Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
BOHARI ya Dawa (MSD), imepata mafanikio makubwa hadi Juni mwaka huu wa 2024 kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuongeza nguvu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza mipira ya mkono (gloves) kilichopo Makambako mkoani Njombe, maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya na ujenzi wa ghala kubwa la kisasa yaliyopo Dodoma.
Mavere amesema kuwa kutokana na nguvu hiyo imechochea mageuzi makubwa katika kuboresha uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwenda vituo vya kutolea huduma vya umma na binafsi kufika kwa wakati na kwa muda mfupi ukilinganisha na kipindi cha nyuma.
“Hadi Juni 2024, Bohari ya Dawa imepata mafanikio mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake. Mafanikio hayo yamepatikana katika maeneo mbalimbali kama kuongezeka kwa utimizaji wa mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya (dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi).
“Bohari ya Dawa imeendelea kuhakikisha mahitaji ya vituo vya kutolea huduma za afya yanatimizwa kwa mujibu wa maombi yao. Kutokana na kuimarika kwa utendaji, utimizaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba kwa vituo vya kutolea huduma za afya umeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2022/23 hadi asilimia 84 mwaka 2023/24, hivyo bidhaa nyingi kupatikana kupitia MSD,” amesema.
Mkurugenzi mkuu huyo amefafanua kuwa, MSD imeendelea kufanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi vituo vinavyotoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini kama mashine za kusafisha damu (dialysis machine), MRI, CT- Scan, Ultrasound, Digital X-Ray na vitendanishi vyake.
Ameongeza kuwa uwepo wa vifaa hivyo unawezesha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi na kutolewa kwa tiba sahihi wakati mafanikio mengine ni kuongeza mizunguko ya usambazaji wa bidhaa za afya kuhakikisha zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma.
Aidha, amesema kupatikana kwa mtaji wa uendeshaji kiasi cha Sh. bilioni 100 kwa mwaka wa fedha 2023/24 zilizotolewa na serikali kuiwezesha MSD kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na kukabiliana na changamoto za mnyororo wa ugavi.
“Fedha hizi zimesaidia MSD kuwa na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya vituo kwa wakati na kutengeneza mikakati itakayofanya taasisi inunue kwa tija na kuimarisha mahusiano na wazabuni mbalimbali. Mafanikio mengine ni kuimarika kwa makusanyo ya fedha kutoka vituo vya kutolea huduma za afya.
“Maboresho yanayoendelea yamewezesha vituo vya kutolea huduma za afya kuwa na imani na utendaji wa MSD ambapo makusanyo ya fedha yatokayo kwenye vyanzo mbalimbali vya vituo vya kutolea huduma za afya na kuletwa MSD yameongezeka kutoka Sh. bilioni 40.3 mwaka 2022/23 na kufikia Sh. bilioni 118.9 kwa mwaka 2023/24,” amesema.
Akieleza zaidi Tukai amesema kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali, mapato ya Bohari ya Dawa yameendelea kuongezeka kutoka Sh. bilioni 359.6 kwa mwaka 2022/23, hadi zaidi ya Sh. bilioni 510.07 mwaka wa fedha 2023/24 likiwa ongezeko la Sh. bilioni 150.43 ambayo ni sawa na asilimia 42.
Kuhusu utekelezaji wa Sera ya Viwanda, amesema katika kutekeleza sera ya uanzishwaji wa viwanda, Bohari ya Dawa imechukua hatua mbalimbali ukiwemo uanzishaji wa Kampuni Tanzu na kuongeza ufanisi wa usimamizi na uendeshaji wa shughuli za uzalishaji, MSD imeanzisha kampuni tanzu inayoitwa “MSD Medipharm Manufacturing Company Limited”.
“Pamoja na hivyo Juni 2024, MSD imezindua Bodi ya Usimamizi wa Kampuni Tanzu hiyo ambayo itakuwa na jukumu la usimamizi wa shughuli za uzalishaji wa bidhaa za afya. Hivyo, Kampuni hii itakuwa na uwezo wa kuingia ubia na wawekezaji wengine,” amesema.
Mbali na hilo, katika kufanikisha azma ya kushirikisha sekta binafsi, Bohari ya Dawa imetambua maeneo yanayohitaji ushirikiano na sekta binafsi na inafanya uchambuzi ili wawekezaji wenye sifa washiriki uanzishaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya.