Msimu wa 25 wa maonyesho ya tiba yamezinduliwa rasmi hapo jana jumanne ya oktoba 9 katika ukumbi wa diamond jubilee ulioko upanga, Dar es salaam.

Maonyesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka ambapo huandaliwa na kampuni expo kwa kushirikiana na mamlaka ya maendeleo ya biashara nchini(Tantrade).

Ufunguzi wa maonyesho hayo ulihudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini pamoja na wataalamu wa mambo wa kiafya kutoka taasisi mbalimbali.

Hafla hiyo ya ufunguzi wa maonyesho hayo yaliongozwa na Dkt: John Regasha ambae ni mkurugenzi wa huduma za tiba kutoka hospitali ya taifa ya muhimbili.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa maonyesho hayo Dkt:Regasha amesema kuwa kupitia maonyesho hayo wanafurahi kuona yamewashawishi watu mbalimbali wakiwemo mabalozi huku akielezea kwa namna alivyojionea ujio wa vifaa vya kisasa na matumizi yake katika ulimwengu wa tiba ya mwanadamu.

“Leo tumekuja kutembelea mabanda haya ya maonyesho tukiwa na ujumbe wa mabalozi kutoka nchi mbalimbali ambao pia na wenyewe wamekuja kujionea maonyesho haya”

“Mimi nikiwa kama mgeni rasmi nimefanikiwa kutembelea na kujionea jinsi ambavyo huduma ya vifaa tiba, maabara na madawa kwenye upande wa uchunguzi vikiwa vimetoka katika nchi mbalimbali ili kuweza kuonesha nini kinaendelea katika ulimwengu wa tiba ya binadamu”

Aidha Dkt: Regesha aliongeza kuwa maonesho hayo yamekuja wakati ambao serikali pia wameweka mkazo kusogeza huduma kwa wananchi ambazo zinafikika kwa urahisi na zenye unafuu wa kulipiwa.

Mbali na hatua hiyo pia Mkurugenzi huyo aliendelea kwa kuhamasisha watoaji huduma za kiafya kutembelea maonyesho hayo ili kujenga uhusiano wa kibiashara ambao utasaidia unafuu wa tiba kwa wananchi uweze kuendelea.

“Kubwa zaidi katika maonesho haya ni kuongeza ushirika kati ya sekta binafsi na sekta za umma ambapo wote wakifanya kazi pamoja kuna mchango mkubwa unaweza ukafanikishwa kwa kutoa huduma bora zaidi”

“Kupitia juhudi kubwa za serikali katika kufungua vituo mbalimbali vya afya kuanzia katika ngazi ya mkoa, wilaya na kata pamoja na wamiliki wa vituo binafsi vya afya hii ni nafasi yao kuja kuangalia hizi teknolojia ambazo zinaendelea na kufanya ushirika huu ili tuweze kufanya gharama za afya kuwa nafuu na zaidi”

Maonesho hayo ya tiba yalifunguliwa rasmi hapo jana huku yakihusisha makampuni mbalimbali yanayojishughulisha huduma za utoaji na usambazaji wa vifaa vya tiba kutoka sehemu mbalimbali duniani ambapo maonesho yataendelea kwa takriban siku mbili mpaka oktoba 11 mwaka huu.

Please follow and like us:
Pin Share