*Orodha ya kwenda Ikulu jina lake lakatwa
*Ukomo wake ni Oktoba 5 mwaka huu
*Kilio cha kina Telele, Sendeka chasikika
Jina la Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Pius Msekwa, halimo katika orodha ya majina ya watu wanaopendekezwa kushika wadhifa huo, JAMHURI imethibitishiwa.
Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-Tanzania Bara), amekuwa akituhumiwa kwa uongozi mbovu ambao Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM), amediriki kusema umevuruga kabisa Mamlaka hiyo.
Habari za uhakika ambazo JAMHURI imezipata zinasema kwamba kukosekana kwa jina la Msekwa miongoni mwa wanaopendekezwa kushika wadhifa huo, kunamfanya afikie ukomo wa uongozi ndani ya Mamlaka hiyo ifikapo Oktoba 5, mwaka huu.
Kwa kawaida Rais ndiye anayeteua mwenyekiti wa bodi kutokana na mapendekezo yanayopelekwa kwake. Wajumbe wa Bodi huteuliwa na waziri mwenye dhamana ya bodi husika.
Kung’olewa kwake kunaweza kuwa kumetokana na kelele za wabunge wengi wa CCM na wa Upinzani ambao mara zote wamehoji uadilifu wake, hasa kwa kutoa vibali kuruhusu ujenzi wa hoteli kwenye kingo za Bonde la Ngorongoro na katika mapito ya faru.
Aidha, mamlaka inayowajibika na uteuzi huo, itazingatia mabadiliko mapya yanayotaka wenyeviti wa bodi waweze kuongoza kwa kipindi kimoja cha miaka mitatu, na kama itaonekana kuna umuhimu wa kuongeza muda, basi ukomo uwe mihula miwili tu. Msekwa ameongoza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa miaka sita sasa.
Mapema mwezi huu wakati wa kujadili Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Telele aliendeleza mashambulizi dhidi ya Msekwa na kumsihi Rais Jakaya Kikwete asimwongeze muda mwingine wa uenyekiti.
Telele alisema Msekwa ameifanya Ngorongoro kama mali yake, huku akishindwa kuwasaidia watu wa jamii ya Wamaasai wanaoishi katika Mamlaka hiyo kwa mujibu wa sheria. Amerejea kauli hiyo alipozungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki kwa kusema, “Msekwa anaburuza watu, Shirika limerudi nyuma, anatoa maeneo tu kienyeki kwa wawekezaji, malisho ya wanyama anagawa, kama atamaliza muda wake Mheshimiwa Rais atuteulie mwenyekiti mwingine mwneye manufaa.”
Katika Mkutano wa Bunge uliomalizika, Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso (Chadema), alihoji matumizi ya Sh milioni 200 zilizotumiwa na bodi kwa safari za nje ya nchi wakati muda wake wa kuwapo madarakani ukikaribia ukingoni.
Jambo jingine linalozua mjadala mkali ni kutokuwapo kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, baada ya aliyekuwapo, Bernard Murunya, kuondoka. Kwa sasa Murunya ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Pamoja na Pareso, Mbunge mwingine aliyehoji kutokuwapo kwa mtendaji huyo ni Beatrice Shellukindo (Viti Maalumu-CCM).
Akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema mapendekezo ya kamati iliyoundwa kuchunguza Ngorongoro yatazingatiwa wakati wa uteuzi wa wajumbe wapya wa Bodi ya Mamlaka hiyo.
Bodi za Wakurugenzi wa NCAA kuingilia kazi za menejimenti
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Maliasili na Mazingira, Peter Msigwa (Chadema), akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo bungeni mwezi huu, alitaka kujua utekelezaji wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) baada ya kuthibitisha kuwa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inaingilia utendaji wa kazi wa menejimenti.
