Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Dk. John Magufuli alizindua ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Mto Rufiji. Mradi huo wa kufua umeme wa Mto Rufiji, mkoani Pwani unatarajiwa kuzalisha megawatt 2,115, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi katika historia ya uzalishaji umeme nchini.
Mradi huu wa kufua umeme unatajwa kuweza kudumu kwa miaka 60 na utasaidia kuzalisha umeme wa kutosha utakaosaidia Tanzania kutekeleza malengo yake ya maendeleo endelevu.
Kuna mengi yatakayoambatana na ujenzi wa mradi huu. Kwa mfano, tayari kuna maagizo kuwa mkandarasi anatakiwa kutumia wafanyakazi walioko karibu kwa kazi ambazo si za kitaalamu. Ajira zinatarajiwa kutolewa kwa wenyeji wa maeneo ya mradi, kwa maana ya mikoa ya Morogoro na Pwani. Kwa ujumla, mradi huu unaambatana na fursa nyingi katika ujenzi wake utakaodumu kwa miezi 36.
Lakini pamoja na uzinduzi huo, hotuba ya rais iliambatana na maagizo kadhaa kwa watendaji wake, hasa wa ngazi ya wizara, kuhusu eneo la uwindaji la Selous ambalo limezunguka mradi huo mkubwa wa umeme likiwa na urefu wa kilomita za mraba 57,000.
Moja ya maagizo hayo ni kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kutenganisha eneo la uwindaji (hunting block) Selous kwa kutengeneza hifadhi ya taifa itakayoitwa Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Julius Nyerere.
Kwa mujibu wa rais, maeneo ya uwindaji wa wanyama yanafikia 47 katika Mbuga ya Wanyama ya Selous, hivyo Wizara ya Maliasili na Utalii lazima itenge eneo la hifadhi na la uwindaji ili kuimarisha utalii na kuvutia watalii wengi katika mbuga hiyo.
Rais Magufuli amesisitiza kuwapo kwa utaratibu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia maeneo yenye vitalu vya uwindaji ili kuhakikisha serikali inafaidika na maeneo hayo. Zaidi ya hapo, aliagiza barabara ya kutoka Fuga – kilomita takriban 60 kwenda mahali ambapo mradi unajengwa ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami ili kufungua sekta ya utalii katika Mbuga ya Wanyama ya Selous.
JAMHURI tunaamini kuwa nia ya utekelezaji wa mradi huu ni njema na kimsingi inalenga kulinufaisha taifa. Hata hivyo, tunasisitiza uadilifu kwa wahusika wakati wote wa utekelezaji wa mradi huu. Lakini mbali na suala la uadilifu na uzingatiaji wa sheria za nchi, tunatarajia taasisi za serikali, wadau binafsi na wananchi kwa ujumla wataendelea kutunza mazingira, kwa sababu uhai wa mradi huu unategemea sana uimara katika utunzaji wa mazingira yetu ambayo ndiyo chanzo cha mvua na mvua ndiyo chanzo cha maji yanayotumika katika uzalishaji wa umeme katika mradi huu. Tusonge mbele kwa kutanguliza masilahi ya taifa.