*Yaingia mikataba ya mabilioni ya fedha bila kufuata taratibu, Mkurugenzi atumbuliwa
* Yalipa watumishi watatu posho ya kujikimu ya Sh milioni 215.99 kwenda China kununua mashine
*Yailipa kampuni hewa ya Misri mabilioni ya fedha, wapotea bila kuleta dawa nchini
*Yadaiwa kununua dawa Kariakoo zilizokosa ithibati za TMDA, mikataba mingi ina utata
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Mwenendo wa utendaji kazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ni ‘kimeo’ baada ya ripoti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kubaini dosari chungu nzima.
Kutokana na dosari hizo, Rais Samia Suluhu Hassan, imeifumua MSD akateua Bodi na Mkurugenzi Mkuu mpya mwishoni mwa wiki. Amemteua Rosemary William Slaa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bohari ya Dawa (MSD). Slaa ni Ofisa Mwandamizi katika Kampuni ya PricewaterhouseCooper (PWC).
Rais Samia amemteua Mavere Ali Tukai kuwa Mtendaji Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD). Tukai hadi anateuliwa alikuwa Kiongozi Mkuu wa Mradi wa USAID Global Health Supply Chain Technical Assistance. Mkurugenzi Mkuu wa MSD aliyetenguliwa ni Meja Jenerali Gabriel Mhidze.
Wakati huo huo, Rais Samia amemteua Raymond William Mndolwa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
Machi 30, 2022 akipokea ripoti ya CAG inayoishia Juni, 2021, Rais Samia, amesema MSD ilifikia hatua ya kupata zabuni ya kuuza dawa zake katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), lakini sasa hivi hata watu wa ndani wanailalamikia.
“Kwa kweli MSD inahitaji general overhauling kama tulivyofanya Tanesco. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga, nikuagize kwa haraka tukafanye general overhauling ya MSD kuanzia uongozi wa juu, ununuzi na vitengo vyote ili sasa twende vizuri,” amesema Rais Samia.
Taarifa za ndani
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kilichozungumza na Gazeti la JAMHURI kwa nyakati tofauti kimedai licha ya ripoti ya CAG kuanika uozo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Meja Jenerali Dk. Gabriel Mhidze, alikuwa anakabiliwa na changamoto kubwa za kiutendaji.
Chanzo hicho ambacho jina lake linahifadhiwa kimedai kwa sasa MSD ni kama sikio la kufa, kwa sababu ina ukosefu mkubwa wa dawa licha ya serikali kutoa karibu Sh bilioni 80 za kuzinunua tangu Aprili, 2021.
Kimedai kuwa ukosefu huo unatokana na Dk. Mhidze kununua dawa za mwezi hadi mwezi na hali hiyo inachukua wiki sita kufika. Pia ananunua kwa ‘washitiri’ wa Kariakoo, jijini Dar es Salaam kinyume kabisa cha alivyokuwa anafanya mtangulizi wake, Laurean Rugambwa Bwanakunu, aliyekuwa ananunua moja kwa moja kutoka viwandani nje ya nchi.
“Hao washitiri wanaagiza dawa nje ya nchi kisha hafuati taratibu za ununuzi. Kwa sasa MSD hakuna Bodi ya Zabuni jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya PPRA,” kimedai chanzo chetu na kuongeza:
“Hanunui kutoka viwanda vya ndani na vya kimataifa vyenye ithibati ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Dawa nyingi ananunua Kariakoo kama bidhaa nyingine.
“Hii si tu inaongeza gharama za dawa na vifaa tiba, lakini changamoto kubwa pia ni ubora wa dawa na vifaa tiba pindi vinaponunuliwa.”
Pia chanzo hicho kimedai kuwa kitendo hicho ndani ya MSD kimesababisha ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwenye halmashauri na mikoa nchini, kwa sababu upatikanaji wake ni karibu asilimia 25.
“Hivi sasa kuna shida kubwa sana ya surgical gloves. Kwa mfano wiki mbili zilizopita Manispaa ya Kahama walilipia katoni 50 za surgical gloves kisha wakaletewa mbili, tena baada ya wiki mbili kupita.
“DG hazingatii taratibu za ununuzi. Yeye ameanzisha mfumo wa kununua dawa kwa pre-qualified suppliers kupitia Google na Ali Baba na anawalipa asilimia 100. Hii ina shida nyingi sana, maana hakuna ushindani wa kimataifa. Pia suala la ubora wa dawa halizingatiwi,” kimedai chanzo hicho.
Vilevile kimedai kuwa Dk. Mhidze ananunua dawa na vifaa tiba kinyume cha Sheria za Ununuzi wa Umma. “Manunuzi kwa quotation by PPRA hayatakiwi kuzidi Sh milioni 120, ila yeye ananunua zaidi ya Sh milioni 120 kwa quotation tena Kariakoo,” kimedai na kuongeza:
“Maana yake ni kuwa hakuna ulinganifu wa bei (comparative bid analysis) na ni mwanya wa vijana wa procurement kupata rushwa, kwa kuwa wanaona quotes za wote kabla ya uamuzi.”
Pia kimedai kuwa amenunua mashine za maabara kinyume cha viwango vilivyowekwa awali na Wizara ya Afya na MSD katika zabuni namba 14.
“Kasababisha hasara kwa kuleta mashine mpya za maabara nje ya viwango. Kwa hiyo ile costly exercise iliyofanywa na Wizara ya Afya ya kutokuwa na mashine, wenye mashine kutokufanya matengenezo, yeye akaileta na kuamua kununua nyingine bila kuzingatia utaratibu na ubora, imeleta hasara kubwa,” kimesema chanzo chetu kingine.
Mbali na hayo, pia chanzo hiki kimesema kuwa Dk. Mhidze ameweka wataalamu wasio na weledi baada ya kuwahamisha wenye weledi pale MSD kwa kuanzia utawala hadi wafagizi.
“Inaweza kuwa ni sawa kubadili menejimenti, lakini hata maofisa wa kawaida kawahamishia ofisi nyingine za serikali waliokuwa na ufahamu na weledi wa mifumo ya MSD na kuweka watu wasio na utaalamu wa ununuzi. Kwa nini kawaweka watumishi wasiojua kitu na kwa nini Utumishi walimruhusu? Hakuna anayejua,” kimedai chanzo hicho.
Kuhusu bei ya dawa zinazotengenezwa katika Kiwanda cha Dawa cha Keko, chanzo kingine kimedai kuwa inapangwa bila kuangalia gharama za uendeshaji.
“MSD sasa inaharibika na kwa jinsi alivyoiharibu itahitaji kati ya miaka miwili hadi mitatu kutengamaa, kwa sababu ameharibu mifumo; mnyororo wa ugavi, procuremenent systems na wafanyakazi wenye uzoefu wameondolewa na si rahisi kuwapata wanaojua hiyo mifumo.
“Mkurugenzi Mkuu ana wasaidizi sita na magari mawili na kila anaposafiri huwa anasafiri kwa gari anakwenda nao, lakini watumishi wanalazimishwa kupanda mabasi. Kwa ufupi ana uhusiano mbaya na wafanyakazi karibu wote.”
Wamehoji, iweje viwanda vya MSD vijengwe Makambako wakati MSD ina kiwanja kwa ajili hiyo walichouziwa na Manispaa ya Kibaha?
“Huo ujenzi haujafuata taratibu za ununuzi. Panahitajika real time audit kujua hasara iliyopata serikali kabla haijawa kubwa,” kimedai chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, kimedai kuwa Oktoba 12, 2021 Dk. Mhidze aliidhinisha malipo ya dola milioni 1.505 za Marekani kwa Kampuni ya ACME Trade Int-Al Handasiya Medical Supplies ya Misri, lakini kampuni hiyo haikuleta dawa hapa nchini kama makubaliano yanavyosema.
“Hiyo kampuni ya Misri ni ya kitapeli na licha ya DG kuidhinisha hizo fedha, hakuna dawa walizosambaza hapa nchini,” kimedai chanzo chetu na kuongeza:
“Na baada ya kugundua kuna utapeli umefanyika, kuna watumishi wa MSD wakatumwa kwenda Misri kuitafuta na walipofika katika mitaa ya Cairo na Alexandria wakawa wanazurura mitaani kuwauliza watu ilipo hiyo kampuni na wakaikosa.”
