Uongozi wa Gazeti la JAMHURI unaungana na ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwenye maombolezo ya wananchi wenzetu 26 waliofariki dunia kwenye ajali iliyohusisha basi dogo (Hiace) na lori iliyotokea Mkuranga mkoani Pwani.
Tunawapa pole majeruhi (tisa) waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Tunawaombea wapone haraka waweze kurejea kwenye shughuli zao za kila siku.
Tunachukua fursa hii kutoa mwito kwa mamlaka zinazohusika kuchunguza na kutoka na majibu ya kudumu ya ajali ambazo kwa muda fulani zilianza kusahaulika nchini.
Bado tunajiuliza ni kwa namba gani Hiace iliweza kupakia abiria zaidi ya 30, ilhali uwezo wake ni abiria 12. Ajali nyingi zinatokea usiku trafiki wakiwa hawapo barabarani. Polisi watafakari kama bado ni sahihi kwao kusimamia usalama barabarani nyakati za mchana pekee.
Tunatoa mwito kwa mamlaka kusimamia vema utoaji leseni kwa madereva na ukaguzi wa magari. Ilivyo sasa stika za usalama barabara hazitolewi kutokana na ubora au uimara wa gari, bali kinachotazamwa zaidi ni biashara ya hizo stika.
Tunawapa pole wafiwa na pia tunawatakia unyonyaji wa haraka majeruhi wote. Tunaamini Tanzania bila ajali inawezekana endapo kila mdau wa usalama barabarani atatekeleza wajibu wake.