Jambazi ni jambazi, fisadi ni fisadi, tapeli ni tapeli tu. Madhara ya
vitendo vya watu hawa kwa jamii ni yale yale bila kujali kuwa wanatoka
chama tawala au upinzani. Madhara ya vitendo hivi hayaangalii kuwa mtu
huyu anajifanya mchungaji, askofu au sheikh. Hayaangalii kwamba mtu
huyu anapenda kuuza sura kwenye runinga kiasi gani. Na wala hayazingatii kuwa mtu huyu anapiga kelele bungeni kiasi gani au anajua
matusi kiasi gani.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndicho chama kikuu cha upinzani nchini. Matarajio yao ni kushika dola, na ndiyo maana siku zote wako mbele kuanika udhaifu na upungufu uliomo ndani ya chama tawala. Ndiyo maana karata dume inayochezwa na Chadema na vyama vingine vya upinzani sasa hivi ni UFISADI wa ESCROW unaonasibishwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM). Sina mgogoro na hilo. Ni wajibu wao na kama kweli wana nia ya
dhati kututoa hapa tulipo na kutupeleka katika nchi ya asali na
maziwa, basi wajitahidi kuhakikisha hili la Escrow na ufisadi mwingine
yanafikia mwisho.
Inatosha sana kwa uongozi wa juu wa Chadema kutafakari juu ya hatua
waliyochukua wana-Chadema wa Iringa kwa kumuengua Msigwa kwenye
kinyang’anyiro cha kugombea uenyekiti wa wilaya. Sababu zilizotolewa
kwa kuenguliwa Msigwa ni kujifanya msomi na mjuaji wa kila kitu; mtu
aliyejaa dharau na mchache wa kukubali kushauriwa, miongoni mwa sababu
nyingine.
Msigwa hajataka kujifunza chochote na bado anajihesabu kuwa na mvuto
kwa wananchi wa Iringa! Nitahadharishe kuwa kama Chadema wamelichoka
Jimbo la Iringa Mjini, basi wampe Msigwa kijiti.
Kupitia mikutano iliyo rasmi na ile ya vijiweni, upinzani unaonekana
kuwa na ajenda nzuri na nia ya dhati kutukwamua kutoka hapa tulipo.
Hata hivyo, upinzani utafanya makosa makubwa kama wataamini kuwa
wananchi tunawapima kwa maneno yao matamu tu. Wananchi wanaona vitendo
vyao au vya baadhi ya viongozi wa upinzani.
Peter Msigwa (nasita kumwita mchungaji au mheshimiwa), ni Waziri
Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Ni mmoja wa viongozi wa
Chadema, chama kinachoonekana mbadala wa CCM.
Komredi Freeman Mbowe amempa Msigwa kazi kuhakikisha kuwa anachunga rasilimali zetu zisifujwe na kuharibiwa hovyo. Naamini kwamba Komredi Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, hakumtuma Msigwa kwenda kuunda genge la ulaji na
mafisadi; kwenda kutetea uhuni unaofanywa na baadhi ya watu na wala
kwenda kutafuta utajiri kwa kutumia kofia ya uwaziri kivuli. Hiyo ni
dhamana na lazima aitunze na aipe heshima yake.
Naomba nisitafune maneno kwamba kama Chadema kweli inataka kuendelea
kuaminika mbele ya Watanzania, basi ingeonesha mfano kwa
kuwawajibisha watu ambao wanaonekana kukitia najisi chama kama
mchungaji huyu.
Katika kipindi cha runinga ya ITV kinachojulikana kama ‘Dakika 45’ Desemba 8,
mwaka huu, Msigwa ndiye aliyekuwa mgeni wa kipindi. Katika maswali
aliyoulizwa ni pamoja na baadhi ya kashfa zinazomhusu Lazaro Nyalandu
na James Lembeli. Kwanza, mtangazaji alitaka kujua kulikoni, kwani
siku za nyuma Msigwa alikuwa akipigia sana kelele Wizara ya Maliasili
na Utalii, lakini siku hizi amekuwa bubu.