Utata mwingine unaonyesha kuwa Oktoba 12, 2021 siku ambayo MSD walisaini mkataba Na. IE-009/2021/2022/HQ/G/50 wa dola 3,120,338.02 (Sh bilioni 7.2) kwa ajili ya kampuni hiyo ya Misri kutoa huduma ya dawa, siku hiyo hiyo mzabuni aliyepatikana kwa kufika ofisini tu, alilipwa dola 1,505,354.68 (Sh bilioni 3.46).
“Sasa tazama maajabu. Mtu huyo huyo aliyesaini mkataba, mkataba wenyewe unaonyesha ulisainiwa Oktoba 12, 2021, ila umegongwa muhuri kuwa umepokewa katika ofisi za MSD Novemba 2, 2021, kuna kila dalili kuwa alilipwa kabla ya mkataba kusainiwa. Amewatapeli, nasikia amekuja mtu mwingine akawaambia yeye atawapatia dawa walizotapeliwa lakini wamhakikishie zabuni ya miaka mitatu ijayo… mambo ya ajabu kabisa.”
Dk. Mhidze ashindwa kujibu maswali
Aprili 8, 2022 Gazeti la JAMHURI lilimtafuta Dk. Mhidze ajibu hoja za madai yote yanayodaiwa kukwamisha utendaji wake ndani ya MSD, lakini hakupokea simu ila baadaye usiku alimpigia mwandishi wa habari hizi na kusema mchana kutwa alikuwa ametingwa na majukumu ya kazi.
“Mchana nilikuwa na kazi na nilikuwa busy kuwaona watu wengine. Sasa sijui unataka maswali yako nikujibu lini, kwa sababu Jumapili Aprili 10, 2022 nafikiri nitaondoka kwenda Dodoma. Utahitaji nikujibu lini sasa? Kama kesho Jumamosi (Aprili 9, 2022) itawezekana.
“Kwa sababu kuna watu fulani hivi nakutana nao mahali fulani, baada ya hapo kuanzia saa nane mchana nitakuwa free na tunaweza kuonana maeneo ya Lugalo au JKT – Dar es Salaam na nitakutaarifu tuonane sehemu moja kati ya hizo,” amesema Dk. Mhidze kabla ya kutenguliwa uteuzi wake.
Hata hivyo, kesho yake Aprili 9, 2022 ilipowadia muda wa saa nne asubuhi akatuma ujumbe mfupi wa maneno kwa mwandishi wa habari hizi kwamba mambo yake yameingiliana na miadi ya kuonana haitakuwapo.
“Habari za asubuhi, niwie radhi kuna mambo yamepandana, hivyo miadi yetu ya leo mchana haitawezekana, nimeona nikutaarifu mapema ili muda huo usiupoteze. Asante kwa kunielewa,” amesema Dk. Mhidze.
Baada ya kutumiwa ujumbe huo, papo hapo mwandishi naye akamtumia maswali 14 akitaka ufafanuzi wa madai mbalimbali yaliyotolewa kuhusu utendaji wake MSD, ila hadi tunakwenda mitamboni kuchapisha toleo hili la Gazeti la JAMHURI hakujibu meseji hizo, wala hakupokea simu alipopigiwa, lakini pia alikuwa amekwisha kutenguliwa.
CAG abaini dosari
Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 iliyowasilishwa bungeni Jumanne ya wiki iliyopita, imesema kuna ofisa masuuli wa MSD aliyeingilia majukumu ya Bodi ya Zabuni kwa kuidhinisha mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 2.79.
“Kifungu cha 41 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 kinawataka maofisa masuuli, bodi ya zabuni, vitengo vya usimamizi wa ununuzi, idara za watumiaji na kamati za tathmini kufanya kazi kwa uhuru kuhusiana na kazi na majukumu yao,” amesema CAG na kuongeza:
“Aidha, kifungu cha 33 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 kinaainisha majukumu ya bodi za zabuni kuwa ni kujadili mapendekezo ya kitengo cha usimamizi wa ununuzi na kuidhinisha utoaji wa mikataba na kuidhinisha zabuni.
“Pia kuidhinisha nyaraka za mikataba, ununuzi na uuzaji wa mali kwa taratibu za zabuni, na kuhakikisha utendaji mzuri katika ununuzi na uuzaji wa mali kwa zabuni unafuatwa kikamilifu na taasisi za ununuzi.”
