*Atumia mbinu chafu kupoka haki ya mke mdogo wa kaka yake, mtoto wa miaka mitatu

Na Anthony Mayunga, JamhuriMedia, Serengeti

Katika hali isiyotarajiwa, Esther Iroga, msimamizi wa mirathi ya Ramadhani Manyabu, anadaiwa kujirithisha magari mawili kinyume cha utaratibu.

Esther alichaguliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya kaka yake, Manyabu, aliyeacha wajane wawili, watoto watatu na mali kadhaa.

Miongoni mwa mali zilizoachwa na Manyabu ni magari mawili yaliyopaswa kurithiwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye mama yake ni mke mdogo.

Manyabu, aliyekuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alifariki dunia Mei 28, 2023.
Miongoni mwa mali alizoacha ni nyumba mbili; moja ikiwa Tegeta jijini Dar es Salaam na nyingine ipo Mugumu eneo la MCU pamoja na kiwanja kimoja kilichopo Kyambahi, Serengeti.

Pia ameacha magari mawili; Nisan Extrail T 251 EAL na Noah – Toyota T 148 DKW, pikipiki aina ya Fekon na ng’ombe 13.
Akizungumza na JAMHURI mjini Mugumu, mke mdogo wa Manyabu, Sophia Boniphace (28), anasema wakati mauti yanamkumba mumewe yeye alikuwa na ujauzito wa mtoto wa pili.

“Tayari nimeshajifungua ingawa baadhi ya ndugu zake (ndugu wa mumewe) wanasema hawamtumbui. Kwamba wanayemtambua ni mtoto mmoja aliyekuwa amezaliwa.

“Kwa hiyo katika mgawo wa mirathi kwa watoto, nyumba zote mbili wakapewa watoto wa mke mwenzangu ambao ni vijana wakubwa wenye umri za zaidi ya miaka 18.

“Yaani ile ya Dar es Salaam aliyokuwa anaishi mke mwenzangu pamoja na ya hapa Mugumu niliyokuwa ninaishi mimi tangu nilipoolewa. Sasa nimebaki ninahangaika na watoto, sina pa kuishi,” amesema Sophia.

Mgawo ulivyofanyika

Sophia anasema kwamba magari yalipaswa kurithiwa na mwanae mdogo mwenye umri wa miaka mitatu ili yauzwe kisha ajengewe nyumba.

Hata hivyo, ni zaidi ya miezi minne sasa tangu kukamilika kwa shauri la mirathi lakini msimamizi, Esther, hajakabidhi magari hayo kwa mtoto wa Sophia huku jitihada za ndugu kumtaka arudi Mugumu wafanye kikao kupitia upya mgawo wa mali zikigonga ukuta.

Sophia anadai kuwa mihtasari iliyotumika kufanya mgawo wa mirathi imeghushiwa hivyo kumweka yeye kando.
JAMHURI limefanikiwa kuuona muhtasari wa mgawo ambapo George Ramadhan Hamisi, kijana mkubwa wa Manyabu, amepewa pikipiki, ng’ombe watatu na nyumba iliyoko MCU Mugumu.

Nyumba hiyo ndiyo aliyokuwa akiishi Sophia kabla ya kifo cha mumewe.
Mtoto mwingine wa mke mkubwa, Janeth Ramadhani Hamisi, amepewa ng’ombe watatu na nyumba iliyoko Tegeta, Dar es Salaam walikokuwa wanaishi na mama yao.

Mtoto mkubwa wa Sophia, Paulo Ramadhani Hamisi, amepewa ng’ombe wanne, kiwanja kilichoko Kyambahi na magari mawili kwa maelekezo kwamba mali hizo zitasimamiwa na msimamizi wa mirathi, Esther, ayauze na kumjengea nyumba katika kiwanja chake kwa kuwa yeye hakupata mgawo wa nyumba.

Mgawo wa ng’ombe watatu pia ulielekezwa kwa Thomas Mwita, kwa madai kuwa ni maelekezo ya Manyabu, kwa kuwa huyu ndiye aliyekuwa akimhudumia alipokuwa mgonjwa.

“Mgawo ulipomalizika, shida ikaanza. Mke mwenzangu akaniondoa ndani ya nyumba niliyokuwa ninaishi kwa kisingizio cha mtoto wake. Ile nyumba ya Tegeta, wamepangisha na kuhamia Mugumu.

“Chumba nilichopewa kuishi kwenye moja ya nyumba zilizopo ndani ya kiwanja hicho na kingine nilichopangisha ili niwe napata pesa ya mahitaji yangu na ya wanangu, msimamizi ameninyang’anya akisema anamwekea mtoto pesa benki, lakini hajawahi kufanya hivyo,” amesema.

Sasa, Sophia anadai kuwa Esther, baada ya kuchukua fedha za wapangaji wake, amechukua na magari na kuyahamishia Musoma mjini anakoishi akisema anakwenda kuyauza.

Juhudi za Sophia kufuatilia kwa shemeji zake na mawifi zimegonga mwamba, wakimwambia kuwa tatizo lipo kwa Esther ambaye hataki vikao.

“Nimefika hadi kwa mkuu wa wilaya, akanielekeza kwenda kwenye Dawati la Jinsia. Wakamwita Esther, akagoma.