Jibu la Msigwa likawa eti Waziri Nyalandu ametumia ‘approach’ nzuri
tofauti na wenzake ambako anamwalika katika shughuli na hafla
mbalimbali na hivyo hana sababu ya kuongea!
Hivi mtu mwenye akili anaweza kutoa jibu la kipuuzi kama hili? Ukweli
ni kwamba hii haina tafsiri nyingine zaidi ya ukweli kwamba Msigwa
anakiri kuingizwa kwenye ulaji, kwa hiyo hawezi tena kupiga kelele!
Vinginevyo, atuambie kwamba unapofadhiliwa unapata wapi ‘moral
authority’ ya kumkemea mfadhili wako.
Jibu jingine lililotia kichefuchefu ni utetezi wake juu ya matumizi
mabaya ya Leseni ya Rais iliyoruhusu kuuawa wanyamapori zaidi ya 700.
Msigwa anadai kuwa si kweli kwamba eti marafiki hawa wa Nyalandu
wameua wanyama 700, bali waliua nyati watano tu na pundamilia wawili.
Akadai kuwa picha za watoto wadogo waliokuwa wanawinda zilizotoka
katika gazeti la JAMHURI hazikuwa zao! Huyu mbunge ni wa ajabu kabisa!
Mchungaji gani mwongo namna hii? Ambacho hakusema kuwa hakikuwa cha
kweli ni juu ya nakala za vibali na nyaraka zilizokuwa gazetini.
Halafu akawafagilia Wamarekani hawa kuwa ingawa hawakutakiwa kulipa,
waliamua kulipa pesa nyingi sana serikalini! Kwa mara nyingine,
nashangaa ni vipi mtu anayejiita mchungaji anaweza kuwa mwongo kiasi
hiki!
Kwanza, Msigwa ameupotosha umma kwa makusudi kuwa eti JAMHURI
iliripoti kuuawa wanyama 700. Hamna aliyeripoti kuwa wanyama 700
wameuawa. Tulichoandika ni juu ya Leseni ya Rais iliyoruhusu kuuawa
wanyama 700. Na ni baada ya JAMHURI kuripoti uhuni huu ndipo
Wamarekani hawa walipoamua kutimka na kurudi kwao huku wakiwa wameua
nyati watano. Jibu alilotakiwa kujibu kibaraka huyu wa Nyalandu na
Wamarekani ni endapo kulikuwa na uhalali wa kutoa Leseni ya Rais kwa
familia ya Friedkin (je, wana sifa hizo?) Leseni nane zilizotolewa
ziliruhusu wanafamilia wanane kuwinda wanyama 49 kila mmoja. Kwa hesabu
za msomi Msigwa jumla ya wanyama wote itakuwa saba!
Kwa kuwa Msigwa ameamua kuwa kuwadi wa Nyalandu na Wamarekani, basi
angetusaidia zaidi kujibu maswali mengine tuliyouliza yakiwamo yale ya
uhalali wa Nyalandu kugawa vitalu kinyume cha sheria kwa marafiki zake
hawa. Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya kuibuka kashfa hii ya matumizi
mabaya ya Leseni ya Rais, tulitabiri kuwa si Msigwa wala Lembeli
ambaye angenyanyua mdomo kukemea ufisadi huu. Tuliweka wazi kuwa hili
lisingewezekana kutokana na kujengeka kwa mtandao wa ulaji kati ya
wawili hawa na Nyalandu.
Uswahiba wa kampuni za Friedkin na Nyalandu na Lembeli
unaeleweka. Tuna taarifa juu ya ufadhili wa ndege alizokuwa anapanda
Nyalandu kwa shughuli zake binafsi. Kwa upande wa Lembeli, mfano mmoja
ni ile hadidu ya rejea aliyojitengenezea kwenye ripoti ya Operesheni
Tokomeza akitaka Mkurugenzi wa Wanyamapori awajibishwe kwa kuwa eti
rafiki zake hawa wamekosa kitalu walichokuwa wanakitaka huko Makao
WMA!
