Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Vyuo binafsi nchini, Mahmoud Mringo amebainisha changamoto nne ambazo zinawakabili Wamiliki wa Vyuo binafsi vya Ufundi Stadi nchini.

Ambapo ametaja moja ya changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni gharama kubwa za mtaji wa kuanzisha vyuo vya Ufundi Stadi.

Amefafanua kuwa ili uanzisha vyuo hivyo ni lazima uwe na mtaji wa kiasi cha Sh. Bilioni moja.

Mringo ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu changamoto zinazowakabili walimiki wa Vyuo hivyo kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Ili kuweza kujenga Chuo kizuri cha VETA hapa nchini inahitaji uwe na gharama ya Sh. Bilioni moja li uweze kurudisha hiyo hela itakuchukua miaka 30 kama hela hizo umechukua Benki inamaana utazilipa Bilioni 10 ndani ya miaka 30.

“Kwahiyo mwanafunzi anayeingia katika shule yetu atalipa gharama halisi ya kusoma pamoja na zile Sh. Bilioni 9 zilizoongezeka. Badala ya kulipa Sh. Laki sita itabidi alipe Sh. milioni 1.2 ili zile laki sita zingine ziwe za kulipia mtaji, amesema na kuongeza kuwa:

“Kama tungepata Benki ambayo unaweza kulipa kwa gharama ndogo tungeweza kutoa elimu kwa nusu ya bei iliyopo sokoni sasa hivi,”.

Amebainisha changamoto nyingine ni Kodi, ambapo amesema kodi zote nchini zinakusanywa ili zikatoe Elimu ikiwemo ya VETA lakini wao wanatozwa tena kodi.

“Sisi watu binafsi katika kutoa elimu hii ya Mafunzo ya Ufundi Stadi, tunatozwa tena kodi kwahiyo gharama ya elimu ninayotoa ni pamoja na zaidi ya asilimia 20 ya kulipa kodi,” amesema.

Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi kutokupewa mkopo.

“Kwenye vyuo vikuu na vya kati mwanafunzi anapewa mkopo anaenda Chuo anachotaka lakini Kwenye VETA hakuna mkopo wowote. Kule Serikali wamelipiwa zaidi ya asilimia 90 kwahiyo analipa ada ndogo, kwetu akija lazima alipe gharama za mtaji, ada na kodi. Kumbuka huyu mtu amemaliza kidato cha nne hata elfu 20 ilikuwa ni ngumu kuitoa,” amesema.

Pia amezungumzia suala la mitaala ambapo amesema haimfundishi mtu kuwa mjasiriamali.

“Mitaala yetu inaendelea kung’ang’ania mtu afundishwe kuwa muajiriwa. Hatutaweza kuajiri watu wote kwa kutegemea mfumo mmoja wa Serikali. Kwahiyo ni lazima mitaala yetu kwanza ianze kumtambua mtu katika ujasiriamali wake. Dhana ya ujasiriamali ndo iwe dhana mama na ya Ufundi iwe shirikishi,” amesema.

Pia Mringo amezungumzia suala la kuwa na Bima ya Elimu ambapo amesema itasaidia mwanafunzi kusoma kwa ubora na mahali popote.

“Ukitaka kila mtu asome kwa ubora na kwa uendelevu lazima tuanzishe utaratibu mwanafunzi apate bima yake ya kusoma halafu aamue mahali ambapo anataka kusoma.

“Tunashawishi tutafute namna hela zipatikane wanafunzi wote wa Tanzania wapewe bima ya Elimu ili baadae kila atakayemaliza atakatwa na Benki zinaweza zikasaidia. Lazima zitafutwe hela kwenye Benki kubwa za dunia zenye riba chini ya asilimia 5 ili zitoe bima,” amesema.