Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwapata watoto wawili Husna Gulam (3) na Mahdi Mohamed (4) walioibiwa na dada wa kazi kwa kushirikiana na mganga wa kienyeji nyumbani kwao Tandika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watoto hao wamepatikana Januari 14, 2025 nyumbani kwa mganga huyo Abdulkarim Shariff (43), Kimara Baruti jijini Dar es Salaam, ambapo walipelekwa Hospitali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na hawajakutwa na tatizo lolote.

Kwa mujibu wa baba mzazi wa watoto hao Mohamed Kassim, dada huyo wa kazi ambaye bado hajakamatwa, wameishi nae nyumbani kwa siku nne tu, hivyo ilikuwa ngumu kutambua kama anaweza kuwa na dhamira mbaya.

Mahojiano ya kina na watuhumiwa yanakamilishwa ili kubaini nini kiini na malengo ya tukio hilo, na watafikishwa kwenye mamlaka zingine za kisheria haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuepuka tabia ya kuchukua wasaidizi wa kazi za nyumbani wasiojua historia na tabia zao ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.