CAG amesema wakati wa kupitia mchakato wa ununuzi na utoaji wa mikataba MSD, akabaini kuwa ofisa masuuli aliingilia majukumu ya Bodi ya Zabuni huku taratibu zote za utoaji wa zabuni aliidhinisha peke yake bila kuishirikisha bodi hiyo kwa mikataba yenye thamani ya dola milioni 1.06 za Marekani, kinyume cha sheria zilizotajwa.
Amesema hali hiyo ilisababishwa na upungufu wa idadi ya wajumbe wa bodi hiyo na hivyo kutokidhi akidi inayotakiwa.
Pia amesema kitendo cha kukiuka udhibiti uliowekwa kinaweza kuhatarisha utendaji mzuri wa mchakato wa ununuzi katika taasisi zinazonunua na inaweza kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Ameitaja mikataba iliyoidhinishwa moja kwa moja na ofisa masuuli kuwa ni wenye namba IE-009/2020/2021/HQ/G/127 huku mzabuni akiwa ni Kampuni ya Wenzhou Liangke Machinery Co. Ltd kwa ajili ya ununuzi wa capsule dosage form production line kwa dola milioni 668.86 za Marekani.
Mwingine una namba IE-009/2020/2020/HQ/G/126 na mzabuni akiwa ni Kampuni ya Shanghai Sheng-Guan Machinery Equipment Co. Ltd kwa ajili ya ununuzi wa oral liquid and syrup manufacturing and filling production line kwa dola milioni 222.50 za Marekani.
Mkataba mwingine una namba IE-009/2020/2020/HQ/G/126 na mzabuni akiwa ni Kampuni ya Guangdong Jinzong Machinery Co. Ltd kwa ajili ya ununuzi wa oral liquid and syrup manufacturing and filling production line kwa dola milioni 163.80 za Marekani.
Pia amesema alibaini barua yenye Kumb. Na. CEA.169/178/03/18 ya Oktoba 13, 2020 ya uteuzi wa maofisa watatu kwenda China kwa ajili ya kutafuta watengenezaji wa mashine 71 za kusafisha damu (hemodialysis) na kuzisambaza na kutoa ushauri kwa serikali kwa ajili ya kuzinunua.
Hata hivyo, amesema utaratibu wa kutafuta watengenezaji na utoaji wa mikataba (namba ya mkataba au kumbukumbu) haukuhusisha Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi na Bodi ya Zabuni bali mchakato mzima wa kuzinunua ulifanywa na watu watatu wakiwa China kwa gharama ya Sh bilioni 2.79.
Pia amesema alibaini kuwa ili kuwezesha ununuzi wa mashine hizo, MSD ilitumia jumla ya Sh milioni 215.99 kuwalipa watumishi watatu posho ya kujikimu kwa siku 61 pamoja na gharama za usafiri kwenda China kwa madhumuni ya mazungumzo na kutafuta viwanda.
“Nina shaka na mchakato mzima wa ununuzi na matumizi ya fedha za umma. Napendekeza MSD ihakikishe mgawanyo wa majukumu unafuatwa ili udhibiti uliowekwa katika Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake unatekelezwa na kila chombo kifanye kazi kwa kujitegemea ili kuwa na taratibu nzuri za ununuzi na uuzaji wa mali kwa njia ya zabuni,” amesema.
Ununuzi bila mikataba
CAG amesema MSD ilifanya ununuzi bila mikataba, wenye thamani ya Sh bilioni 9.90 na dola milioni 1.42 za Marekani.
“Kanuni ya 233(1) (2) na Kanuni ya 75 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 (kama zilivyorekebishwa mwaka 2016) zinazitaka taasisi zinazonunua na watu ambao zabuni zao zimekubaliwa kuingia mikataba rasmi ndani ya siku 14 za kazi,” amesema na kuongeza:
“Baada ya kukamilisha masharti yote kabla ya kusainiwa kwa mikataba na mikataba rasmi kuwa katika fomu maalumu iliyowekwa na kuwa na masharti na matakwa yaliyowekwa kwenye nyaraka za zabuni.
