Na Eleuteri Mangi, JamhuriMedia, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Gerson Msigwa, amekutana na watumishi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa ambapo amewasisitiza watumishi hao wawe wabunifu na wachukue hatua kulinda maadili ya Mtanzania.
Katibu Mkuu Msigwa amesema hayo alipokutana na kufanya kikao na watumishi hao Oktoba 9, 2023 katika ofisi ya wizara hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
“Bahati nzuri eneo hili la utamaduni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analipenda na kulipa kipaumbele, amekua akitusisitiza tulinde maadili yetu na anapenda kutangaza Utamaduni wetu na ndiyo maana anaitwa Chifu Hangaya. Kwetu sisi Rais kuwa Chifu Hangaya ni fursa ya kuhakikisha ajenda yetu ya kulinda na kutangaza Utamaduni wa Taifa letu tunaisimamia vizuri” amesema Katibu Mkuu Bw. Msigwa.
Katibu Mkuu Msigwa ameongeza kuwa wizara kupitia Idara ya Utamaduni na Idara ya Sanaa ina wajibu wa kuwaelimisha vijana ili wajue kuwa Tanzania ina Utamaduni wake na maadili yake akiwataka vijana wawe sehemu ya kulinda na kuendeleza maadili na utamaduni wa Taifa.
Katika hatua nyingine amewasisitiza atumishi hao wafanyekazi kwa bidii na kumpatia ushirikiano ili kwa pamoja wajenge mazingira wezeshi ambayo yataleta furaha na ufanisi kwa watumishi hao mahala pa kazi.