“Kitendo hiki ni kasoro kubwa na inapunguza uhuru wa menejimenti kutoka kwa bodi na inaleta migongano ya kimaslahi kati ya pande hizi mbili…ilithibitisha namna ambavyo bodi ya wakurugenzi ilivyojihusisha mara kadhaa katika maonyesho ya kimataifa ya utalii katika kipindi kati ya Julai 2010 na Juni 2011.
“Hali hii ni kinyume na utawala bora na Waraka wa Ikulu Na. SHC/B.40/6/21 wa Machi 28, 1994 aya ya 3 na 5. Utaratibu huu huathiri kazi za bodi za usimamizi kwa kuwa zitakuwa zimegawanyika kimtazamo na kimaslahi.
“Pamoja na Kambi Rasmi ya Upinzani kuishauri Serikali na kuhakikisha tume ya kuchunguza Bodi ya Ngorongoro akiwamo Mwenyekiti wa Bodi, Pius Msekwa, sasa ni zaidi ya siku mia tatu sitini na tano na robo yaani mwaka, tume hiyo imeshindwa kuleta ripoti ya uchunguzi ili ifanyiwe kazi, na bado serikali imeendelea kujiita serikali sikivu,” alisema Msigwa.
Msekwa ajibu mapigo
Tangu mwaka jana, Msekwa amekuwa akijibu tuhuma zinazoelekezwa kwake na baadhi ya wabunge juu ya uongozi wake wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Agosti, mwaka jana aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kumjibu Telele na wabunge wengine, akisema kwamba kauli alizotoa bungeni dhidi yake ni fitina yenye uongo ndani yake. “Ni aina ya uongo unaoitwa usongombwingo,” alisema.
“Maneno yaliyonukuliwa na magazeti kwamba yalisemwa bungeni na Mheshimiwa Telele yalikuwa na lengo la kuchafua jina langu mbele ya umma. Yalikuwa ni maneno ya kashfa dhidi yangu, yaliyojikita katika kuchafua historia ya muda mrefu ya uadilifu wangu katika kutekeleza kazi za umma nilizopangiwa katika nyakati mbalimbali na marais wangu, kuanzia Rais Nyerere hadi Rais Kikwete,” alijitetea.
Kuhusu kutokuwapo kwake kwenye mjadala wa hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema bila shaka hoja hiyo inatokana na dhana mpya iliyojengeka ya kukusanya watu wengi Dodoma kwa gharama kubwa wakati wa mikutano ya Bunge la bajeti bila sababu za msingi.
Alisema kwa kuwa alishakuwa amekutana na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, hakuona umuhimu wa kuwapo Dodoma, badala yake alipanga ratiba ya shughuli nyingine zinazohusiana na uenyekiti wake wa bodi.
Alisema kazi hizo ni pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro na si kugawa viwanja kwa wawekezaji pamoja na miradi mingine inayotekelezwa kwa fedha za NCAA ikiwamo Shule ya Sekondari ya Nainokanoka ambayo imekuwa ikijengwa kwa muda mrefu bila kukamilika.
“Hii ni kazi muhimu zaidi kuliko kukaa tu kwenye Gallery ya Bunge na kulipwa posho za kusikiliza hoja mbalimbali za wabunge zinazoelekezwa kwa Waziri,” alisema.
Msekwa alisema kimsingi bajeti ya wizara ni sehemu ya Bajeti Kuu ya Serikali ambayo ilishapitishwa na kwamba kazi wanayofanya wabunge hivi sasa kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (b) cha Katiba ya nchi ni kujadili utekelezaji wa kila wizara.
“Kwa hiyo hakuna kazi inayohitajika ya mwenyekiti kusaidia kuhakikisha kuwa bajeti ya wizara inapitishwa vizuri na Bunge, kwa sababu bajeti ya wizara inakuwa tayari imepitishwa wakati Bunge linapopitisha bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha,” alisema.