“Nilipitia ununuzi wa bidhaa 30 uliopangwa chini ya zabuni namba IE 009/2020/2021/HQ/G/160 ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba MSD na kubaini kuwa ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 9.90 na dola milioni 1.42 za Marekani ulifanywa bila kusaini mikataba kinyume cha kanuni iliyotajwa hapo juu.”
CAG amesema badala yake menejimenti ilitumia barua ya dharura iliyosainiwa kuagizwa na ofisa masuuli na kufanya malipo kamili ya bidhaa kabla ya kupokewa kwa bidhaa kwa sababu ununuzi ulikuwa wa dharura.
Vilevile amesema hakukuwa na ushindani wa zabuni uliofanywa kama inavyotakiwa na taratibu za ununuzi.
Amesema menejimenti nayo haikuzingatia udhibiti wa vihatarishi kwa sababu haikutoa matakwa au masharti yoyote kama vile vifungu vya kutoza fidia kwa kushindwa kutekeleza mkataba iwapo bidhaa au huduma itachelewa kuwasilishwa au kutowasilishwa.
Mikataba kusainiwa bila kupitiwa na AG
Katika hatua nyingine, CAG, amesema mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 17.14 ilitolewa na kusainiwa bila kupekuliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
“Wakati Kanuni ya 59 (1)(2) na Kanuni ya 2 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013 (kama zilivyorekebishwa mwaka 2016) zinaeleza kuwa mkataba wowote rasmi unaotokana na kukubalika kwa zabuni yenye thamani ya Sh bilioni moja au zaidi na kwa ununuzi unaofanywa kupitia zabuni ya ushindani wa kimataifa utapekuliwa na AG kabla ya mkataba husika kusainiwa na wahusika na zabuni ambayo mkataba wake haujapekuliwa na AG itakuwa batili.
“Lakini wakati ninakagua nilibaini kuwa mikataba sita yenye thamani ya dola milioni 7.46 za Marekani sawa na Sh bilioni 17.14 ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika MSD iliingiwa na wazabuni bila kupekuliwa na AG kinyume cha kanuni iliyotajwa hapo juu.”
CAG amependekeza kuwa katika siku zijazo mashirika ya umma yahakikishe mikataba inapekuliwa na AG na ushauri anaoutoa unazingatiwa ili kuepusha migogoro ya kisheria itakayojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi.
Katika hatua nyingine, CAG anaitaja MSD kuwa ni moja kati ya shirika la umma lililofanya ununuzi wa Sh milioni 43,984.55 katika mikataba sita nje ya bajeti na mipango hiyo haikujumuishwa katika mpango wa ununuzi wa mwaka kama inavyotakiwa na Kanuni ya 69 (3) na (7) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 (kama zilivyorekebishwa) na Kanuni ya 26 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma (kama zilivyorekebishwa) za mwaka 2016.
Amesema mwenendo wa ununuzi uliofanywa nje ya mpango wa mwaka ulioidhinishwa unaongezeka kwa sababu katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 ameripoti taasisi moja, ila katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 kuna ongezeko la taasisi tatu.
Amesema MSD imeanzisha kiwanda chake cha kutengeneza glovu bila kufanya upembuzi yakinifu wa biashara.
“Nilipitia muhtasari wa Mkutano wa 157 wa Bodi ya Wadhamini ya MSD na kubaini kuwa bodi iliibua wasiwasi juu ya upembuzi yakinifu wa mapendekezo ya Kiwanda cha Idofi cha uzalishaji wa glovu na kuagiza maelezo yatolewe kwa uwazi na uwezo wao katika fedha, utaalamu, teknolojia na kuonyesha chanzo cha asilimia 10 ya malighafi kwa ajili ya uzalishaji kutoka vyanzo vya ndani.
“Licha ya wasiwasi wa bodi, sikupewa upembuzi yakinifu uliorekebishwa na uliozingatia hoja zilizotolewa na bodi. Nina shaka kuwa bila upembuzi yakinifu wa kina utendaji wa kiwanda hicho hautafikiwa kama ilivyopangwa,” amesema.
CAG amesema alibaini kuwa ripoti ya upembuzi yakinifu ya MSD ya Septemba, 2020 juu ya kuanzishwa kwa eneo la viwanda la Idofi haikujumuisha mchanganuo wa biashara pamoja na mpango wa kina ulioandaliwa ili kupata hoja za kuanzisha mradi na kutathmini faida, gharama na vihatarishi vya biashara.
