Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dodoma

BOHARI ya Dawa (MSD), imedhamiria kuongeza uwezo wa kuhifadhi dawa kwa kujenga maghala na kuangalia maeneo ambayo yatapunguza gharama za usambazaji pamoja na kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayohusu usimamizi wa maghala na ushiriki kwenye kutengeneza mifumo ya NesT.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dodoma waliokuwa kwenye ziara ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MSD katika Kanda ya Iringa na Kanda ya Dodoma.;

Mavere aliweka wazi mikakati mbalimbali iliyojiwekea MSD ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya na kuweza kujiendesha kibiashara.

“MSD imejiwekea mikakati mbalimbali itakayochangia kuongezeka kwa mapato na kuboresha ujtendajikazi” alisema.

Alisema kuwa baada ya kuongezewa mtaji na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwanza, Bohari ya Dawa itafanya ununuzi wenye tija kutoka kwa wazalishaji na hivyo kuongeza upatikanaji wa bidhaa za afya.

Alisema kuwa mkakati wa tatu, alisema kupitia Kampuni Tanzu, Bohari ya Dawa itaendelea na jitihada za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Mavere alisema mkakati wa tatu ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye Bima ya Afya ya Taifa na kuweza kutambua wahitaji zaidi wa bidhaa hizo nje ya MSD.

Kwa mujibu wa Tukai mkakati wa nne ni kutekeleza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa za afya katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Ruvuma, Arusha na Geita.

Aidha, alisema MSD itaongeza uwezo wa kuhifadhi kwa kujenga maghala na kuangalia maeneo ambayo yatapunguza gharama za usambazaji, kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayohusu usimamizi wa maghala na ushiriki kwenye kutengeneza mifumo ya NesT.

“Kupitia mifumo inayohusu gharama za uendeshaji (logistiki) kwa kuongeza usimamizi kupitia Idara maalum ya uendeshaji,” alisema Tukai.

Hatua nyingine ni pamoja na kuimarisha mifumo ya Utawala kufanya maboresho ya muundo ili kuendana na utendaji na kufanya tafiti na kushirikiana na taasisi mbalimbali kuboresha uendeshaji wa taasisi zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu kuimarisha kitengo cha ndani cha usimamizi wa utendaji.

Please follow and like us:
Pin Share