Veronica Simba-REA
Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Ijangala, kijiji cha Masisiwe, wilayani Makete, Mkoa wa Njombe, uko katika hatua za mwisho kukamilika.
Hayo yamebainika wakati wa ziara iliyofanywa na viongozi wa juu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Janet Mbene, Machi 15, mwaka huu.
Akiwa ameongozana na mmojawapo wa Wajumbe wa Bodi, Florian Haule pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, Mwenyekiti amekiri kufurahishwa na kuridhishwa na kazi nzuri ya utekelezaji wa Mradi huo ambao REA unaotarajiwa kuzalisha kilowati 360 za umeme pindi utakapokamilika.
Pamoja na pongezi, Mwenyekiti ameeleza kuwa anaamini kukamilika kwa Mradi huo unaotekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kufadhiliwa na REA pamoja na wadau wengine, kutatoa hamasa na kuchochea makundi na asasi mbalimbali za kijamii kuiga mfano wake hivyo kuwezesha umeme vijijini kuenea kwa kasi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu REA alikiri kuwa imani aliyoiweka kwa Taasisi hiyo ya Kanisa na kukubali kufadhili Mradi huo haikupotea bure kwani Mradi umetekelezwa kwa wakati na viwango vilivyotarajiwa.
“Katika hali ya kawaida, unatoa hela unaogopa kidogo, lakini niliwaambia matarajio yangu ni kwamba watafanya vizuri katika utekelezaji wa mradi huu wa nishati kama ambavyo wamefanya vizuri katika sekta za elimu na afya. Nawashukuru hawajaniangusha na nimefarijika sana,” ameeleza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi Mtendaji anayesimamia Mradi huo, Mchungaji Elikana Kitahenga pamoja na Msaidizi wa Askofu KKKT Njombe, Mchungaji Mathayo Sanga, waliishukuru REA kwa ushirikiano na mchango wake mkubwa tangu kuanza utekelezaji wa Mradi huo.
Walisema, REA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Mradi unatekelezwa siyo tu kupitia ufadhili wa fedha bali pia kwa viongozi na wataalamu wake kutembelea Mradi huo mara kwa mara kujionea maendeleo yake.
Mradi huo utakapokamila na kuanza uzalishaji, unatarajiwa kuuza umeme huo kwa Shirika la Umeme Tanzania ili uingizwe kwenye gridi ya Taifa ikiwa ni Mkataba maalumu baina ya pande hizo mbili.
REA, ikiwa ni taasisi inayoshughulika upelekaji nishati vijijini, hutumia mbinu mbalimbali za kutekeleza kazi hiyo ikiwemo kufadhili vikundi au hata watu binafsi wanaojihusisha na uzalishaji nishati vijijini ili kutimiza azma ya serikali inayolenga kuhakikisha maeneo ya vijijini yanafikiwa na nishati bora.