“Kwa mtazamo wangu, kukosa hoja za kibiashara na mpango wa kina wa mradi, MSD inaweza kukosa uhalali wa kutosha wa kuanzisha mradi huo, jambo linaloweza kusababisha lengo lililokusudiwa la mradi kutofikiwa,” amesema.
Vilevile amesema MSD haikuzingatia suala muhimu la umbali kutoka bandarini hadi kiwandani (takriban kilomita 565 kutoka Bandari ya Dar es Salaam), upatikanaji wa malighafi ambayo bado haijatambuliwa na menejimenti na chanzo cha nishati ikiwa ni pamoja na umeme na upatikanaji wa gesi asilia inayoweza kusababisha bei ya mwisho ya bidhaa kuwa juu kutokana na ongezeko kubwa la gharama ya uzalishaji.
Mbali na hayo, amesema alibaini kuwa MSD inamiliki ardhi yenye ukubwa wa takriban ekari 100 katika Manispaa ya Kibaha ambayo ingeweza kutumika kwa mradi huu (kama mchanganuo sahihi wa biashara ungefanyika) badala ya Idofi ili kupunguza umbali wa usafiri na kuwa mahali ambako upatikanaji wa huduma za umeme na gesi asilia zinapatikana kwa urahisi.
Amesema alibaini kuwa MSD haikupanga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Idofi katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Pia amesema alibaini kuwa hadi Septemba 30, 2020, Sh bilioni 9 zilitumiwa na MSD kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, ikiwa ni sehemu ya Sh bilioni 16.32 kutoka serikalini zilizotolewa kwa ajili ya kulipa madeni ya awali ya wazabuni wake na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Amesema hadi Septemba 30, 2021 hapakuwa na idhini ya Mlipaji Mkuu wa Serikali juu ya mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo zilizopokewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Malipo ya Sh bilioni 15 bila mkataba
CAG amesema MSD ilifanya malipo ya awali ya Sh bilioni 15 kwa mzabuni bila mkataba na ushahidi wa bidhaa kupokewa.
“Wakati kifungu cha 164 cha Kanuni za Fedha za MSD za mwaka 2011 kinasema kuwa malipo ya awali kwa wazabuni yatafanywa tu kwa mujibu wa masharti ya mkataba kama upo au kulingana na utaratibu wa kibiashara unaokubalika kwa ujumla,” amesema.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021, amesema MSD ilifanya malipo ya awali ya Sh bilioni 14.89 kwa wazabuni watano (Keko Pharmaceutical Industry, Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini, Nakuroi Investment Company Ltd, Technical Services and General na Wide Spectru (T) Ltd bila mikataba yoyote au makubaliano mengine yanayobainisha msingi wa malipo ya awali.
Amesema alibaini kuwa kuanzia Julai Mosi, 2021 hadi wakati wa ukaguzi huu Septemba, 2021, salio la malipo ya awali lilipunguzwa kwa Sh bilioni 8.03 na hakuna ushahidi wa utoaji wa huduma au bidhaa uliopatikana ili kuhalalisha kupunguzwa kwa malipo ya awali.
Pia amebaini kuwa vocha za malipo ya awali ziligongwa muhuri wa ‘imelipwa’ kabla ya tarehe ya kuidhinishwa na malipo mengine yaliwekwa muhuri wa kulipwa baada ya mwaka kupita.
Amesema hali hiyo inatokana na ukosefu wa udhibiti wa ndani ili kuwezesha mikopo nafuu kwa wazabuni.
CAG amesema malipo ya awali kwa wazabuni bila mikataba na ushahidi wa utoaji wa bidhaa au huduma kunaweza kuashiria uwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wasambazaji.
“Napendekeza MSD wachunguze sababu za bidhaa zilizolipiwa kutowasilishwa hadi Juni 30, 2021 licha ya kuagizwa kwa sababu ya mahitaji ya dharura, wafuatilie wazabuni waliolipwa ili kuhakikisha bidhaa au huduma zilizolipiwa zinawasilishwa au marejesho yanafanywa na ihakikishe katika siku zijazo hakuna malipo ya awali yanafanywa kwa wazabuni bila mikataba,” amesema.