Alisema alipokutana na Kamati ya Bunge, alijibu hoja zote alizoulizwa na kamati hiyo na kwamba tuhuma zilizotolewa na Telele hazikujitokeza wakati huo. Alisema madai ya Telele kwamba alikwenda Ngorongoro kugawa maeneo ni lugha ya kuudhi ambayo inakatazwa bungeni.
Wakati Telele akichangia alisema wakati wenyeviti wenzake wote wako Dodoma yeye alikwenda kutafuta maeneo ya kujenga hoteli.
“Mwenyekiti wa Tanapa yuko hapa. Yeye hayumo humu, labda alijua kwamba tutazungumza huku, lakini kule aliko anatusikia,” alisema Telele bungeni.
Akanusha kutumia jina la Rais
Tuhuma nyingine aliyoikanusha Msekwa ni madai kwamba alitumia jina la Rais Kikwete kuhalalisha utoaji wa maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama kujengwa hoteli. Alisema Desemba 28, 2006 alikutana na Rais Kikwete pamoja na Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Murunya wakati huo, akikaimu nafasi hiyo na kiongozi huyo wa nchi aliwapa maagizo ambayo yaliwasilishwa kwenye mkutano wa bodi kwa waraka maalumu.
“Katika waraka huo, maelekezo ya Rais kuhusu haja ya kuongeza idadi ya vitanda katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yameainishwa waziwazi,” alisema. Alisema maombi ya kujenga hoteli kwenye mapitio ya wanyama yaliwahi kutolewa na Bodi iliyokuwapo wakati huo kukubali, lakini mradi ulizuiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
“Tunaendelea kutekeleza uamuzi wa NEMC kwa kutoruhusu hoteli yoyote nyingine kujengwa katika mapitio ya wanyama. Ndiyo sababu katika orodha ya viwanja vilivyogawiwa na Bodi katika mkutano wake wa 87 wa Oktoba 2007, hakuna kiwanja chochote kilichopo kwenye mapitio ya wanyama kama Mheshimiwa Telele anavyodai,” alisema.
Kuhodhi kazi za menejimenti
Msekwa alisema hajawahi kufanya kazi za watendaji na kwamba tuhuma hizo si za leo, kwani zilianza muda mfupi tu baada ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi.
Alisema baada ya siku 100 tangu kuteuliwa kwake, alimwandikia waraka Waziri husika ambaye wakati huo alikuwa Anthony Diallo akimweleza jinsi atakavyofanya kazi na kwamba amekuwa na utaratibu wa kutoa taarifa ya bodi yake kila baada ya muda fulani kwa waziri.
Alisema tuhuma hizo ziliendelea hata baada ya Waziri Jumanne Maghembe kuhamishiwa katika wizara hiyo na kwamba waziri huyo alifanya uchunguzi na kubaini kuwa hazina ukweli wowote. Msekwa aliongeza kuwa hata kikao cha bodi kilichojadili tuhuma hizo kilizitupilia mbali na kwamba anamshangaa Telele ambaye wakati huo alikuwa mjumbe kuziibua upya, hali akifahamu kwamba zilikuwa zimeshawekwa kando.
Alisema Ngorongoro haiwezi kufia mikononi mwake kwani tangu alipochukua uenyekiti wa chombo hicho ameongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato kutoka Sh bilioni 17.79 mwaka 2005/2006 hadi Sh bilioni 48.7 mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2011.
Telele: Tunamheshimu Msekwa
Telele akichangia bungeni, alisema, “Nadhani jambo hili aangalie, tunaheshimu sana Chama Cha Mapinduzi – ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na maombi yanavyokuja ya kujenga hoteli wanasema Rais amesema, Rais gani anasema kwamba tujenge hoteli aende kinyume na taratibu zilizowekwa na wahifadhi na wataalamu wa hifadhi?”
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), naye amekuwa akitoa wito bungeni wa kuvunjwa kwa Bodi ya NCCA kwa maelezo kwamba ilikuwa imekiuka ushauri wa NEMC kwa kuruhusu ujenzi kwenye mapito ya faru.