“Tupo tayari kula hata nyasi, lakini lazima ndege ya Rais inunuliwe”

Haya ni maneno aliyoyatoa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Pesambili Mramba wakati wa Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa Bunge lilipoelekea kukataa ununuzi wa ndege ya Rais.

Massaburi: Mnafikiria kwa makalio

“Wabunge wa Dar es Salaam wanafikiri kwa kutumia makalio”

Haya ni maneno makali aliyoyatoa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Massaburi siku chache baada ya kuingia madarakani kama Meya wa Jiji hilo kisha akaingia katika mgogoro na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam alipoanza kudhibiti uovu na matumizi mabovu ya fedha za umma kwenye halmashauri. Siku hizi hasikiki tena.

Msuya: Beba msalaba wako

“Katika suala la kujiletea maendeleo kila mtu atabeba msalaba wake.”

Haya ni maneno aliyoyatoa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa David Msuya, alipokuwa akiwahamasisha wananchi kujiletea maendeleo. Kauli hii ilitafsiriwa kuwa amekiuka misingi ya Ujamaa na Kujitegemea na amejitanabaisha na ubepari.

Obama: Sikiliza hata mabaya

“Hamkunichagua kuwambia mnayotaka kuyasikia. Mlinichagua kuwambia ukweli.”

Haya ni maneno ya Rais Barack Obama aliyoyatoa wiki iliyopita wakati akiwashukuru wanachama wa chama chake kwa kumteua tena kugombea urais wa nchi hiyo Novemba, mwaka huu kwa tiketi ya chama cha Democrat. Kati ya aliyoyasema ni kuwa Marekani bado inayo kazi kufuta umasikini.