Ingawa suala hili halikuwa na uhusiano kabisa na ujangili, Lembeli
hakuona soni kuliweka kwenye ripoti ili kuwafurahisha Nyalandu na
mawakala zake Wamarekani.
Huhitaji akili nyingi kugundua kuwa Msigwa naye ameingizwa kwenye
ulaji wa kampuni hizi; na kuingia kwake humo kumekuja kutokana na haja
ya kumtumia kufanikisha unyang’anyi wa kitalu cha Green Miles ambacho
Nyalandu kawakabidhi Wamarekani bila kufuata sheria za nchi.
Katika hali kama hiyo ambako Msigwa tayari kageuka bidhaa, tunatarajia
angethubutu vipi kusema lolote kuhusu uharamia wa Wamarekani hawa
kuruhusiwa kuua wanyama wetu 700? Ujasiri huo atautoa wapi? Ni kwa
sababu hiyo hiyo Msigwa aliamua kuufyata ghafla juu ya ile kashfa ya
Nyalandu kuamua kurefusha msimu wa uwindaji ili kuwafurahisha
Wamarekani hawa waliotaka waruhusiwe kuwinda mwaka mzima.
Awali, Msigwa alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari kulaani kitendo
kile akikiita ufisadi. Lakini huhitaji akili nyingi sana kugundua kuwa
baada ya kuingizwa kwenye ulaji, hakuwa na ujasiri wa kusema chochote
na ndiyo maana hata kwenye hotuba yake ya bajeti aliipotezea.
Atasemaje wakati kusema ina maana kugusa maslahi ya waajiri wake?
Swali juu ya mpango wa Nyalandu na Lembeli kuuza mbuga na hifadhi za
Taifa, Msigwa anawatetea maswahiba wake hawa akidai kuwa ni upuuzi
mtupu na kwamba eti tulitaka kuuza gazeti tu!
Afadhali basi Msigwa angeamua kukaa kimya kuliko kuropoka upuuzi huo.
Lakini kwa kuwa ameamua kuwa kuwadi na msemaji mkuu wa mabwana hawa,
basi angejibu maswali ya msingi yaliyojitokeza kwenye makala zetu
kadhaa kuhusu kashfa hii.
Atuambie rafiki zake hawa walifuata nini Afrika Kusini hata baada ya
kupata ushauri wa kitaalamu juu ya hatari ya African Parks Network
(APN)? Atuambie ilikuwaje Lembeli ambaye ni mmoja wa Wakurugenzi wa
Bodi ya APN (asasi inayotaka kukabidhiwa mbuga zetu) aiwakilishe
Serikali kwenye mapatano na asasi hiyo. Kama akili ya Msigwa haiwezi
kuyaona hayo, basi hatuna budi kurejea kuhoji ule utata wa kupata
‘division zero form four’ na hatimaye kutunukiwa digrii ya uchungaji!
Lakini wakati tunashangaa majibu ya kipuuzi ya Msigwa kwa maswali ya
Emmanuel Buhohela wa ITV, kuna haja ya kurejea historia yake kwa
ufupi ili tujue kuwa huyu ni mtu wa namna gani. Peter Msigwa amekuwa
akijipambanua kama kiongozi wa dini msomi mwenye digrii (graduate),
ingawa wapo wanaohoji uchungaji wake na kutaka kujua kuwa ni chuo
kikuu kipi ambacho hupokea wanafunzi waliofeli. ‘Mtumishi huyu wa
Mungu na msomi’ ndiye Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.
Alhamisi, Februari 13, mwaka huu, Nyalandu alipomjibu Martin Fletcher
kutokana na makala yake kuhusu ujangili kwenye gazeti la Daily Mail,
Msigwa alimjia juu huku akimtuhumu kuwa anawabembeleza majangili ambao
wanafahamika kwa majina na wapo mitaani wakiendelea na ujangili.
Msigwa alibainisha kuwa mara nyingi Nyalandu amekuwa akinukuliwa na
vyombo vya habari akidai kuwa mtandao wa ujangili unafahamika na ni
mpana unaohusisha watu wenye nguvu za pesa na huku akiwaomba
wanaojihusisha na biashara hiyo waachane nayo mara moja.
