Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Waandishi wa habari wameaswa kutumia nguvu ya kalamu zao kuandika taarifa za mradi wa Shule Bora ,mpango ambao unalenga kuweka mikakati na kutafuta suluhisho kwa watoto wa makundi maalum ,wakike na wale wa kiume wanapata elimu iliyo kwenye mazingira bora.
Waandishi hao wametakiwa kushirikiana na Serikali na vitengo vya elimu ili kuweza kupata taarifa mbalimbali na zilizo sahihi.
Katibu Tawala Mkoani Pwani, Zuwena Omari akifungua semina ya uhamasishaji wa mradi wa Shule Bora kwa wahariri na wasimamizi wa vyombo vya habari mkoani humo ,alieleza wanaendelea kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na vyombo vya habari ili mradi ulete tija .
“Hakuna asiyejua nguvu ya kalamu za waandishi wa habari,kwa kuandika taarifa zinazoaminika kwenye kampeni za maendeleo nchini,Sisi Kama mkoa tutaimarisha mahusiano na vyombo vya habari ili kuhakikisha mradi unaleta mafanikio “alifafanua Zuwena.
Akielezea mradi ,Zuwena alieleza umefadhiliwa na mfuko wa Ukaid unalenga kuunga mkono uboreshaji wa elimu msingi Tanzania kwa miaka sita ,katika Halmashauri 67 na itahusisha watoto milioni 3.8 katika mikoa 9 inapotekelezwa mradi ikiwemo mkoa wa Tanga ,Pwani, Dodoma, Singida, Kigoma,Katavi ,Simiyu ,Mara na Rukwa.
“Utekelezaji wa mradi umelenga kuboresha ufundishaji kwa walimu, kuboresha elimu jumuishi kwa makundi ya watoto wenye mahitaji maalum , kuboresha ujifunzaji kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mfumo wa usimamiaji wa sekta ya elimu katika kuhakikisha kila kiongozi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake ili kufikia adhma iliyokusudiwa”alisema .
Ofisa elimu mkoa wa Pwani,Sara Mlaki alieleza mradi wa Shule Bora ulizinduliwa Kitaifa na Kimataifa mwaka 2021 katika shule ya msingi Mkoani iliyopo Pwani .
Alieleza kwasasa zipo kazi zinazoendelea kufanywa kulingana na matakwa ya mradi ikiwa ni sanjali na uboreshaji wa ufundishaji darasa la 1,2 , kuimarisha usimamizi wa shule na elimu katika Mamlaka za Serikali ya mitaa ambapo wameshaanza kuona matokeo chanya kwa kupanda kwa ufaulu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa habari Mkoani Pwani, Ally Hengo alishukuru waandishi kuachiwa mlango wazi kupata taarifa ama kupewa ufafanuzi juu ya masuala ya elimu kupitia maafisa habari kwani changamoto kubwa wanayoipata ni kukosa taarifa kwa wakati.