Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAPENZI wa mchezo wa Gofu nchini watakusanyika Jumapili Desemba 22, 2024 viwanja vya Dar Gymkhana ili kumjua mshindi wa mashindano ya gofu ya Lina PG Tour ambayo yana lengo la kumuenzi mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa Gofu marehemu Lina Nkya.
Mshindi ambaye atapatikana jumapili hiyo atapata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya gofu jijini Dubai, Falme za Kiarabu mwakani.
Lina Nkya anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika mchezo, huo na urithi wake umejengwa kupitia ufanisi wa kipekee, juhudi zisizo na kifani, na mapenzi kwa gofu ambayo yamehamasisha vizazi vingi.
Michuano hiyo ya gofu ya Lina PG Tour imeandaliwa na familia ya Said Nkya kwa kushirikiana na Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kwa lengo la kumuenzi mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya gofu Marehemu Lina aliyekuwa na mchango mkubwa kwenye timu na TLGU.
Lina alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliopeperusha vyema bendera ya Tanzania mwaka 2011 walipotwaa taji la Afrika Mashariki na Kati katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Dar es Salaam.
Wakizungumza Jijini Dar es Salaam Wachezaji na washiriki wamesema mashindano hayo wamepongeza uamuzi uliofanywa na familia ya Lina kwa kushirikiana na TLGU kuenzi mchango wa mchezaji huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mchezaji wa Gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Kili Gofu, Isack Wanyeche amesema michuano hiyo ni fursa na furaha kwake kushiriki na anaamini kwa msaada wa Mungu atafanikiwa kwenda Dubai na kuiwakilisha Tanzania kuputia mchezo huop.
“Kama mchezaji wa gofu wa kulipwa ni heshima kushiriki katika mashindano haya kumuenzi mchezaji mwenzetu wa zamani, tunaendelea na mashindano na tunamuomba Mungu ili niendelee kufanya vizuri ili kujiweka katika nafasi nzuri” amesema Wanyeche na kuongeza
“Tukio hili limeleta hamasa kubwa miongoni mwa washiriki. Sote tumejipanga vyema na kwa mazoezi ya ziada niliyofanya, nina imani na nafasi yangu. Jumapili, mshindi ambaye atakwenda Dubai atapatikana—natumaini nitakuwa mmoja wa washindi.” amesema
Naye Mchezaji wa gofu wa kulipwa kutoka klabu ya Arusha, Nuru Mollel amesema kuwa amejiandaa vyema kwa mashindano hayo na anaimani ataendelea kufanya vizuri.
“Mashindano haya yameandaliwa vyema na nimekuja kwa maandalizi na nimekuja kushindana,Tumefanya sehemu yetu ya kujiandaa, lakini mwishowe, tunamuachia Mungu mwenyewe, kwani yeye anajua kila kitu.” amesema Mollel
Kwa upande wake Msaidizi wa wachezaji wa gofu viwanja vya Gykhana, Habib Seif amesema kuwa kwa zaidi ya miongo minne, amekuwa nguzo muhimu katika mchezo huo.
Amesema jukumu lake limekuwa kuwasaidia wachezaji wa gofu wakati wa michezo yao, kuwahamasisha ili waweze kucheza kwa ubora zaidi hatimaye kuibuka washindi.
“Kwa miaka mingi, nimewafundisha wachezaji wengi, na bila mimi, hawawezi kucheza vizuri kama wanavyocheza. Hata wachezaji bora zaidi wanahitaji msaada wangu,” amesema.
Habib aliongeza kuwa mchango wake ni muhimu zaidi ya uwanjani kwani anashiriki katika mashindano ya wazi pia.
Mashindano hayo yanayoshirikisha wanawake na wanaume, yatafanyika kwa siku nne kuanzia leo kwa mashimo 18 kwa siku na kukamilisha mashimo 72 yatakapomalizika.