Akasema kuwa kauli hizo za Nyalandu zinaonesha dhahiri kuwa kuna watu
hawaguswi na sheria na wapo juu ya sheria. Msigwa akasema: “Majibu
haya ya Waziri (Nyalandu) yanadhihirisha kuwa mtandao huu
unaolalamikiwa na kuogopwa ndiyo unaohusisha Ikulu, wanasiasa,
watumishi wa Serikali, maafisa wanyamapori, maafisa usalama, polisi,
wanajeshi, pamoja na wafanyabiashara wakubwa, ambao wamekuwa
wakijihusisha na Serikali ya CCM.”
Akaendelea kumponda Nyalandu kuwa anatumia hisia badala ya vielelezo
kujibu hoja. Akatuhumu kuwa Serikali haichukui hatua kwa wahusika
ambao wanajulikana kwa majina na wako mitaani wakiendelea na biashara
hiyo haramu kwa kuwa wanatafuta fedha kwa ajili ya uchaguzi ujao.
Machi 23, mwaka huu, Msigwa alitoa taarifa kwa umma iliyokuwa na kichwa
cha habari kilichosema: “Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu
mazingira ya rushwa na ufisadi katika sekta ya uwindaji nchini.”
Katika taarifa hiyo, Msigwa alisema: “Ndugu wanahabari, kati ya mambo
yanayoashiria mazingira ya rushwa katika sekta ya uwindaji hapa nchini
ni kitendo cha Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
kurefusha, kinyume cha sheria, muda wa msimu wa uwindaji kuanzia
tarehe 1 Julai hadi 31 Machi kila mwaka tofauti na muda wa kisheria
ambao ni kuanzia tarehe 1 Julai hadi 31 Desemba kila mwaka. Waziri
Nyalandu ametoa agizo la kurefusha msimu wa uwindaji tarehe 19 Machi,
2014 akiwa na wamiliki wa vitalu na makampuni ya uwindaji.”
Aidha katika taarifa hiyo Msigwa akasema: “Ndugu wanahabari, jambo
linaloashiria mazingira ya rushwa zaidi ni kwamba wenye makampuni ya
uwindaji wamemmwagia sifa waziri na kusema kuwa ni mtu makini na
msikivu. Jambo hili la wenye makampuni kufurahia uamuzi wa waziri
linaonesha japo kwa mazingira kwamba wenye makampuni hao walikuwa
wakitafuta kubatilisha sheria iliyoweka ukomo wa msimu wa uwindaji
kuwa miezi sita na badala yake wanataka wawinde bila ukomo kwa ajili
ya kujinufaisha wao wenyewe.”
Mwisho akamuonya Nyalandu na kumtaka abatilishe uamuzi wake mara moja
huku akisema: “Wafanyabiashara ni wadau muhimu sana, ila ni hatari
kuwaruhusu waiburuze wizara kiasi cha kuhatarisha maslahi ya uhifadhi
wa wanyamapori.”
Mei 13, mwaka huu, wakati anawasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, Msigwa alianika
udhaifu wa Nyalandu huku akimlaumu kwa kukiuka kwa makusudi sheria na
taratibu za utumishi wa umma, kutumia vibaya pesa za umma kumwalika
Martin Fletcher wa Daily Mail nchini kama njia ya kumhonga n.k.
Msigwa akasema: “Si mara ya kwanza kwa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii, na mara
kadhaa tumeonesha kwa kiasi kikubwa udhaifu wake na kutoa vielelezo
mbalimbali vinavyotilia shaka utendaji wake kabla na hata baada ya
kukabidhiwa wizara hii nyeti!”
Ndugu msomaji, taarifa hizo za Msigwa kwa umma na hotuba yake bungeni,
achilia mbali kauli nyingine ambazo si rasmi, zinaonesha mtazamo wa
Msigwa kwa Nyalandu katika kipindi cha miezi michache tu iliyopita.
Hapa kuna vimelea vya rushwa.
Itaendelea