“Nimewafuata wasaidizi wa kisheria, nao walipomtafuta, anawapiga chenga. Sasa nimebaki njiapanda. Nashindwa kujua hatima ya haki ya mwanangu na mimi mwenyewe.

“Niliolewa kihalali, nikanyimwa nyumba. Wakasema watauza magari wanijengee, lakini tangu mwaka jana hadi leo sipati mrejesho,” amesema.

Sophia amesema hata haki nyingine zinazotokana na utumishi wa mumewe jeshini hashirikishwi.
Akizungumza na JAMHURI kuhusu kadhia hiyo, Esther amekiri kuchukua magari hayo akisema yapo sokoni kwa sasa, lakini wanunuzi hawajapatikana.

Hata hivyo, hakuwa tayari kusema kiwango cha pesa alichotarajia kupata baada ya kuyauza wala mahali yalipo magari hayo au sababu ya kutotoa mrejesho kwa Sophia na wanafamilia wengine.

“Magari yapo tu. Mimi siyatumii. Naona mambo yanazidi kuwa mengi kutoka kila kona. Nitajitahidi kwenda Mugumu kuitisha kikao ili uamuzi upitiwe upya.

“Shida ni kwamba, nina mambo mengi ndiyo maana huwa ninaahidi lakini nashindwa kufika. Ninaomba sana unielewe,” amesema kwa msisitizo.

Alipoulizwa sababu za kutumia mihtasari feki ikiwa ni pamoja na kughushi baadhi ya saini za watu wakati hawajui kusoma wala kuandika, amesema:

“Kwa kweli hili jambo linazidi kuwa gumu. Ninaomba niende Mugumu tuyamalizie huko nyumbani. Mimi nilijua tumefanya na kumaliza kumbe kuna mambo hivi!” anashangaa.

Ndugu wamshangaa msimamizi

Sophia Kisiri, dada mkubwa wa Esther, ameliambia JAMHURI akisema: “Mke mdogo anastahili kupata nyumba moja na gari, maana aliolewa na mdogo wetu mwaka 2021 kwa mahari ya ng’ombe sita.

“Mumewe akasema yeye ndiye atakayeishi kwenye nyumba ya Mugumu. Katika mgawo kulifanyika mbinu za ovyo kutaka kupoteza haki zake na wanae. Kweli mtoto wa miaka miwili unampa urithi wa magari wakubwa unawapa nyumba?”

Anadai alishangaa kusikia amechukua magari yote na anayatumia kwa shughuli zake huku familia ikipata shida, na kwamba baada ya watu mbalimbali kutoafikiana kuhusu mgawo, waliomba kikao kifanyike wapitie upya; lakini Esther hataki.

Mchungaji Paulo Nyambarya, mkazi wa Kyambahi ambaye ni kaka yake Esther, amesema kwa masikitiko:
“Wakati wa uhai wake, mdogo wangu aliwahi kuniambia kuwa akifa nyumba ya Mugumu apewe mke mdogo na ya Tegeta apewe mke mkubwa, na kila mmoja apewe gari moja, lakini kilichofanyika ni aibu kwa familia.”
Anashangazwa na jeuri ya mdogo wake, Esther, kuchukua magari ya marehemu wakati yeye si sehemu ya warithi.

Josephat Marwa, katibu wa ukoo, anakiri kuwa mgawo ulitawaliwa na kampeni chafu ambazo sasa zinawatesa kifamilia, kwa kuwa hata muhtasari alioandika yeye si uliotumika mahakamani.

“Siku moja Esther aliniomba muhtasari niliouandika akisema kuna marekebisho. Nikampa. Toka hapo sijawahi kuuona mpaka leo! Huu unaonionyesha ni mwingine kabisa,” amesema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha MCU, Emmanuel Sagonge, anakiri kushiriki vikao hivyo kama kiongozi wa eneo, akisema mazingira yake yalikuwa magumu ndiyo sababu wakafikia kufanya mgawo ambao kila mmoja anajiuliza na vikao havifanyiki tena.

“Ni muda mrefu umepita amechukua magari kuwa anakwenda kuuza amjengee mtoto nyumba. Hakuna kinachoendelea. Hii familia inataabika.

“Nilimuuliza katibu wa ukoo, naye anaonekana kukata tamaa maana tangu wakati wa kikao alionyesha kuwa kinyume cha uamuzi huo. Wakamuona adui, hawampi ushirikiano akiitisha mkutano,” amesema.

Mkurugenzi wa Shirika la Geitasamo Paralegal Organization (GEPAO), Gabriel Simion, amesema Sophia alifika kwake kuomba msaada wa kisheria, akampigia simu Esther akiomba taarifa iliyoandikwa kurudisha mahakamani, akadai kuwa hana.

“Hapa Tanzania mirathi huongozwa na sheria ya serikali, mila na dini ya Kiislamu. Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 Kifungu cha 10 imetamka kwamba hakuna mtu atakuwa na haki ya kumnyima mtoto haki ya urithi wa mali ya wazazi wake. Niliomba aje tuelimishane kama kuna wosia au la, lakini kwa kuwa alikuwa anajua anachokifanya amekaidi,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share