Baada ya miezi 10 bila ya wafanyakazi wa MSCL kupata mishahara, Serikali imeonekana kutaka kutekeleza ahadi yake ya kutaka kuifufua Kampuni hii. Serikali imefanya mabadiliko ya uongozi katika baadhi ya nafasi kwenye menejimenti, imekaribisha na inashindanisha makampuni mawili ya kigeni kwa lengo la kufanya ukarabati mkubwa kwenye baadhi ya meli na inakusudia kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria.

Serikali imebadilisha viongozi watatu katika nafasi ya Meneja Mkuu, Meneja rasilimali watu na Mwanasheria wa kampuni. Makampuni yaliyojitokeza kushindania zabuni ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati kwenye meli zilizotajwa hapo juu ni Korea Total Marine Innovation (KTMI). CO. LTD kutoka Jamhuri ya watu wa Korea na Kampuni moja kutoka Serikali ya China.

Meli zinazotegemea kufanyiwa ukarabati ni mbili katika Ziwa Victoria na moja katika Ziwa Tanganyika, meli hizo ni MV Victoria, MV Butiama na MV Liemba. Hii ni hatua inayotia moyo na kwa hili wafanyakazi wa MSCL  na wananchi wanaotegemea huduma ya usafiri kwa njia ya majini katika maziwa haya wameanza kurejesha matumaini na hivyo wanatoa pongezi kwa Serikali na maombi yao kwa Serikali ni kuhakikisha kuwa mchakato wa kupitisha na kusaini mkataba kwa kampuni itakayoshinda zabuni hii usicheleweshwe.

Wakati mikakati ya kushughulikia matengenezo ya meli imeanza kuonekana, sintofahamu ya mishahara kwa wafanyakazi inaendelea na Serikali imekaa kimya!

Ujio wa viongozi wa juu kwenye menejimenti nayo ni dalili njema kwani hiki kilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi. Haifahamiki madhumuni yaliyokuwepo katika uteuzi wa viongozi walioiongoza kampuni kwa hii miaka miwili yalikuwa ni yapi. Ukweli ulio wazi ni kuwa hii ilikuwa ni menejimenti dhaifu na ambayo haikuwa inazingatia maadili ya utumishi wa umma hata kidogo. Menejimenti hiyo ilikuwa haina uadilifu, ilikuwa imejaa ubaguzi na kimsingi ilikuwa inaipaka matope Serikali kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na mabadiliko hayo ya uongozi, tatizo bado lipo kwani viongozi wageni wamezungukwa na mchwa. Wafanyakazi wanaendelea kuifahamisha Serikali kupitia gazeti hili la JAMHURI kuwa kuna watu wameshika nafasi wasizokuwa na sifa nazo. Hawana sifa za kitaaluma, na hawana ubunifu wala uadilifu katika utendaji wao. Wengine wamechoka kiutendaji kwani walishastaafu na uwezo wao wa kufanya kazi ulishapungua. Hawana mbinu mpya zenye uwezekano wa kuleta tija katika operation za Kampuni.

Wafanyakazi hao wameshikilia vitengo nyeti. Mbali na kutokuwa na sifa, hawana uhusiano mwema na wafanyakazi wenzao kazini. Wamefikisha taarifa zao kwa Katibu Mkuu, uongozi wa Bodi ya Kampuni na mara zote wakubwa hawa wanatamba kuwa hakuna wa kuwafanya lolote.

Mbaya zaidi, wengine wamefikisha umri wa kustaafu lakini bado wanang’ang’ania kuendelea kuwa kazini. Kwa upungufu ulivyo wazi kiasi hiki, kuna sababu gani ya kuendelea kuwa na watu hawa kwenye nafasi hizi nyeti? Ipo harufu mbaya katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya kampuni kwenye meli pekee inayofanya kazi kwa sasa katika Ziwa Victoria (MV UMOJA). Idara zinazotajwa kuhusika na tatizo hili ni uongozi kwenye meli, idara ya masoko na idara ya uhasibu. Tunaiomba Serikali itupie macho katika eneo hili.

Wafanyakazi wanalazimika kutumia njia hii ili Umma wa Watanzania ufahamu kinachoendelea katika Taasisi hii, kwa hali ilivyo sasa ni dhahiri kuwa nia njema ya Serikali haitafanikiwa kama timu ya menejimenti katika nafasi nyeti walioshiriki kufilisi shirika haitabadilishwa. Hakuna sababu hata kidogo kwa Serikali kuendelea kubeba mizigo hiyo. Kuna Watanzania wengi wenye sifa, waadilifu na wenye uzoefu wa kutosha wanaoweza kuisaidia kukabili changamoto zilizopo kwenye kampuni hii ya Marine Services Company Limited (MSCL) nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwatumikia wananchi iweze kutimia.

Tunaomba tatizo la Seti mbili za mameneja waliosimamishwa kazi lishughulikiwe na limalizike kwani kuendelea kuwaweka pembeni bila kuwasikiliza kwa miaka miwili sasa ni kuendelea kuongeza mzigo kwa kampuni na Serikali pia.