Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani (RAS), Salvera Salvatory ameishauri Bohari ya Dawa (MSD) kuwa na mikakati endelevu ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya ili kuondoa malalamiko ambayo kwa kiasi kikubwa yameanza kupungua.

Salvatory ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa MSD Kanda ya Dar es Salaam na wadau wake wa mkoa wa Pwani uliofanyika mkoani Kibaha.

“Wananchi wanafarijika sana wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakapatiwa dawa zote walizoandikiwa”.

Kiongozi huyo amekiri kuvutiwa na MSD kuwa na kitengo cha huduma kwa wateja, ambao ndio hufanya mawasiliano kwa karibu na wadau na wateja ambapo amewashauri kuhakikisha wanafuatilia malalamiko ya wateja na kufuatilia namna yanavyoshughulikiwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Miradi wa MSD Victor Sungusia ameeleza kuwa usambazaji wa bidhaa za afya mara sita kwa mwaka umesaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa jizo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya MSD Betia Kaema ameahidi kufanyia kazi maazimio yote yaliyo adhimiwa kwenye kikao hicho huku akisisitiza ushirikiano na mawasiliano ya mara kwa mara na wadau hao.