Katika miaka ya hivi karibuni kosa la utakatishaji fedha limesababisha watu wengi kuwekwa mahabusu kwa kipindi kirefu, kwa sababu kwa mujibu wa sheria, kosa hilo halina dhamana.
Ingawa serikali ilikuwa na dhamira njema ilipotunga sheria hiyo, lakini baadhi ya wataalamu wa sheria wanasema sheria kama hiyo ni mbaya kwa sababu kadhaa.
Kwanza, inamnyima uhuru mtuhumiwa na kumfanya aonekane mwenye hatia wakati kesi dhidi yake haijasikilizwa, kwani analazimishwa kuwekwa ‘kifungoni’ kwa kipindi kirefu bila kupata fursa ya kusikilizwa. Pili, dhamana inafungwa na hati inayotolewa na DPP ambaye mara nyingi ndiye husimama upande wa mlalamikaji; Serikali.
Karibu kesi zote za utakatishaji zimetumia muda mwingi kuanza kusikilizwa, kwani zinafunguliwa kabla upelelezi haujakamilika na mamlaka zinazohusika hutumia muda mrefu kufanya upelelezi ili kesi hizo zianze kusikilizwa. Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, anataka upelelezi ukamlishwe kwanza ndipo kesi zifunguliwe na kila kosa liruhusiwe kudhaminika.
Pili, sheria hiyo inainyima Mahakama uhuru wa kuamua kuhusiana na masuala yanayoletwa mbele yake, ikiwamo dhamana kwa watuhumiwa. Sheria imetamka moja kwa moja kuwa kosa hilo halina dhamana, Mahakama inajikuta imefungwa mikono.
Hapo ndipo Jaji Mkuu anapojenga hoja yake ya kutaka suala hilo liangaliwe upya ili kuipa Mahakama uhuru unaostahili katika kutafsri sheria na uendeshaji wa mashtaka. Kimsingi, katika utekelezaji wa majukumu yoyote makubwa, hasa yanayohusu utoaji wa haki, ni vema chombo kinachofanya hivyo kiwe na uhuru kamili katika kufikia uamuzi wa masuala hayo.
Hivyo, haipendezi kuona katika hili Mahakama ikibanwa na kushindwa kutoa uamuzi kuhusu hatima ya watu wanaoshitakiwa.
Katika mazingira kama haya, inaonekana kuwa Mahakama inatumiwa kuhalalisha ambacho Serikali inakitaka. Inaonekana kuwa Serikali imetunga sheria za aina hii kukwepa kiunzi kwa Mahakama kuwa na uhuru wa kuamua kuhusu dhamana ya watuhumiwa.
Ni muhimu hili litazamwe upya kama anavyopendekeza Jaji Mkuu, hasa ikizingatiwa kuwapo malalamiko yanayoibuka kuwa sheria hiyo inatumika kama fimbo ya kuwaadhibu watu kabla hawajahukumiwa na mahakama.
Tumeshuhudia jinsi watu wengi walivyosota magerezani kwa muda mrefu wakiwa mahabusu baada ya kushitakiwa chini ya sheria hii.
Kwa kutunga na kuitumia sheria hiyo inayoondoa haki ya dhamana, Serikali inaweza kudhani kuwa inatumia haki yake kwa kuhakikisha wale wanaovunja sheria wanashughulikiwa ipasavyo, lakini kwa upande mwingine sheria hiyo inaweka rekodi mbaya kwa kuendelea kuwa na sheria ambayo inanyima haki za msingi za binadamu kwa watuhumiwa.