Na Mwandishi Maalum
Bohari ya Dawa nchini (MSD) imeendelea kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 – 2020 kwa vitendo baada ya kujipanga kushiriki kwenye kujenga viwanda vya kuzalisha dawa nchini kwa nia ya kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi ambao kwa sasa ni asilimia 85.
Mpango huu unalenga kupunguza gharama za ununuzi wa dawa na kurahisisha upatikanaji wa dawa kote nchini, hali itakayolisaidia taifa kuwa na wananchi wenye afya nzuri na hivyo kuimarisha nguvu kazi ya taifa la Tanzania.
Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Rugambwa Bwanakunu, amesema mchakato wa kununua dawa nje ya nchi pamoja na kuupunguza kutoka miezi 9 hadi wastani wa kati ya miezi 6 na 4 kulingana na aina kifaatiba kinachonunuliwa, bado anaona muda huu ni mrefu na unaligharimu taifa fedha nyingi kitu ambacho hakikubaliki.
Bwanakunu amesema ni aibu nchi hii kuendelea kuagiza maji nje ya nchi na vifaatiba vingine visivyokuwa na ugumu wowote kutengengezwa hapa nchini. “Mfano tunaagiza pamba China. Bidhaa za pamba katika hospitali zetu tunatumia product zaidi ya 100 zinazohitajika. Sisi nchi yetu inazalisha pamba, bado tunaiuza nje na kisha tunanunua pamba iliyosindikwa kutoka huko. Hii haikubaliki.
“Kwa mwezi tunaagiza na kunaleta makontena karibu 50 ya maji na kontena 20 za pamba. Tanzania kuna viwanda 13 vya dawa kwa sasa. Ukiangalia viwanda vilivyo na mikataba na MSD na vyenye uwezo ni vitano tu. Miaka zaidi ya 50 nchi yetu bado ina viwanda vichache kiasi hiki, haikubaliki.
“Sasa tunatekeleza kwa vitendo sera na sheria ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, yaani Public Private Partnership (PPP) kuwezesha ujenzi wa viwanda. MSD inahudumia zaidi ya hospitali na vituo vya afya 7, 309, nchini. Mtu akijenga kiwanda cha dawa hapa nchini afahamu kuwa soko lipo kwa hospitali za ndani na nje. Tayari tumepata ekari 100 za ardhi pale Kibaha na kupitia PPP tutajenga viwanda,” amesema.
Amesema zaidi ya huo mpango wa PPP, MSD kwa kushirikiana na taasisi rafiki 8 yaani toka Wizara ya Afya ni NHIF, TFDA na MSD, Ofisi ya Waziri Mkuu ni Workers Compensation Fund (WCF), Wizara ya Viwanda na Biashara ni TIRDO, TEMDO, NDC na TBS na Wizara ya Fedha kuna benki ya TIB Corporate na TIB Development na Mkuu wa Mkoa Simiyu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati. MSD kwa kushirikiana na wadau hawa itajenga viwanda vya vifaatiba mkoani Simiyu.
Mkoa wa Simiyu umeunda Kamati ya Viwanda vya Dawa inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, chini ya usimamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa sasa upembuzi yakinifu umeishafanyika, na tuko kwenye gharama za mradi. Mradi huu utazalishaji maji ya drip (Intravenous Fluid, cotton wool, gauze absorbent and diapers) ambavyo ni vifaa vya hospital vitokanavyo na pamba ambayo tunayo nyingi.
“Soko ni kubwa hata tukiwa na viwanda 10 vya maji ya drip bado wote watapata soko, soko ni kubwa sana. Wafanyabiasjhara wengi wameonyesha nia na sisi kazi yetu ni kuwapa taarifa za mahitaji ili waweze kujua ukubwa wa soko,” amesema Bwanakunu.
Bwanakunu amesema nchi kama DRC, Malawi na Zambia nazo zinaagiza dawa kutoka nje ya nchi ambazo zote zinapitia Tanzania kwa kujenga viwanda vyenye ubora unaotakiwa nchi hizo ni soko ambalo liko tayari. Pia nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC) zimeiteua MSD kuwa mnunuzi wa dawa kwa ajili ya nchi hizo kutokana na kuwa na mfumo bora za ununuzi, uhifadhi na usambazaji dawa, hivyo hili nalo ni soko.
“MSD ina mtandao mzuri wa kununua na kusambazaji dawa hadi vijijini. Nchi nyingine unakuta mnunuzi wa dawa, anayehifadhi na msambazaji ni watu watatu tofauti. Sisi tumepata magari 181 na kwa sababu tunasubiri uzinduzi kwa sasa sitayazungumzia sana. Lakini nikuhakikishie MSD inatekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo kabisa,” amesema.
MSD imekuwa taasisi ya pili nchini katika Sekta ya Afya kupata ithibati hii ya ISO 9001:2015 baada ya TFDP. Taasisi inayopata ithibati ya ubora ya ISO 9001, ambayo ilianza kutolewa mwaka 2008 na sasa imeboreshwa kuwa ya 2015, inapaswa kuwa imedhihirisha ubora katika maeneo saba kama ifuatavyo:-
1. Mtazamo chanya kwa wateja – inaboresha kiwango cha wateja kuridhika na kukaa nao bila kuwapoteza.
2. Uongozi – kuainisha bayana majukumu na wajibu wa viongozi.
3. Kushirikisha watu – kuimarisha mawasiliano ya ndani ya taasisi.
4. Mkondo wa mchakato – kuongeza ubora na kupunguza uharibifu kila wakati.
5. Uboreshaji – kuhakikisha utendaji wa taasisi yako unakua kupitia maboresho.
6. Uamuzi unaotegemea ushahidi – kutambua na kutekeleza matakwa ya wateja na waajiriwa.
7. Kuuishi uhusiano – kuifanya taasisi yako kuvutia watu kufanya nayo kazi.
Kwa kufuata vyema vigezo hivi vilivyotajwa hapo juu, taasisi husika inaongeza ufanisi, mtandao mpana na faida. MSD imeendelea kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa katika mfumo wa ununuzi, utunzaji na usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara (Supply Chain Management), hivyo imepata Ithibati ya Kimataifa ya Ubora ya Daraja la Juu inayojulikana kama ISO 9001:2015 ambayo itadumu kwa miaka mitatu (2017 – 2020).
MSD imepata ithibati hii baada ya ukaguzi wa ubora wa huduma zinazotolewa na MSD uliofanywa na kampuni ya Kimataifa ya ACM LIMITED ya nchini Uingereza, mwezi Agosti 2017, na kudhihirisha kuwa huduma inazotoa MSD na bidhaa inazosambaza inafuata miongozo ya kimataifa na matakwa ya mamlaka za udhibiti nchini katika utoaji wa huduma za mnyororo wa ugavi.
Tayari MSD imeanza mchakato wa kujenga bohari katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba na Songea kwa kupata ardhi na sasa inaendelea na mchakato wa zabuni ya ujenzi wa bohari hizo zitakazokamilika kwa kiwango kikubwa katika mwaka huu wa fedha.