Na Mwamvua Mwinyi, JammhuriMedia, Chalinze
Baadhi ya wanafunzi kutoka jimbo la Chalinze, mkoani Pwani, wamejitokeza katika kampeni ya msaada wa kisheria ya MAMA SAMIA, kutoa changamoto zinazowakabili katika malezi na matunzo ili kupata ushauri wa kisheria na ufumbuzi.
Vilevile, baadhi ya wananchi wameeleza kusogezwa karibu kwa huduma za kisheria kwenye kata na vitongoji ni mkombozi mkubwa.

Akizungumza na wanafunzi wa Shule ya sekondari Chahua na wananchi wa Mdaula Asia Festus, Wakili na mratibu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na maofisa wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MAMA SAMIA Halmashauri ya Chalinze, alieleza watakuwa Chalinze kwa siku tisa kwenye kata kumi na vitongoji 30.
Alisema, wanatembelea shule mbalimbali ili kuzungumza na wanafunzi kuhusu changamoto za ukatili wa kijinsia, malezi, na masuala ya kiusalama katika shule.
“Tunazungumza nao kwa usiri na urafiki mkubwa ili kusikiliza changamoto zao, kisha tunatoa ufumbuzi na elimu ya kisheria,” alifafanua Asia.

Kwa mujibu wake, kampeni hii imesaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kisheria, na kutoa huduma za bure za kisheria kwa wananchi.
Naye Philemone Mganga, Wakili kutoka Chama cha Wanasheria (TLS) na Mwenyekiti wa Haki za Binadamu mkoani Pwani, alieleza kampeni hiyo inasaidia makundi yote, hususan wanafunzi wanaokumbwa na masuala ya ukatili wa kijinsia na malezi, lakini wanakosa sehemu ya kusema.
Mganga alisisitiza ,huduma za kampeni hii zinapaswa kuwa za kisheria pekee, na hazipaswi kuhusishwa na masuala ya kisiasa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Jovin Bararata, aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kutambua umuhimu wa kutoa misaada ya haki na kisheria.
“Wapo wananchi wanaodhulumiwa haki zao, ikiwemo kwenye mashamba na nyumba zao, lakini kampeni hii itawawezesha kupata msaada na kuwafungua kiuchumi na kisheria,” alieleza Bararata.

Wanafunzi, akiwemo Abdallah Saidi Juma na Fatuma Rahim kutoka Shule ya Sekondari Chahua, walimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kampeni hiyo, kwani imesaidia wanafunzi wengi kupata msaada wa kisheria.
Kampeni hiyo itatoa huduma kwa wananchi kuanzia Februari 25 hadi Machi 5, 2025, mkoani Pwani, na itahusisha utoaji wa elimu kuhusu masuala ya kisheria, utatuzi wa migogoro, na ushauri wa kisheria.
Huduma hii inatolewa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na tayari imetekelezwa katika mikoa 19. Pwani ni mkoa wa 20 kunufaika na huduma hii.