Pia amesema hadi kufikia Juni 30, 2021, MSD ilikuwa inadaiwa Sh bilioni 176.31 na kati ya deni hilo, Sh bilioni 163.97 (asilimia 93) zilikuwa hazijalipwa kwa zaidi ya miezi 12.
Amesema madeni hayo yalitokana na hali ya ukwasi usioridhisha ili kukidhi majukumu ya kifedha yanapohitajika kulipwa na kushindwa kuwalipa wadai kwa wakati, jambo linaloweza kuathiri sifa nzuri ya taasisi na uwezo wao wa kukopesheka.
Kushindwa kufikia malengo
Katika hatua nyingine, amesema MSD ilishindwa kwa asilimia 66 kutimiza mahitaji ya bidhaa za dawa na vifaa tiba kwa wateja wake kwa mujibu wa Mpango wake wa Biashara wa mwaka 2021.
Amesema MSD ilipaswa kuimarisha utimizaji wa mahitaji ya dawa na vifaa tiba kwa wateja hadi kufikia asilimia 75 ya bidhaa zilizoagizwa kufikia Juni, 2021.
Hata hivyo, amesema hadi Juni 30, 2021, MSD ilitimiza asilimia 34 tu ya jumla ya bidhaa 43,180,884 za dawa na vifaa tiba zilizoagizwa na wateja na kuacha asilimia 66 ikiwa haijatimizwa.
Amesema japo kuna uboreshaji katika utimizaji wa mahitaji ya bidhaa zilizoagizwa na wateja kutoka asilimia 0.6 iliyoripotiwa katika ripoti yake ya mwaka uliopita wa fedha wa 2019/2020 hadi asilimia 34 mwaka wa fedha wa 2020/2021 bado MSD inahitaji kujitahidi zaidi ili kufikia lengo la asilimia 75 ililojiwekea.
Dawa zilizokwisha muda wake
CAG amesema kuna dawa zenye thamani ya Sh bilioni 22.80 zilizokwisha muda wake katika maghala ya MSD ambazo ni jumla ya bidhaa 7,676,436 baada ya kuhifadhiwa kuanzia Aprili 16, 2000 hadi Juni 30, 2021.
Amesema kiwango cha kwisha kwa muda wa dawa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kilikuwa asilimia tano ya gharama za mauzo ya Sh bilioni 196.83 sawasawa na kiwango kilichoripotiwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 cha asilimia tano.
Amesema kiwango hiki kimezidi kiwango kinachotakiwa kwa asilimia mbili kama kilivyoelezwa katika Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za MSD wa Juni, 2018.
Vilevile amebaini MSD ilipokea fedha kutoka kwa wafadhili kiasi cha dola 239,023.92 za Marekani kama gharama za kuziharibu dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV’s).
Licha ya ruhusa ya kuteketeza dawa hizo kutolewa na Wizara ya Fedha na Mipango tangu Oktoba 7, 2021, amesema dawa hizo hazikuharibiwa hadi wakati wa ukaguzi Desemba, 2021.
Katika hatua nyingine, amesema MSD ni moja ya shirika la umma lililofanya ununuzi wa bidhaa na huduma katika mikataba 23 kwa Sh milioni 8,548.93 nje ya Mfumo wa Ununuzi wa Kielektroniki wa TANePS unaotumika kuwasilisha kwa mtandao mipango ya ununuzi, wito wa zabuni na utoaji wa mikataba.
“MSD imefanya hivyo kinyume cha Kanuni Na. 342 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 na Waraka Na. 4 wa Mwaka 2019 wenye Kumb. Na. EB/AG/485/01/Juz. XII/26 wa Novemba 23, 2019 uliotolewa na Hazina unaozitaka taasisi zote zinazofanya ununuzi kutumia TANePS kuanzia Januari Mosi, 2020,” amesema.
Pia amesema MSD ilifanya ununuzi katika mikataba minane kwa dola 3,956,145 za Marekani nje ya mfumo wa TANePS.
“Utekelezaji wa taratibu za zabuni nje ya mfumo wa kielektroniki unaweza kuzuia uwazi kutokana na upendeleo wakati wa kutathmini na kuchagua wazabuni, hivyo thamani ya fedha inaweza isipatikane katika zabuni husika,” amesema.